Saturday, 21 September 2013

Biashara ya binadamu TZ-2


Na Herieth Makwetta, Mwananchi

Posted  Septemba21  2013  saa 13:22 PM
Kwa ufupi
Esther Meshaki kutoka kijiji cha Ibagi, Kata ya Mang’oto wilayani Makete aliunguzwa kwa maji ya moto baada ya bosi wake wa kike kumfumania akitaka kubakwa na baba mwenye nyumba.


Dar es Salaam. Pascalina aliyefiwa na baba yake mwaka 1989 na mama yake mwaka 1996 anasema hata alivyojaribu kuhoji kwa bosi wake alijibiwa vibaya; “aliniambia ‘wewe hapa ni mfanyakazi wa ndani sasa kazi yako ni nini ikiwa mtoto wangu afanye kazi mimi nakupa mshahara wa bure humu ndani’ lile jibu ndilo lililoniondoa katika ile nyumba, miezi minne niliyoishi ilikuwa mingi sana kwangu, niliona haina haja ni heri nirudi kijijini,” anasema Pascalina mama wa watoto wawili sasa.
Esther Meshaki kutoka kijiji cha Ibagi, Kata ya Mang’oto wilayani Makete aliunguzwa kwa maji ya moto baada ya bosi wake wa kike kumfumania akitaka kubakwa na baba mwenye nyumba.
“Niliunguzwa kwa maji ya moto kifuani mwaka 1987, nilikuwa nafanya kazi jijini Dar es Salaam, huko nilichukuliwa na baba mmoja aliyekuja huku Makete kwa shughuli za kikazi, alinichukua nikiwa mdogo sana kama miaka 16 hivi wakati huo nilikuwa nimetoka kumaliza elimu ya msingi. Mkewe alinipokea vizuri tu. Nilifanya kazi kwake kwa miaka 10, nikiwa na miaka sita nyumbani kwake mkewe alifariki dunia, niliendelea kumlelea watoto wake na baada ya mwaka mmoja yule baba alioa tena.
“Huyu mke aliyemuoa kilikuwa chanzo, alikuwa hamtunzi mumewe ananipa majukumu yasiyo na msingi mwishowe yule baba akaanza kunitaka kimapenzi, nilimkatalia siku moja usiku mkewe alichelewa kurudi, matokeo yake yule baba aliingia chumbani kwangu na kuanza kunilazimisha nilikataa wakati akiendelea kutaka kunikamata kwa nguvu yule mama aliingia, waligombana na mwishowe nilijua yameisha.
Baada ya wiki moja yule mama alichukua sufuria ya maji ya moto niliyotenga kwa ajili ya ubwabwa na kunimwagia kifuani,” anasimulia.
Esther anasema alipelekwa hospitali na kutibiwa ila alivyopona aliondoka na kurudi kwao Ibagi, “niliondoka lakini yule baba alianza kuwa hanilipi fedha zangu kwa kuwa sikuwa nikikubaliana na matakwa yake, nilirudi na majeraha yasiyo na fedha ya kujitibia,” anasema Esther mwenye watoto sita na mjukuu mmoja.
Wapo waliopotezana na familia
Kuna idadi kubwa ya wazazi huwaruhusu watoto wao kwenda kutafuta kazi za ndani pasipo kujua watakapofikia, hawa mara nyingi hukosa mawasiliano na ndugu zao na iwapo atapatwa na matatizo ni ngumu ndugu kujua.
Monica, 54, anayeishi kijiji cha Ivilikinge Wilayani Makete anasema “Binti yangu aliondoka mwaka 1992 wakati huo alikuwa na miaka 14 tu tangu hapo hakurudi tena mpaka leo, ilifikia hatua tulitaka kufanya matanga ‘arobaini’ kwa kuamini kwamba amekufa baadhi ya ndugu walikataa na kudai kuwa bado wana matumaini kuwa yupo hai.”
Anasema binti yake aliondoka na kundi la wasichana wenzake ambao wanasema waliachana Ubungo, baada ya mtu wasiyemfahamu aliyefika kijijini hapo kutafuta wasichana kwa ajili ya kazi kuwatawanya kwa watu mbalimbali stendi ya Mnazi Mmoja.
“Wenzake walisharudi siku nyingi sana wana watoto wakubwa tu, sasa mimi nasema kila siku mwanangu yupo ila harudi, mpaka sasa nimeshamsahau kabisa machoni mwangu naweza pishana naye nisimtambue,” anasema Monica.
Agnetha Sanga, 34, anasema; “Mimi nimepotelewa na mdogo wangu Zawadi Sanga mwaka 2006, tangu hapo mpaka leo hatujawahi kuonana, kuna kipindi nilisikia kwamba anafanya kazi Mbeya mjini, ila sina hakika kwani sijawahi kumuona tangu usiku huo alipotoroka huku nyumbani.”

Anasema mdogo wake aligombana na watu kijijini hapo, hivyo aliamua kuondoka kwa hasira; “Hakuwa amepanga kuondoka, lakini baada ya ugomvi ule aliaga kuwa anakwenda kutafuta maisha mbele na tukiona harudi tujue amekwenda kutafuta kazi za ndani.”
Cassian Kasi mwenye miaka zaidi ya 45, yeye anamtafuta mama yake mzazi Eberina Mahenge aliyeondoka katika Kijiji cha Ivalalila mwaka 1981.
“Mama yangu aliondoka kwa madai kuwa anakwenda kutafuta, wakati huo mimi nilikuwa mdogo kwa kuwa mama yangu hakuwa na elimu yoyote alikwenda kufanya kazi ili tujikimu nyumbani, lakini mpaka leo hajawahi kurudi, nimehangaika kumtafuta sijawahi kumpata,” anasema Kasi.
Wasichana wanaouzwa Makete
Si kwamba wasichana hutolewa vijijini na kupelekwa miji mikubwa. Mambo ni tofauti wapo wanaotolewa mijini na kuuzwa kwa gharama kubwa maeneo ya vijijini.
Jirani na hoteli niliyofikia mjini Makete kuna hoteli nyingine iliyosheheni mabinti wa rika la kati yaani miaka 17 hadi 25, ni hoteli ya kawaida sana. Wasichana hawa wanafanya biashara ya kuhudumia wateja mbalimbali wanaofika hotelini hapo kwa malazi na wale wanaofika kwa ajili ya vinywaji.
Baada ya kuchunguza sana ninagundua kuwepo kwa kumbi ya starehe pembeni mwa hoteli hiyo (jina linahifadhiwa) iliyopakana kabisa. Lakini kitu cha ajabu wasichana hawa wanaongea lugha tofauti na wakazi wa eneo hilo hata lafudhi yao pia ni tofauti.
Ninapojaribu kuchunguza kwa kina ninagundua kuwa si wakazi wa eneo hilo, namuuliza kijana mmoja naye ananielezea “hawa wasichana huletwa kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Iringa na maeneo mengine ya miji mikubwa kwa ajili ya kuvutia biashara hapa lakini kama una pesa yako pia unamwona mkubwa wao unaweza mpata yoyote umtakaye,” ananielezea kijana huyo anayefanya shughuli za kuuza vocha karibu na eneo hilo.
Namfuata mmoja wa wasichana anayefanya kazi eneo hilo, ninamuuliza mkubwa wao nikiwa na lengo la kuzungumza naye, msichana huyu ananihoji shida yangu nami namweleza kuwa ninahitaji anitafutie wasichana katika vijiji vya jirani na hapo ili niweze kwenda nao jijini Dar es Salaam, msichana huyu ananiambia.
“Subiri mimi naweza kuondoka hapa usimwambie chochote nimechoshwa na kazi za hapa ambazo natumikishwa bila kujijua sikutaka kufika hapa, ngoja nikuunganishe na dada mwingine wa kule baa,” anamwita msichana mwingine wa upande wa baa ambaye naye pia ni msichana mdogo tu ninamweleza shida yangu naye ananiahidi kunitafutia.
Ninaondoka katika mji wa Makete kuelekea Ikonda. Pale ninashukia Tandale karibu kabisa na Chuo cha Ualimu Tandale. Hapo nakutana na hekaheka za wanachuo wakitoka chuoni na abiria mbalimbali wanaosubiri usafiri.
Hapo pia kuna wasichana wengi tu waliotolewa mijini na kuuzwa katika mji huo mdogo. Hiyo ni biashara kukiwa na mteja mkubwa wao anafika bei, pia ni maalumu kwa ajili ya kuvutia biashara, huku ni baa lakini huwezi kuwaona wakihudumia katika vilabu vya pombe za kienyeji.

“Siwezi kwenda baa yenye wasichana wabaya au wasichana waliotoka hapa Ikonda ni bora nikanywe Msabe au Nzuge (pombe za kienyeji), lazima niende baa yenye wasichana warembo ili nikinywa bia inakuwa na ladha na hata nikimchukua napata ladha ninayoitaka,” anasema mmoja wa wanaume ambaye alikiri kutotumia zana katika tendo la uasherati.
Wasichana wanaofanya biashara eneo hilo wanakuwa wagumu kuzungumzia hilo, lakini mmoja wao anakiri kufanya biashara za aina tofauti na ile inayowatambulisha kijijini hapo kama wahudumu wa baa.
Kauli za viongozi Mkoa wa Njombe
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Makete iliyopo mkoa wa Njombe, Leoncek Panga, anasema ingawa imepungua kasi, lakini biashara ya binadamu ni kati ya biashara kubwa zilizokuwa zikifanywa tangu miaka ya nyuma.
“Kwa hapa Makete ni ngumu kuwatambua watu hawa, kwani hutumia kigezo cha ndugu, zamani walifika na kuwanunua, lakini baada ya matatizo kadha wa kadha walianza kuchukuliwa na ndugu zao wenyewe wakipelekwa mijini na huko hutafutiwa kazi za ndani kwa madai kuwa atafute fedha ya kutuma nyumbani,” anasema.
Panga anafafanua kuwa hata chanzo cha Ukimwi kuenea wilayani Makete ni wasichana waliokuwa wakifika mijini na kisha kurudi vijijini mwao; “Ukimwi huu umeletwa na watu waliokuwa wakisafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine na wengi hasa walikuwa mabinti na wanaume walioacha familia zao na kwenda mbali kutafuta fedha kwa kazi za kuchana mbao au nyinginezo,” anasema.
Mkuu wa Wilaya ya Makete, Josephine Matiro anasema hali kwa sasa ni shwari kidogo kutokana na shule za Kata zilizojengwa miaka ya hivi karibuni.
“Hata kama bado biashara hii inaendelea, lakini shule za Kata zimesaidia kuipunguza, lakini nina imani kuwa hata wasichana wanaochukuliwa hapa Makete bado wana elimu duni ndiyo maana nimeamua kuwa na mpango wa kujenga shule ya wasichana hapa wilayani, hii itasaidia kuokoa wasichana wengi wanaofanywa mtaji na wale wanaopewa mimba wakiwa shuleni,” anasema Matiro.
Matiro anafafanua kuwa uhamaji wa watu katika wilaya yake umesababisha kupungua kwa idadi ya watu mwaka hadi mwaka pindi sensa za watu na makazi zinavyopita wilayani hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Kapteni Mstaafu Asseri Msangi, anasema tatizo hilo lilitokana na ukosefu wa muendelezo kielimu kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba sehemu mbalimbali za Mkoa huo hasa vijijini.
“Miaka ya nyuma hakukuwa na muendelezo kielimu wa kuwawezesha wahitimu darasa la saba kuendelea mbele zaidi, na huwezi kumkataza mzazi asimtoe kijana wake kwenda kutafuta kipato kwani isingekuwa rahisi kiulinzi na hujui atamtoa saa ngapi.
“Vijana wengi waliomaliza shule wazazi wao walifikiri ni vizuri wakiwatafutia kazi vijana wao, na hiyo ndiyo sababu kubwa iliyokuza biashara hiyo katika mkoa wa Njombe zamani uliotambulika mkoa wa Iringa kabla ya kujitegemea.”

Msangi anasema hivi sasa mkoa wa Njombe unajenga vyuo vya ufundi vya Veta vitakavyokuwa mkombozi wa janga la biashara za binadamu ambalo kwa sasa limechukua sura mpya.
“Ili kukomesha biashara ya binadamu hasa hawa watoto wa kike, mkoa sasa umeanza kujenga vyuo vya ufundi katika Wilaya ya Makete na Njombe kwa ajili ya kutoa elimu kwa vijana ili kupata ujuzi ambao utawawezesha kujitegemea tofauti na ilivyokuwa awali,” anasema Msangi na kuongeza; “mkoa wa Njombe unahitaji wawekezaji, kuna maeneo mengi yanayoweza kuanzishwa viwanda hivi karibuni, kuna mashamba ya nanasi na fursa nyinginezo ambazo tunafikiria itakuwa mkombozi kwa vijana hapa mkoani.”
Madalali wa biashara hii
Madalali wa wadada wa kazi wamejaa katika majiji makubwa na wapo ambao wamefungua ofisi rasmi wanazozimiliki sambamba na kutengeneza mikataba mbalimbali ya ajira kwa watu wanaowanunua wasichana hao.
Mwananchi Jumapili lilifika katika ofisi moja iliyopo Mwananyamala A na kushuhudia ofisi hiyo inayouza msichana mmoja kwa gharama ya sh Sh 50,000, sambamba na kiasi hicho kikihusika kama mkataba wa malipo kwa msichana huyo kila mwisho wa mwezi.
Dalali hutumia kiasi kidogo cha fedha kuwarubuni wazazi vijijini na kuwahadaa kwa maneno ya uongo na kisha huwachukua mabinti na kwenda nao mijini. Baada ya kuwafikisha mjini huwauza kwa watu wenye uhitaji wa wasichana.
Hata hivyo wasichana hawa huwekwa katika nyumba moja na kupewa chakula kwa kipindi fulani kwanza kabla ya kuuzwa. Wapo waliofikia hatua ya kuwafundisha hata kupika ili wanapofika kwa waajiri wao wasiwe mbumbumbu wa kila kitu. Mawakala hawa hutumia kila mbinu kuhakikisha wanakuwa na wasichana bora ili mnunuzi avutike kumwitia wateja wengine.
Wanunuzi wa bidhaa hii ni wanawake wenye watoto wadogo au wale wanaofanya kazi na hivyo kutafuta msichana kwa ajili ya kazi za ndani, hawa ndio wamegeuka wahanga wakubwa na pindi unapoanzisha habari hii hata ukiwa kwenye chombo cha usafiri lazima wachangie mada kwa namna walivyo waathirika wakubwa.
Hali ikoje jijini Dar es Saalam
Katika vitu vinavyowaumiza wanawake walioajiriwa au kujiajiri katika shughuli mbalimbali katikati ya jiji, basi ni malezi ya watoto ambayo hata hivyo wameamua kutafuta mbinu mbadala ambayo ni msichana wa kazi za ndani, msichana huyu anapewa jukumu la kumpikia mtoto kumpa mahitaji yake yote sambamba na kumwangalia kwa ukaribu zaidi.
Japokuwa wapo wasichana wanaofanya kazi hizi kwa ufanisi zaidi, lakini asilimia 70 ya wasichana wa kazi miaka ya hivi karibuni ni ‘pasua kichwa’. Haya yote yanasababishwa na mawakala ambao wamejiajiri katika hii kazi kwa kutegemea kipato cha kila siku.
Mama Jerry, mkazi wa Kimara jijini anaanza kutoa ushuhuda wake “Mimi mtoto wangu ana miaka minne, lakini nimemlea kwa taabu sana, nimeshabadilisha wasichana 30 nyumbani kwangu kuna dalali mmoja wa wadada wa kazi alinibadilishia wadada kama 10 hivi kwa kipindi cha mwaka mmoja, aliniambia kuwa anawatoa Tanga, wasichana hawa kila mmoja alikuwa na staili yake.

“Yupo aliyekaa mwezi mmoja au mmoja na kidogo, huyu wa mwisho alikaa miezi mitatu lakini ni kwa sababu nilimfichia simu baada ya kugundua anawafundisha wafanye maajabu pindi akimpata mtu mwingine anayehitaji mdada,” anasema Mama Jerry ambaye alimlipa elfu 30 kwa kila mdada aliyeletewa kama nauli.
Neema (si jina lake halisi) mwenye mtoto wa miezi saba anasimulia “nilimpata mwanangu kwa shida sana, mama yangu alinitunza mpaka miezi mitatu nilipoanza kazi, akaniahidi kukaa tena miezi mingine ila nianze kutafuta mdada, mwanangu alikuwa na afya nzuri sana, nilimpata dalali wa wasichana naye aliniletea msichana kutoka Tanga.
“Msichana huyu alikaa miezi miwili mama akaondoka, kila siku yule dalali akawa haishi sababu mara ooh nataka kuongea naye mama yake anaumwa, nikimpa simu wanaongea kilugha (Kisambaa), nikawa simwelewi.
Siku isiyo na jina aliniaga kuwa amefiwa saa moja asubuhi mimi nataka kutoka kwenda kazini, sikwenda kazini wiki nzima aliondoka, baada muda nakwenda kumsalimia shangazi yangu namkuta kule tarehe aliyoondoka kwangu, ndiyo aliyopelekwa kwa shangazi,” anasimulia Neema.
Mwanamke mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Husna anayeishi Mikocheni jijini anasema, amekuza watoto wake wanne kwa taabu.
“Watoto wangu wawili nilikuza kwa kubadili wasichana watatu tu, ila hawa wawili wa mwisho nimekoma sitamani tena kuzaa nilipata wasichana kutoka kwa dalali mmoja ambao wanasumbua hatari,” anasema.
Anasema dalali huyo maarufu kwa nambari ya simu asiyejulikana ofisi yake ilipo huwachukua wasichana Tanga, Singida na Iringa na huwauza kwa gharama ya sh 40,000 kwa kila mmoja.
“Huyu baba hukosi kumpigia simu asikupe msichana lakini wasichana wake hawakai, niliwahi muuliza msichana wangu mmoja alifikia wapi akaniambia Ukonga na huko walikuwa wengi kama 14 hivi. Wakati huo alitokea Korogwe Tanga.”
Mkasa huu umewapata wanawake wengi ambao hata hivyo wanahisi kukosa msaada kwa kushindwa kuwa na ndugu atakayeweza kujitolea kuwasaidia malezi ya watoto wao.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wanunuzi walidai kuwa licha ya gharama kubwa wanazolipwa wasichana hao bado wamekuwa si watekelezaji wazuri wa majukumu kiasi kinachomfanya mwajiri aamue kubadilisha wasichana mara kwa mara.
“Sijajua wanafanya hivyo kwa sababu zipi, lakini hali ni mbaya utakuta kila baada ya miezi miwili au mitatu unabadilisha msichana kwa hiyo inakubidi uende ukamnunue upya yaani imekuwa kama biashara na ninahisi wanafunzwa,” anasema mwanamke mmoja mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mwananchi lilifika maeneo ya Kinyerezi mwisho jijini Dar es Salaam ambako kuna nyumba ya dalali mmoja ilinayodaiwa kuwa ni chaka la biashara hiyo. Hata hivyo baada ya kufika karibu na maeneo hayo hakukuwa na dalili ya kuwapo kwa watu wengi au wasichana wadogo wanaoishi katika nyumba hiyo.

“Japokuwa unaona kimya huyu baba huwa analeta hapa wasichana ambao anawatoa vijijini na hawa huwa anawauza kutoka kwa watu mbalimbali wanaotafuta wasichana wa kazi za ndani. Hatujui ila utaona mara msichana karudi anakaa siku moja anaondoka tena baada ya miezi miwili mitatu karudi tena kisha kuondoka yaani ndio mchezo huo,” anasema mama Dulla mmoja wa majirani na eneo ilipo nyumba hiyo.
Mama Dulla anafafanua kwamba kuna wakati baba huyo hurudi na kundi la wasichana ambao huchukuliwa na watu nyumbani hapo “ Oktoba hadi Desemba ndiyo miezi yake utaona wasichana hadi 16 wanafika, msimu huo utaona magari ya wanawake na wanaume yanapaki hapo kuchukua wasichana, na wapo wanawake wengi hufika tena kwa baba huyo wakilalamika kuwa amewatorosha wasichana wao wa kazi.
“Ninavyohisi huyu baba amewageuza mtaji huwauza kwa watu tofauti tofauti. Nimewahi kumuuliza msichana mmoja akaniambia kwamba baba huyo wanayemwita ‘Baba’ huchukua elfu 50 na wao hulipwa ujira huohuo kwa waajiri wao licha ya ujira halali kuwa elfu 40,” anasimulia.
Oliva anayefanya kazi katika saluni ya kike Ukonga jijini Dar es Salaam, anasimulia namna alivyowahi kufanya kazi za ndani miaka mitano iliyopita.
“Nilifanya kazi za ndani huko Magomeni, nilitolewa Korogwe na baba mmoja aliyetutaka tumwite ‘mjomba’, nasikitika yule baba alikuwa ananipigia simu na kunidanganya kuwa nimefiwa au nina ugonjwa, nikirudi nyumbani kwake Mwananyamala alinieleza kuwa natakiwa kwenda sehemu nyingine, nikienda huko wembe ni ule ule.
“Nilihama nyumba tano kumbe mwenzangu anachukua elfu 15 kila akinihamisha, siku moja alinipeleka kwa mama mmoja aliyekuwa akiishi Mikocheni alikuwa na pesa sana akanihamishia saluni, mjomba alivyopiga simu yule mama alinihoji nami nikamweleza ukweli tangu siku hiyo mawasiliano baina yangu na mjomba yule hewa yalikatika,” anasema Oliva huku akicheka na kufafanua kwamba kwa sasa anamiliki saluni yake iliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam.
Ripoti ya UNHCR
Ripoti ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), ya mwaka jana inaonyesha kuwa Tanzania moja ya nchi ambazo zinafanya biashara ya binadamu kwa wingi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Tanzania inatuhumiwa kuwa ni kiutuo kikuu cha biashara ya binadamu ambao wanasafirishwa kwenda nje ya nchi na wengine wakitolewa katika maeneo ya vijiji kwenda mijini kwa madai ya kutafutiwa kazi.
Inaelezwa kuwa watu wanaochangiwa kuwepo kwa biashara hiyo ni ndugu ambao hukubali watoto wa kike au wanaume kupelekwa mijini kufanya kazi ukahana au vijana wa kiume kupelekwa kwenye mashamba ya migodi kufanya kazi.
Nchi ambazo baadhi ya watu wanatuhumiwa
Vijana wanaelezwa kupelekwa kuuzwa kutokea Tanzania ni pamoja na Afrika Kusini, Oman, Falme za Kiarabu, Saudi Arabi, Uingereza,Ufaransa na Marekani.

CHANZO: MWANANCHI