Monday 2 September 2013

Yanayomkuta Bo Xilai nchini China yanakumbusha ya Jiang Qing

Posted  Jumapili,Septemba1  2013  saa 14:15 PM
Kwa ufupi
Ilichukua miaka minne kwa kundi hilo kufikishwa mahakamani. Lakini kwa Wachina muda huo haukuwa tatizo kwani kiu yao ilikuwa ni kujua ukweli katika hilo.

Beijing (CNN) – Kesi ya Bo Xilai, mwanamume ambaye nyota yake ilikuwa iking’aa na kutajwa kuwa kati ya watu 25 wenye nguvu nchini China sasa anaelekea ukingoni.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba hata kama atashinda, lakini heshima aliyokuwa nayo, ambayo ingemwezesha kushika madaraka haitakuwepo tena, hivyo ndoto zake kisiasa zitakuwa zimekoma kwa kuwa nchini humo hakuna sheria itakayomruhusu kuwania uongozi na pengine ndiyo hasa lilikuwa lengo la mlolongo mzima wa kesi aliyonayo.
Huku kesi hiyo ikitawaliwa na visa vya mapenzi, ulaghai na ushahidi wa video, imekuwa na mvuto wa kipekee na kubatizwa jina la ‘Kesi ya Muongo’.
Ingawa inatajwa kuendeshwa kwa uhuru na haki, picha chache na video zilizohaririwa zimekuwa zikirushwa mtandaoni na mahakama inayosikiliza kesi hiyo.
Watu wachache waliopata bahati ya kuhudhuria kesi ya Bo, wanasema kuwa kama kila kinachoendelea katika mahakama hiyo kingewekwa wazi, angekuwa na nafasi kubwa ya kushinda, lakini imekuwa ndivyo sivyo.
Bo anakumbusha kesi kama hiyo iliyowahi kutokea katika miaka ya 80 iliyojulikana kama ‘Gang of Four’ iliyowahusisha vigogo wa nchi hiyo wanne.
Kundi hilo la watukutu likiongozwa na Jiang Zedong aliyekuwa mjane wa Mao na washirika wake watatu ilivuta hisia za watu duniani kote kutokana na namna ilivyoendeshwa.
Qing ambaye alijipatia umaarufu na kupata wadhifa wa juu katika Chama cha Kikomunisti cha China kabla ya kuangushwa akituhumiwa kutaka kufanya mapinduzi.
Mwezi mmoja baada ya mumewe kuuawa mwaka 1976, kundi hilo la watu wanne na washirika wao wengine walikamatwa kwa makosa ya uhaini, pia kuhusishwa kutaka kumuua Mao.
Ilichukua miaka minne kwa kundi hilo kufikishwa mahakamani. Lakini kwa Wachina muda huo haukuwa tatizo kwani kiu yao ilikuwa ni kujua ukweli katika hilo.
Zaidi ya watu 600, wengi wakiwa viongozi wa Serikali, wawakilishi wa jamii , waandishi wa kuaminika na ndugu wa watuhumiwa, walikuwa wakihudhuria kesi hiyo.
Kesi hiyo ilikuwa habari kubwa duniani kote, iliripotiwa na nchi mbalimbali kwa mapana. Wakati ule China ndiyo kwanza ilikuwa imetoka katika utawala wa kidikteta wa Mao.

Aidha, kesi hiyo ilidumu kwa miezi miwili. Kwa waandishi wa nje walitegemea habari kutoka kwa waandishi walioaminiwa na Serikali.
Miongoni mwa mambo yaliyovutia katika kesi hiyo ni pale, Jiang Qing alipojitetea kuwa kila alichokifanya ilikuwa ni kutii matakwa ya Mao, akijifanaisha na mbwa.
Jiang alipiga kelele akisema: “Nilifanya yote kwa ajili ya Mao, mimi nilikuwa mbwa wake niliyemng’ata kila aliye mbele yangu kwa maelekezo ya bosi wangu.”
Katika hotuba yake ya mwisho, ambayo ilichukua muda wa saa mbili, mwanamke huyo aliyekuwa na umri wa miaka 66 alisema yuko tayari kufa kwa sababu kila alichokifanya ilikuwa ni kwa ajili ya kumuenzi mume wake.
Mwanzoni mwa mwaka 1981, Madame Mao, kama alivyokuwa akijulikana alihukumiwa kifo, lakini miaka mkichache baadaye alijiua wakati akiwa katika kifungo cha nyumbani.
Biashara kama kawaida
Bado kuna mambo hayajabadilika, hata baada ya kubadilisha mfumo wa mahakama katika miaka ya karibuni.
Mfano mwaka 1981, mahakama iliibatiza jina la kesi ya Biao na wenzake kwa kuuita, “ Kesi ya Lin Biao na Jiang Quing kundi lililotaka kufanya mapinduzi.” Kichwa hicho cha habari kinamhukumu mtuhumiwa moja kwa moja, hata kabla ya kesi kuanza kusikilizwa.
Miongo mitatu baadaye, hakuna kesi kubwa iliyoashiria kuwa mtuhumiwa anaweza kushinda. Unaposikia kesi ikianza kuunguruma, tayari inakuwa imeshatoa hukumu. Katika kesi ya Bo, wachambuzi wa mambo ya siasa wanasema uongozi mpya wa Rais Xi Jinping unataka kujihakikishia kuwa unashinda bila kubaki na ‘damu mikononi’.
Kwa kuwa Bo anagomea kukiri kile ambacho Serikali inataka afanye, suala hilo zito ndilo linaloiweka njia panda kesi hiyo katika kutoa hukumu.
Imetafafsiriwa na Julieth Kulangwa kutoka cnn.com

source: Mwananchi