Tuesday 22 October 2013

Mulugo: Waliokosa mikopo vyuo vikuu wajilaumu wenyewe

22nd October 2013
Philipo Mulugo
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema wanafunzi waliokosa mikopo kwa ajili ya masomo ya vyuo vikuu wanapaswa kujilaumu wenyewe kwa kufanya makosa wakati wa kujaza fomu za kuombea mikopo kama taratibu na sheria za  Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) zinavyotaka.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philipo Mulugo, alisema  hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya tisa ya pamoja ya vyuo na shule za Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani ambayo jumla ya wahitimu 800 walitunukiwa vyeti.

Alisema baadhi ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu waliokosa mikopo mwaka huu wamekuwa wakiitupia lawama serikali bila kutambua kuwa wao ndiyo walifanya makosa wakati wa kujaza fomu hizo na hata walielekezwa  wazirekebishe hawakufanya hivyo kwa wakati.

Alisema wanafunzi hao lazima watambue kuwa pamoja na kwamba waliomba mikopo, idadi kubwa ya waombaji walikuwa na sifa za kupata mikopo lakini serikali ilikuwa inaangalia zaidi uhitaji kwenye masomo maalumu hasa fani zenye upungufu wa wataalamu.

Alitaja baadhi ya sababu zilizowafanya wanafunzi kukosa mikopo hiyo ni waombaji kukosea majina na vitu vingine vidogo vidogo na walipotangaziwa kwenye vyombo vya habari warudi kurekebisha fomu zao hawakufanya hivyo.

“Wao wanailaumu tu serikali lakini wengi wao walikosea kujaza fomu za mikopo, wengine hawakuweka picha zao kwenye fomu, hawakuzisaini na wengine hawakuzipeleka mahakamani zikasainiwe na hakimu, tulipowaambia rekebisheni makosa hayo hawakufanya kwa wakati ikabidi wachukuliwe wengine ambao nao walikuwa na vigezo,” alisema.

Mulugo alisema waliokosea kujaza fomu hizo walikuwa 6,000 lakini waliorudi kufanya marekebisho walikuwa ni 3,000 na wengine 2,000 walikuwa na vigezo lakini wamekosa kutokana na fedha kutotosheleza.

Alisema kutokana na ufinyu wa bajeti ni vigumu kwa serikali kutoa tamko kama kuna fedha nyingine zitakazopatikana kwa ajili ya kuwakopesha waliokosa.
 
CHANZO: NIPASHE