Kwa ufupi
Mbali na kufikisha kilio cha wajane, anasema
ziara hiyo ina lengo pia kuhamasisha utalii wa ndani kwa kutembelea
maeneo ya kihistoria kama hayo yakihusisha shughuli za kiutamaduni.
Japo ujane unachukuliwa kama hali ya ukiwa
kutokana na mwanamke kufiwa na mumewe, lakini hali hiyo sasa kwa
wanawake imekuwa changamoto nchini katika kujiletea maendeleo.
Grace Mahumbuka ni mjane anayeishi wilayani
Karagwe mkoani Kagera, ambaye sasa ameamua kuanzisha kikundi cha wajane
akiwa na ndoto ya kuwangusha wajane nchini ili kujiletea maendeleo ya
kiuchumi na jamii.
Mwanamke huyo ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu
la Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT), ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
Wajane katika Wilaya ya Karagwe na Kyerwa (UWK) ulio na jumla ya
wanachama 685.
“Kuwa mjane siyo kubweteka, nimeamua kuwaunganisha
wanawake wajane ili tujiletee maendeleo. Tangu mume wangu alipofariki
nimekuwa na mtazamo wa kuwatafuta wanawake walio kama mimi ili tuungane
katika kupambana na umasikini,” anasema Grace na kuongeza:
“Kwa sasa tuna mradi wa ushirika wa kuweka na kukopa (Saccoss) unaotuwezesha kukopa na kufanya miradi ya maendeleo.”
Anafafanua kuwa, mwamko wa kutetea wanawake wajane
umeelekezwa pia katika mabadiliko ya Katiba, akieleza kuwa wamepeleka
maoni yao kwenye Mabaraza ya Katiba ili yaingizwe kwenye Rasimu ya
Katiba.
“Rasimu ya Katiba haitambui wanawake wajane, sana
sana inazungumzia haki za wanawake kwa jumla katika ibara ya 46.
Tunataka walau kuwe na ibara ya 46 (b) ili kundi hili nalo likumbukwe.
Tulipeleka maoni yetu na sasa tunatarajia kuwa yataingizwa kwenye Katiba
Mpya,” anasema Grace.
Anaongeza: “Kwa kuwa wajane tunajitegemea wenyewe
katika shughuli zetu, Katiba itoe msamaha walau wa kodi kwenye biashara
au unafuu kwenye kipato chetu ili tujimudu kimaisha.”
Kuhusu mikakati mingine, Grace anasema kuwa sasa
wanapanga ziara ya kumtembelea Mama Maria Nyerere, ambaye pia ni mjane
nyumbani kwake Mwitongo Butiama mkoani Mara, ikiwa ni sehemu ya
kuhamasisha umoja wa wanawake wajane nchini.
“Juhudi zetu hazitafanikiwa bila kumshirikisha
mjane mwenzetu aliye na hadhi kubwa yaani, Mama Maria Nyerere. Yeye
anajua uchungu wa kuwa mjane, hivyo atatusaidia kuwahamasisha wanawake
wengine na Serikali kwa jumla. Tutatumia ziara hiyo pia kuzuru kaburi la
Mwalimu Nyerere na kufikisha kilio cha wajane nchi nzima,” anasema.
Anasema kuwa katika mikakati yao wameushirikisha uongozi wa Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera, Bunge na Serikali Kuu.
“Tunataka ziara hiyo iwe na siku maalumu ya
maadhimisho ya kazi za wajane na tumemwomba Waziri Mkuu Mizengo Pinda
kuwa mgeni rasmi. Tumewashirikisha pia Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Spika Anna Makinda. Hayo
yote yako kwenye maandalizi ili kuhakikisha kuwa ziara yetu inafanikiwa
kuleta mwamko kwa wanawake wajane nchini,” anasema.
Mbali na kufikisha kilio cha wajane, anasema ziara hiyo ina
lengo pia kuhamasisha utalii wa ndani kwa kutembelea maeneo ya
kihistoria kama hayo yakihusisha shughuli za kiutamaduni.
Mbali na kutembelea kwa Mwalimu Nyerere, Grace
anasema kuwa pia watatembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa lengo
hilo hilo la kuhamasisha utalii wa ndani.
“Tunaandaa vazi la asili za mwanamke wa Tanzania
ambalo litaonyeshwa wakati wa ziara hiyo. Huo ni mchango wetu tulioutoa
kwenye kamati ya Taifa ya vazi la Taifa. Lengo ni kuwa na vazi la
kitaifa siyo kuendeleza mavazi ya tamaduni za wengine,” anasema na
kuongeza:
“Tumeishirikisha Mamlaka ya Hifadhi za Taifa
(Tanapa) katika kuhamasisha utalii wa ndani, pia kutakuwa na wasichana
20 watakaoshiriki katika maonyesho hayo ya mavazi.”
Kazi nyingine ya sanaa ambayo itafanywa na kikundi
hicho wakati za ziara hiyo Butiama ni kuimba nyimbo zilizoko kwenye
albamu waliyoiandaa.
“Tunazo nyimbo tisa katika albamu yetu ambazo
zitazinduliwa Butiama baadhi zikiwa ni Umoja wa wajane ulipoingia,
Kilimo kwanza, Mama na Tanzania nakupenda. Nyimbo hizo ni moja ya kazi
zetu katika kikundi,” anasema.
Akizungumzia malengo ya baadaye, Grace anasema
kuwa wanakusudia kufungua chuo cha sanaa watakachokitumia kuwafundisha
watoto yatina sanaa za mikono na maonyesho.
“Tunaomba Serikali na wadau wengine watuunge mkono ili kufanikisha jitihada za wanawake kujikomboa,” anasema Grace.
source: Mwananhi
source: Mwananhi