Kwa ufupi
Wadai Sheikh Bungo alitamka kauli za uchochezi kwenye mkutano uliofanyika wilayani Temeke hivi karibuni
Dar es Salaam. Polisi Makao Makuu Kitengo cha
Makosa ya Jinai Rasimali Watu, juzi ilimhoji Amir Mkuu wa Jumuiya ya
Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Kundecha kwa kile walichodai kuwa mtu
huyo ni rafiki mkubwa wa Sheikh Kondo Bungo anayetafutwa polisi.
Taarifa kutoka kwenye vyanzo vya polisi Makao
Makuu zilieleza kuwa Bungo anatafutwa na polisi kwa kile walichodai
alitoa maneno ya uchochezi katika Mkutano wa Waislamu uliofanyika
Viwanja vya Mwembeyanga wilayani Temeke, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Advocate
Nyombi, kutoka Kitengo cha Upelelezi Makao Makuu alipotafutwa jana
kuzungumzia suala hilo, simu yake ilikuwa haipatikani.
Chanzo chetu kilidokezwa kuwa baada ya mkutano huo
ambao pia ulihudhuriwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert
Kiondo, Polisi walipanga kumkamata Bungo kwa wakati maalumu na siyo eneo
lile ili kuepusha vurugu ambazo zingeweza kutokea endapo angetiwa
nguvuni.
“Kundecha aliitwa jana (juzi) na kuhojiwa kwa saa
kadhaa na kumtaka amlete Bungo ambaye ni mtu wake wa karibu, “ alisema
mtoa habari huyo kuongeza kuwa: “Asipofanya hivyo kwa muda aliopangiwa
basi atakamatwa yeye hadi hapo atakapo patikana Bungo.”
Katika hatua nyingine, Polisi Kanda Maalumu
inamshikilia Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa m Kitengo cha
Utafiti wa Mimea kwa tuhuma za kumjeruhi kwa risasi fundi ujenzi,
Fadhili Mkachino.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa
10 alasiri maeneo ya SalaSala Benako wilayani Kinondoni.
Alisema Mkachino akiwa na mafundi wenzake
wakijenga nyumba moja ya Khadija, ndipo profesa huyo alitokea na
kuwataka kusisitisha mpango huo mara moja kwa kile alichodai ni eneo
lake.
“Kabla ya mafundi hao hawajafanya chochote ghafla
Profesa huyo alitoa bastola na kumpiga risasi mbili tumboni Mkachino
ambaye alikuwa kiongozi wa mafundi hao na kumsababishia maumivu makali,”
alisema Kamishna Kova.
Kova alisema kitendo cha kumpiga risasi mtu ni
kosa la jinai na kwamba ni jambo lisilokubalika katika jamii. Alitoa
wito kwa wenye silaha kuwa wavumilivu wakati wote.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi