Saturday, 21 September 2013

‘Mateja’ wasimulia walivyoanza ‘kula unga’

Kessy akiwa amesimama kwenye lango la kituo hicho 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Septemba21  2013  saa 13:20 PM
Kwa ufupi
Joseph anasema rafiki yake huyo alimwambia, “Ukivuta gundi unajisikia kama upo Ulaya,” kitu ambacho kilimfanya ashawishike na kuvuta ambapo ni kweli akili yake ilihama na kujisikia tofauti ingawa siku ya kwanza alijisikia vibaya.

Dar es Salaam. “Sielewi hata nifanye nini kuhakikisha mwanangu anarudi kwenye hali yake ya kawaida hata baada ya kukaa kwenye kituo cha PilliMisanah ambako alipatiwa tiba na elimu ya matumizi ya dawa za kulevya, bado sina imani kuwa ameacha kabisa ingawa mwenyewe ananithibitishia hatorudia kutokana na elimu aliyopata akiwa huko,” hiyo ni kauli ya Zabibu Kitwana ambaye ni mmoja wa wazazi waliowahi kupeleka vijana wao kwenye kituo hicho.
Akizungumzia namna alivyoingia katika matumizi ya dawa za kulevya Saya Joseph anasema mwanafunzi mwenzake katika Shule ya Msingi Bunju B, ndiye alimshawishi kutumia dawa za kulevya.
Joseph anasema rafiki yake huyo alimwambia, “Ukivuta gundi unajisikia kama upo Ulaya,” kitu ambacho kilimfanya ashawishike na kuvuta ambapo ni kweli akili yake ilihama na kujisikia tofauti ingawa siku ya kwanza alijisikia vibaya.
“Nilijisikia vibaya lakini sikuweza kuacha matokeo yake siku nyingine nikavuta bangi na kuwa mzoefu, lakini mvuke wa gundi ndio ulinivutia sana na nilikuwa tayari kufanya chochote,”anasema Joseph.
Anasema utumiaji wa dawa za kulevya ulimfanya awe ‘kibaka’ na kuwa maarufu mtaani kwao, akifahamika mwizi mwenye umri mdogo.
Naye Zackaria Kessy , mwenye umri wa miaka 55, alisema kuwa kilichomfanya aingie kwenye matumizi ya dawa za kulevya ni kutokana na msongo wa mawazo uliosababishwa na mikasa ya kimaisha.
Anasema kuwa usaliti wa mkewe uliosababisha hadi akapata mtoto nje ya ndoa, ulimfanya akawa mlevi wa pombe na siku moja katika mizozo yao mwanamke alianguka na kufa, alikamatwa na kuwekwa mahabusu ya Keko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, na baadaye alihukumiwa kifungo cha nje kwa miaka miwili.
“Nikiwa Keko tatizo ndiyo lilipoanzia kwani nilikuwa sipati usingizi hata tone yaani hata ile kuyumba, siku moja tukiwa kwenye shughuli za kawaida nikawa nawalalamikia wenzangu ambapo baadaye kijana mmoja (mahabusu mwenzangu) akaja na kunipa bangi na kuniambia nivute nitalala nikavuta na kulala kidogo siyo kwa kiwango cha kawaida,”anasema Kessy.
Anasema kuwa kabla ya kukamatwa, alikuwa na gereji maeneo ya Magomeni ambapo baada ya kuachiwa na kufungwa kifungo cha nje alirudi kwenye biashara yake, ambapo alikuwa hata akivuta bangi hapati tena usingizi na kujikuta akiangalia televisheni usiku kucha.
Kessy anasimulia kuwa siku moja akawa anawalalamikia mafundi kwenye gereji yake na vijana wengine ambao walikuwa wakija kupiga stori ofisini hapo kuwa halali, ndipo kijana mmoja akamwambia ampe Sh500, ili ampe dawa ya usingizi, akampa na kupewa kete ambayo mwanzoni hakujua kama ni unga lakini alipofuata maelekezo aliyopewa na kufanikiwa kulala usingizi mnono alioupoteza kwa zaidi ya miaka mitatu, alihisi ni unga lakini kuacha ilikuwa ngumu kwani alishachoka adha ya kukesha.
“Jioni iliyofuata akaja tena yule kijana na kuniuliza maendeleo huku akinifariji kuwa hiyo ni dawa kuu na itanirudisha kwenye hali ya kawaida, nikashawishika zaidi na kujikuta kila jioni napata kete moja kwa muda na baadaye nikawa napata mara mbili kwa usiku mmoja, kwa kuwa ilikuwa inakata mapema kabla hakuja kucha,” anasema Kessy.
Kessy anaendelea kueleza kuwa alipoanza kuvuta mara mbili kwa usiku na mwili ukaanza kuchoka asubuhi akiamka hawezi kufanya kazi, ikabidi amueleze yule kijana ambapo alimshauri awe anapata na kete nyingine asubuhi kabla ya kwenda kazini na kweli akawa anafanya hivyo na kujisikia kuwa na nguvu.

Anasema kuwa baada ya muda akawa anahitaji kupata kila baada ya muda, ambapo alilazimika kuuza gereji yake kwa Sh15 milioni na ilikuwa na kila kitu, hakuishia hapo bali baadaye aliuza hadi gari lake la Mitsubishi Pajero kwa Sh2 milioni, ambapo aliweka dhamana ya Sh laki nane na kushindwa kuzimalizia na kupewa milioni mbili ambazo ziliteketea na unga.
Anasimulia kuwa baada ya hapo akawa anafanya kazi ya udereva, ambako kote aliharibu kutokana na unga na kushindwa kabisa kufanya kazi yoyote.
Anasema kuwa amevuta dawa kuanzia mwaka 2004, hadi mwezi uliopita watoto wake walipoamua kumpeleka kwenye kituo hicho baada ya kupata habari zake.
Khalfani Ngasa, ambaye ametumia dawa kwa miaka 13, anasimulia kuwa alikuwa kwenye hali mbaya wakati anafikishwa kituoni hapo, kwani alikuwa anaumwa kifua kikuu na kuzimia mara kadhaa kabla ya kupona.
Anasimulia jinsi alivyoingia kwenye matumizi ya dawa kuwa ni baada ya kushauriwa na rafiki yake wauze dawa hizo, ambapo walikuwa wananunua maeneo ya Ilala kwa mtu mmoja anayeitwa Mfenesi.
Ngasa anasema ili ujue kama mzigo mzuri ni lazima uonje kitu ambacho hawakukifanya siku ya kwanza ambapo walinunua gramu moja kwa lugha ya kiteja ni ‘Gmoja’ kwa Sh25,000 ambapo walinunua Gtatu kwa Sh75,000 na kupata hasara kwani haukuwa mzuri na hawakuonja ikabidi wagombane na kila mmoja kuamua kufanya biashara kivyake.
“Nikaamua nifanye mwenyewe na niwe makini zaidi na kwenda peke yangu kwa Mfenesi, nikanunua gmbili kwa Sh50,000, na mimi ndiyo mtu wa kwanza kuuza unga kwenye kituo cha Tabata Segerea, ambapo ilikuwa inanilipa, kabla ya kulipa fedha nilionja , nilitapika sana na kulala kwa muda kabla ya kuamka na kuuingiza sokoni ilinilipa kwa kuwa tulikuwa tunapima kidogo sana,” anasema Ngasa.
Aidha Ngasa anasema kuwa kuanzia hapo akawa akijaribu anakaa dakika mbili anatoka jasho na kurudi kijiweni kuwauzia vijana ambao ni makonda na baadhi ya wapiga debe na kujikuta anakuwa teja, kwani lazima apate ndiyo afanye shughuli zake.
“Nilikuwa teja kwa kuonja ambapo sikuweza kuacha tena na nilibadilka nikawa kama chizi lakini baada ya kuletwa hapa na dada na shemeji yangu, naendelea vizuri na ndiyo nawapeleka wenzangu hospitali wakiwa wagonjwa na ninakwenda popote wala sina hamu nao tena, kwani ulinitesa mimi pamoja na familia yangu,” anasema Ngasa.

SOURCE: MWANANCHI