Posted Jumapili,Septemba1 2013 saa 14:11 PM
Kwa ufupi
Mada hii ilianza Jumapili iliyopita; Iliishia
kutoa amelezo kuhusu haki ya mtoto kuishi na baba na mama, bila kujali
wametengana au la.
Kutokana na sababu mbalimbali, wazazi wengi
wanaishi sehemu tofauti. Ikiwa utengano huo unatokana na makubaliano
yenye lengo la kunufaisha familia husika; mara nyingi huwa hakuna tatizo
kwa mtoto.
Matatizo hutokea endapo utengano unatokana na
uhusiano ulioleta mtoto au watoto umeshindikana kuendelea. Yaani wazazi
kutengana au kuachana.
Iwapo mmoja kati ya wazazi waliotengana hana
busara, huruma wala upendo wa dhati kwa watoto husika, huanza kuonyesha
ubabe kwa kuzuia upande wa pili kuishi au kuwa karibu na mtoto wake.
Kuzuia huko kunaweza kufanywa kwa maneno, vitendo
au kwa mzuiaji kujenga mazingira yasiyo rafiki kwa mwenzi wake kuishi au
kuwa karibu na mtoto wake. Jambo hili halikubaliki kwa sababu
linamwathiri zaidi mtoto.
Kwa ufupi, ili mtoto aishi na baba na mama yake,
lazima kila aliye mzazi atambue kuwa bila mwenzi wake, mtoto
asingepatikana, hivyo awe tayari kumwezesha mtoto kuishi karibu, hata
kama siyo pamoja na mzazi wake mwingine.
Ili mzazi afanikiwe katika hilo, hana budi
kudhibiti tabia za uroho, uchoyo, wizi, uzinzi, ulevi wa kupindukia,
kutotekeleza majukumu yake kwa familia, ubaguzi kwa watoto na ubinafsi.
Tabia hizi ni kiini cha mtu kushindwa kutekeleza haki za mtoto, hata
kama anazifahamu vizuri.
Wajibu wa mtoto kwa wazazi
Kila mtoto analo jukumu la kuheshimu wazazi pamoja na waangalizi wake wote, kama wao wanavyotakiwa kumheshimu.
Kuna wakati mzazi anaweza kutamani kutokuwa na
mtoto, kutokana na utukutu wa mtoto wake. Pengine amejitahidi kwa kadiri
ya uwezo wake kumfunza mtoto namna ya kuishi vizuri, lakini bahati
mbaya mtoto mwenyewe siyo msikivu; watoto lazima watoe ushirikiano kwa
wazazi wao.
Jambo hili lipo tangu enzi, ndiyo maana hata
wahenga walitoa usemi kwamba; “Samaki mkunje angali mbichi,” au
“Ukichelea mwana kulia utalia wewe,” na nyingine nyingi, lengo likiwa
kuwaadharisha wazazi kutolegea na kuacha watoto waendelee na tabia
zisizokubalika.
Mtoto asiyezingatia heshima, asitegemee kuwa
wanaomlea watazingatia baadhi ya haki zake; kwa sababu ili arejeshwe
kwenye mstari uliyonyooka, pamoja na mbinu nyingine ni kufinya baadhi ya
haki zake.
Mathalani kumzuia kushiriki michezo kwa kipindi fulani, hadi
atakapobadili tabia isiyokubalika kwa mujibu wa mazingira na jamii
aliyomo.
Kila mtoto anao wajibu wa kusaidia wazazi, walezi,
ndugu na jamaa zake wote walio katika uhitaji wa msaada ulio ndani ya
uwezo wake. Kwa kutimiza wajibu huu, mtoto husika ataondokana na tabia
kadhaa mbaya mathalani uvivu, dharau, kujikweza na kutokuwa na
ushirikiano na wengine.
Wajibu wa mtoto kwa jamii
Mtoto ni mwanachama kamili wa kila jamii, hivyo
anapotazamwa kijamii wajibu wake unabadilika kwa kuongezeka kutegemeana
na umri wake.
Lakini ili atekeleze ipasavyo wajibu wake ni
lazima awe ametendewa haki ya kueleweshwa vizuri na kwa ufasaha juu ya
masuala yanayoihusu jamii husika, kama vile elimu kuhusu Katiba ya taifa
lake.
Kila mtoto anawajibu wa kufahamu na kutii
taratibu, kanuni na sheria za nchi yake; kuthamini na kuzingatia
utamaduni, mazingira asilia pamoja na kanuni zinazolenga kudhibiti
mienendo ya tabia zinazotawala mahali pa kuishi, kazi na shuleni.
Wajibu wa watoto kwa wenzao
Adabu ya mtoto inatakiwa kuonekana siyo tu kwa
wakubwa bali hata kwa watoto wenzake. Hatakiwi kutumia kisingizio cha
kutetea au kutumia haki zake za kisheria au kikatiba, kudhuru wengine,
(mtoto au mtu mzima)
Itaendelea wiki ijayo…
source: Mwananchi
source: Mwananchi