Kwa ufupi
Dar es Salaam. Pato la Taifa (GDP)limeongezeka
kwa asilimia 7.5 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu
ikilinganishwa na asilimia 7.4 ya kipindi kama hicho mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi wa Uchumi katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Morrice
Oyuke, imesema kuwa katika kipindi hicho sekta zote za uchumi zilifanya
vizuri, isipokuwa sekta ya madini iliyoshuka kutokana na bei ya madini
katika soko la dunia kushuka.
Oyuke alibainisha kwamba katika kipindi hicho cha
miezi mitatu, pato la taifa lilifikia Sh4. 5 trilioni tofauti na Sh4.2
trilioni kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Alisema sekta ya uchukuzi na mawasiliano ilikuwa
hadi kufikia asilimia 22.2, wakati huduma za usafiri wa treni ya abiria
iliyoanzishwa jijini Dar es Salaam mwishoni mwaka jana, ikichangia
ongezeko hilo.
“Shughuli za kilimo na uvuvi zilifikia asilimia
1.4 ikilinganishwa na asilimia 0.4 ya kipindi kama hicho mwaka jana,”
alisema mkurugenzi huyo.
Alisema shughuli za uzalishaji viwandani zilikuwa hadi kufikia asilimia 8.6 ikilinganishwa na asilimia 5.7 mwaka uliopita.
“Ukuaji katika sekta hiyo ulichangiwa na kuongezeka la uzalishaji wa vinywaji, bidhaa za tumbaku na sukari,” alinena .
Alisema mafuta na gesi vilichangia ongezeko la
ukuaji wa nishati ya umeme kwa asilimia 6.3 ikilinganishwa na asilimia
5.1 katika mwaka jana.
Mkurugenzi huyo alisema shughuli za uchimbaji
madini, mawe na kokoto zilishuka kwa asilimia 4.7 ikilinganishwa na
asilimia 23.8 mwaka uliopita.