Kwa ufupi
Awataka kujituma kwa bidii katika kazi, na kwamba asiyeweza aende akakaange chipsi
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe amewataka watendaji katika Bandari ya Dar es Salaam
kuhakikisha wanajituma kwa uwezo wao na asiyeweza aende akakaange chipsi
kwani itakuwa ndiyo kazi anayoweza.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo jana katika mkutano wa
wadau wa uchukuzi wa bandari kuhusu Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa
Bandari, mkutano uliofanyika Dar es Salaam.
“Tuna mpango wa kuboresha bandari kwenye nyanja
mbalimbali kama vile kuongeza wafanyakazi wenye ujuzi na kuboresha
mazingira ya bandari kwa ujumla ili kufikia mwaka 2015 bandari yetu iwe
na uwezo wa kuingiza takriban tani 12.1 hadi tani 18 ya mizigo kwa
mwaka” alisema na kuongeza:
Alisema wizara yake imejipanga kikamilifu
kutekeleza majukumu iliyopewa na Serikali kuhakikisha wananchi wanayaona
matokeo ambayo yatawanufaisha na kuinua uchumi wa nchi na kuwataka
watendaji kufanya kazi kwa kujituma zaidi.
Dk Mwakyembe alisema Serikali inajipanga
kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam inaboresha utendaji wake na kuwa
miongoni mwa Bandari bora Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuondoa
urasimu unaokwamisha utendaji wake.
Kwa muda mrefu, Dk Mwakyembe amekuwa akifuatilia
kwa karibu utendaji wa watendaji wa Bandari ikiwemo kuwasimamisha
viongozi saba, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini
(TPA), Ephraim Mgawe.
Dk Mwakyembe alisema baada ya kuusimamisha uongozi
kuwa uamuzi wake umekuja baada ya kubainika kuwepo kwa matatizo
yanayokwamisha ufanisi wa shughuli za mamlaka hiyo ikiwa ni pamoja na
mgongano wa kimasilahi ambapo viongozi wa ndani ya mamlaka hiyo wamekuwa
na kampuni zao zinazohudumia bandari.