Kwa ufupi
Licha ya kuwepo katika kundi hilo, msanii huyo
amepewa uhuru wa kufanya kazi zake binafsi na hivi sasa ameonyesha
kufanya kazi nzuri inayopendwa na wengi, hasa anapokuwa katika majukwaa.
“Ukihitaji kufanya kazi na Meninah au kupata
taarifa za ndani za msanii huyu, huna sababu ya kuhangaika, bali mtafute
kaka yangu Atick maarufu kwa jina la Tik tik.”
Hiyo ni sehemu ya maelezo ya Meninah na ndiyo
msimamo wa staa huyo wa Bongo Star Search 2012, Meninah Abdulkarim Atick
anayewika na vibao kama ‘Dream Tonight na Shaghalabaghala’, akiamini
kuwa kumilikiwa ndugu yake wa damu kutamfanya aweze kuwa huru na imani
ya kipato chake, tofauti na mtu mwingine.
“Meneja wangu ni kaka yangu, sidhani kama ninaweza
kumilikiwa na mtu mwingine kwani sina imani. Unajua ndugu yako anaweza
kuthamini kile ukipatacho na siyo mtu mwingine kwani hana uchungu na
wewe. Kaka yangu amenisaidia sana mpaka hapa nilipofika, yeye ndiye
aliyekuwa akinipa mwongozo, hivyo namwamini kunisimamia,” anasema.
Meninah anasema kuwa kufanya kazi na mtu baki
kumewasababishia wasanii wengi kushindwa kusonga mbele kimaendeleo, hata
mameneja wao kuwapoteza katika soko la muziki mara wasanii wanapodai
masilahi yao.
“Ni ngumu kufanya kazi na mtu baki,lawama tu,
mtatofautiana mwisho wa siku. Kaka yangu ananipenda na ataweza
kunisimamia vizuri. Idadi kubwa ya wasanii wanapotea kutokana na meneja
husika, wengi hawawasimamii kama inavyopaswa, ikitokea wakatofautiana ni
rahisi kumharibia msanii kazi yake. Ni wachache huachana kwa amani,”
anasema Meninah ambaye ni mtoto wa mwisho katika familia ya Abdulkarim
Atick.
Licha ya kufanya muziki akiwa mwenyewe, Meninah
pia anaunda Kundi la Shosteez akiwa sambamba na Nuru Yogo na Salma
Mahin, kundi lililoundwa na prodyuza maarufu Lamar.
Akizungumzia kundi hilo, Meninah anasema: “Kundi
letu bado ni changa na tangu tuliunde tayari tumefanikiwa kuachia wimbo
wa ‘On The Show’ sambamba na video ya wimbo huo. Lakini wiki tatu
zilizopita tumeachia wimbo mwingine ‘Nifikirie’ na umepokelewa vizuri tu
na mashabiki.”
Anasema kuwa hakuwahi kufahamiana na wasichana
hao, bali aliunganishwa na Lamar aliyekuwa akitafuta vipaji kutoka kwa
wasanii wanaojua kuzitumia sauti zao.
“Sikuwahi kufahamiana na Salma wala Nuru, ila
Lamar ndiye aliyetuunganisha. Nashkuru, huko ninapata uzoefu mkubwa tu
ambao nahisi nitaweza kuutumia sehemu yoyote. Hakuna kitu kizuri kama
kufundishwa kazi na mtu aliyewaongoza wasanii wakubwa walioshika chati
za juu hapa nchini.”
Licha ya kuwepo katika kundi hilo, msanii huyo
amepewa uhuru wa kufanya kazi zake binafsi na hivi sasa ameonyesha
kufanya kazi nzuri inayopendwa na wengi, hasa anapokuwa katika majukwaa.
“Nashkuru Mungu nina pumzi ndiyo sababu ninapata
kazi nzuri. Alhamdulilah, naweza kupata mahitaji yangu binafsi kwani
sasa simwombi tena mama pesa ya saluni, vocha na vitu vingine vidogo
vidogo.”
Hata hivyo, Meninah hataki kuweka wazi ni kiasi
gani cha fedha analipwa kwa shoo moja; “Kwa kweli siyo rahisi kusema,
kwani huwa sipendi. Lakini shoo Napata, ila bado ni zile za chini huku,
ila nina imani kwamba ipo siku nitafanya shoo kubwa zaidi nje ya nchil
Ila, watu watambue kuwa Meninah siyo msanii ghali, bali ni makubaliano
kati yangu na promota anayetaka kunipa kazi.”
Kwa sasa ameachia wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la
Shaghala bhagala, unayofanya vizuri kwenye vituo mbalimbali vya redio,
huku akiwa mbioni pia kutoa video ya wimbo huo chini ya prodyuza, Nash
Designer.
Maisha yake halisi
Meninah ni mtoto wa tatu na wa mwisho kuzaliwa
katika familia yake, huku Atick ‘Tik tik’ ambaye ndiye meneja wake akiwa
mtoto wa kwanza kuzaliwa.
Msanii huyu ni mwanafunzi katika Shule Kuu ya
Uandishi wa Habari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC), akisomea
Mawasiliano ya Umma.
Anasema kuwa licha ya kuwa na mambo mengi ya
shughuli zake za kimuziki, bado anaweza kuhimili mikiki mikiki ya shule,
pamoja na kutekeleza majukumu anayopangiwa na wazazi wake.
“Awali nilikuwa naona kama nataka kuchanganya
mambo, lakini namshukuru Mungu kwani kwa sasa akili yangu imetulia. Mimi
ni mwanamuziki nina majukumu mengi, kila wiki nakuwa na safari za
mikoani kwa ajili ya shoo, bado natakiwa kuhudhuria darasani,” anasema.
Meninah anaongeza kuwa licha ya majukumu
aliyonayo, anahakikisha anapata muda sahihi wa kusaidia wazazi wake
katika kazi mbalimbali nyumbani. “Najipanga sana, nakabiliwa na mambo
mengi,” anasema.
Aidha amewashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono katika kazi yake, vilevile anawaomba mashabiki kuipokea kazi yake.
Msanii huyo anayeishi na wazazi wake Mikocheni
jijini Dar es Salaam, anasema kwamba licha ya yeye kuwa ni mwanamuziki
anajitahidi kuwa katika maadili aliyofundishwa na wazazi wake, ikiwa ni
pamoja na kujisitiri kimavazi.
source: Mwananchi
source: Mwananchi