Na Florence Majani, Mwananchi
Posted Septemba21 2013 saa 12:42 PM
Posted Septemba21 2013 saa 12:42 PM
Kwa ufupi
Wanaume wanaotakiwa kuchangia mayai hupelekwa katika chumba maalumu na kutakiwa kujichua
Kadri matatizo ya uzazi yanavyoendelea kukithiri
duniani kote, wataalamu wa afya nao wanaendelea kuvumbua njia
mbalimbali za kuwasaidia wenye matatizo ya kukosa watoto.
Katika harakati hizo Kliniki ya Upandikizaji ya
Dar es Salaam, (Dar IVF and fertility clinic) wameanzisha huduma ya
kununua mbegu za kiume na mayai ya wanawake, kwa ajili ya kutoa huduma
ya uzazi kwa njia ya upandikizaji au IVF.
Gazeti hili lilipiga simu katika kliniki hiyo
kutaka kujua iwapo linaweza kuchangia mayai na daktari aliyekuwapo zamu
alijibu; “inawezekana”.
Daktari huyo ambaye hata hivyo alisema kliniki
hiyo bado haijaruhusiwa kujitangaza katika vyombo vya habari, alisema
kwa sasa kifaa cha kuhifadhi mayai (ya mwanamke) hakipo ila kifaa cha
kuhifadhi mbegu za kiume kipo na wanapokea wachangiaji wanaotaka kuuza
mayai hayo kwa makubaliano rasmi.
“Ukija tutajadiliana bei, kwa sasa hatuna bei
rasmi, lakini nadhani ukija tutakubaliana. Siku ukiwa tayari njoo
tujadili. Bei ni makubaliano,” alisema daktari huyo.
Alisema kwa kuwa kifaa cha kuhifadhi mayai hakipo
hivyo mchangiaji atakapochangia mayai, yatatakiwa yatumike siku hiyo
hiyo katika upandikizaji, lakini kifaa cha kuhifadhi mbegu za kiume,
kipo.
Dk huyo (tunamuhifadhi jina kwa sababu ya sheria
za hospitali hiyo), alisema mchangiaji wa mbegu au mayai atatakiwa
kupimwa kwa kina, kwanza atapimwa damu kama ana maambukizi ya VVU,
atapimwa iwapo ana maradhi ya urithi na kundi la damu kabla ya
kukubaliwa kuchangia.
Tovuti ya kliniki hiyo inaeleza wazi huduma
zinazotolewa ambapo mbali na uchangiaji wa mbegu na mayai, lakini huduma
kuu ni kuwasaidia wenye matatizo ya uzazi, kupata watoto kwa njia ya
upandikizaji.
Huduma nyingine ni kutibu matatizo ya ugumba kwa
wanawake na wanaume, kuchagua jinsia ya mtoto, upasuaji wa kukaza kizazi
kuzuia mimba kutoka (shridkar shuture) pamoja na huduma za matenite.
Madhumuni ya watu kuchangia mbegu au mayai ni
katika kuhakikisha hakuna upungufu wa mbegu, na kuwasaidia wale wote
ambao wameshindwa kutimiza ndoto za kuwa na familia.
Dk Henry Mwakyoma, Daktari Bingwa wa masuala ya
uzazi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili anasema, maendeleo hayo
yanafanikiwa zaidi nchi za nje ambako kuna teknolojia na utayari wa
watu.
“Kwa hapa kwetu kwanza teknolojia hii bado
haijapata umaarufu, lakini ni lazima kuhakikisha kuwa Watanzania wenyewe
wapo tayari kukubali uzazi wa njia hii,” alisema Dk Mwakyoma.
Alisema mchakato wa uhifadhi wa mayai unahitaji mazingira rafiki
ya maabara ambayo yanafanana na mazingira yaliyo tumboni mwa mama.
“Wakati wa upandikizaji huu, ni lazima mbegu
ziwekwe kwenye chombo chenye kiwango fulani cha joto, kemikali na viini
lishe ili kulisaidia kurutubishwa kabla halijawekwa tumboni mwa mama,”
anasema Dk Mwakyoma.
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa afya na
saikolojia wamekosoa azimio hili wakidai kuwa, litawafanya wasichana na
vijana wenye tamaa ya fedha kukimbilia kutoa mbegu zao bila kutafakari
madhara ya baadaye.
“Kwa jinsi dunia ilivyozingirwa na mahitaji ya
fedha kwa kiasi kikubwa, lazima vijana wadogo watumie nafasi hii
wakidhani itawapunguzia makali ya maisha.” Anasema kiongozi wa kampeni
ya maadili ya uzazi,” Josephine Quintavalle,
Moja ya madhara hayo ni yale yanayosababishwa na
sindano zinazotumika kuyavuta mayai ambazo husababisha mirija ya uzazi
kufanya kazi kwa kulazimishwa.
Mirija ya uzazi inapolazimishwa kufanya kazi kwa
nguvu kinyume na mfumo wake, husababisha ishindwe kufuata mfumo wa
kawaida wa kuyatoa mayai.
Vilevile, wataalamu wa saikolojia wanasema kuwa
kuchangia mayai, ukiwa kijana au binti mdogo kunaweza kusababisha
kushindwa kupata watoto siku za usoni, hasa kisaikoloia kwa kuhisi kuwa
tayari una watoto sehemu mbalimbali duniani.
Hivi karibuni kliniki ya wanawake nchini Uingereza ilianzisha benki ya kuhifadhi mbegu na mayai kwa wenye matatizo ya uzazi.
Mkurugenzi wa kliniki hiyo, Dk Kamal Ahuja
anasema, anatarajia wengi watakaochangia mayai wawe ni wanawake ambao
tayari wana watoto na wangependa kuwasaidia wanawake wenye matatizo ya
uzazi.
“Wachangiaji wengi wanaokuja hapa ni wale ambao
tayari wana watoto wana uhusiano wa muda mrefu na wameona jinsi watu
wenye matatizo ya uzazi wanavyoteseka, hivyo wameguswa kusaidia,”
anasema Dk Ahuja.
Kwa kliniki hiyo mchangiaji hulipwa dola za Marekani 750 (sawa na Sh1.2 milioni)kila anapochangia mbegu au mayai.
Mchakato wa uchangiaji mayai/mbegu unavyofanyika
Kuchangia mayai, ni mchakato ambao mwanamke anatoa yai (ova)
moja au mengi(yanaweza kuwa 10 -15) kwa malengo ya kusaidia uzalishwaji.
Mchangiaji anayetoa mayai, kama ni mwanamke huweza kwenda kliniki zaidi ya mara nane kabla ya mayai hayo kutolewa.
Mchangiaji huchomwa sindano yenye dawa ambayo husaidia kuzalishwa kwa mayai mengi.
Upimaji wa maradhi ya kurithi, VVU, na dalili
zozote za maradhi huangaliwa kwa makini kabla ya kumruhusu mchangiaji
kutoa mayai yake.
Baada ya mayai hayo kutolewa huwekwa katika chombo
maalumu maabara na kuchanganywa na mbegu za kiume(Sperm donor).
Zinaweza kuwa mbegu za mwanamume ambaye mwenza wake ana matatizo.
Baada ya siku kadhaa, mayai/mbegu ambazo
zinaonyesha dalili za utungwaji wa mimba, hupandikizwa katika tumbo la
uzazi la mwanamke.
Iwapo mayai yatabaki, huwekwa katika jokofu na baadaye huweza kutumiwa tena.
Kwa wanaume
Wanaume wanaotakiwa kuchangia mayai hupelekwa katika chumba maalumu na kutakiwa kujichua ili kupata mbegu.
Mbegu za mwanaume hutumika iwapo mwanamke ana
matatizo. Mbegu hizo hupandikizwa kwa mwanamke pindi zinapoonyesha uwezo
wa kulichavusha yai la mama.
Hata hivyo wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, au wanaotumia dawa za kulevya hawahitajiki kuchangia mbegu.
Sababu za kupata watoto kwa njia ya IVF
Zipo sababu mbalimbali za watu kuamua au kulazimika kutumia njia hii kupata mtoto.
Kwa mfano, wapo wanawake wanaopata kikomo cha hedhi (menopause) mapema zaidi wakiwa na umri wa miaka 30 au 40 tu.
Maradhi mbalimbali ambayo husababisha mirija ya
uzazi kushindwa kupitisha mayai, kizazi kushindwa kuibeba mimba (mimba
kuharibika mara kwa mara), wapo wanawake ambao wamezaliwa bila mirija
hiyo na wengine ambao hawana matatizo haya lakini wanashindwa kushika
mimba.
Sababu nyingine ni mwanaume kuwa na mbegu dhaifu zinazoshindwa kurutubisha yai la mwanamke.
Dk Mwakyoma anasema, mbegu dhaifu ni sababu kubwa
ya matatizo ya uzazi. Anataja sifa za mbegu bora kuwa ni zile zinazoweza
kuogelea hadi kufika katika mirija na kulipevusha yai la mama.
Mbegu hizo lazima ziwe na kichwa bapa, ziwe na mkia na maji mazito yanayoziwezesha kusafiri kwa urahisi.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI