Tuesday 22 October 2013

Kagasheki amkabidhi IGP Mwema kigogo wa polisi

22nd October 2013
Waziri wa Maliasili na Utalii,Balozi Khamisi Kagasheki
 
Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki, amesema sakata la Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO), Duwan Nyanda, anayetuhumiwa kuhujumu operesheni tokomeza majangili kwa kutorosha majangili wawili raia wa kigeni, linashughulikiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema.

Waziri huyo alisema hayo jana mara baada ya kutoka katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Vyombo vya Utangazaji, vilivyopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, unaofanyika jijini hapa.

Alisema operesheni ya kupambana na ujangili ni kubwa na inakumbana na vikwazo vingi kutokana na baadhi ya watumishi ndani ya Jeshi la Polisi na serikalini kushirikiana na majangili wa ndani na nje ya nchi kwa tamaa ya kujitajirisha.

"Kuhusu suala la RCO Arusha nimelifikisha kwa bosi wake IGP na analishughulikia vizuri  na tena lipo katika hatua nzuri, tunasubiri," alisema Kagasheki.

Aidha, aliviomba vyombo vya habari kusaidia kuelimisha wananchi madhara ya ujangili, ili waelewe na kuachana na suala hilo kwa faida ya Taifa na kizazi kijacho.

Alisema kupitia ujangili huo nchi imepata aibu kubwa na kuichafua nchi kwa kiasi kikubwa, kitu ambacho viongozi wa serikali hawako tayari kuvumilia tatizo hilo liendelee.
"Lakini katika Operesheni hii hakuna atakayepona wote wanaohusika watakamatwa na tayari wapo watu wamefikishwa mahakamani na wengine wapo nje kwa dhamana," alisema Balozi Kagasheki.

Pia alisema katika operesheni hiyo wameweka njia za kuwezesha upatikanaji wa habari za operesheni zinapatika kwa urahisi na kuwafikia wanahabari, ili kuieleza jamii kinachoendelea.

Oktoba 18 mwaka huu, Balozi, Khamisi Kagasheki, alimtuhumu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO), Duwan Nyanda kuhusika na kuhujumu operesheni tokomeza majangili kwa kuwatorosha majangili wawili raia wa kigeni toka Saud Arabia.
 
CHANZO: NIPASHE