Kwa ufupi
Maofisa wanne wa polisi wavuliwa madaraka, saba wafukuzwa kazi, mmoja asimamishwa.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk Emmanuel Nchimbi amewavua madaraka maofisa wanne wa polisi kwa
kushindwa kuwajibika ipasavyo, huku akiwafukuza kazi askari saba wa vyeo
vya chini pamoja na kuwapa onyo wawili kutokana na kushiriki moja kwa
moja katika matukio ya wizi, kusababisha mauaji na uzembe kazini.
Nchimbi alipoulizwa sababu za kutowafukuza kazi
maofisa wa juu, badala yake amekuwa akiwavua madaraka alisema, “Hawa
niliowataja sio kama wanahusika, tunawavua madaraka kwa sababu ya
kushindwa kusimamia majukumu yao kikamilifu. Madaraka waliyopewa
yamewashinda hivyo tumewanyang’anya.”
Maofisa waliovuliwa madaraka ni Mkuu wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Arusha, Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro,
Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mvomelo, Jamal Ramadhan, Mkuu wa Kituo cha
Polisi Dumila, Juma Pamba na Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kasulu, Daniel
Bendarugaho.
Hii ni mara ya pili kwa Dk Nchimbi kuwachukulia
hatua maofisa wa polisi, kwani Machi mwaka huu waziri huyo aliwafukuza
kazi maofisa watano wa polisi na kumsimamisha kazi kwa mwezi mmoja
Kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi hilo, Renatus Chalamila kutokana
na kuhusishwa na rushwa katika kuajiri.
Pia aliwafukuza makuruta 95 waliokuwa Chuo cha Polisi (CCP), Moshi kutokana na kugundulika kutumia rushwa kupata ajira.
Maofisa watatu kati ya hao watano walifukuzwa
kutokana na kugundulika kuwa walikamata dawa za kulevya aina ya cocaine
lakini zilipopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ziligundulika ni chumvi
na sukari.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk
Nchimbi alisema amechukua hatua hiyo baada ya kupata ripoti ya kamati
aliyoiunda kuchunguza matukio yaliyotokea kati ya Desemba 26 mwaka jana
na Mei 18 mwaka huu.
Alisema matukio hayo ni lile la gari la FFU
kutumika kubeba bangi mkoani Kilimanjaro, polisi kutumia fuvu la kichwa
cha binadamu kumbambikizia mfanyabiashara kesi kwa lengo la kupata fedha
mkoani Morogoro pamoja na mauaji ya mfanyabiashara wilayani Kasulu
yaliyofanywa na askari wawili.
Sababu za kuvuliwa madaraka
Alisema Giro amevuliwa madaraka kutokana na
kushindwa kusimamia kikamilifu askari na maofisa walio chini yake na
kusababisha Mei 18 mwaka huu, kutumika kwa gari la polisi lenye namba za
usajili PT 2025 kubeba bangi kilogramu 540 zenye thamani ya Sh81
milioni.
“Yeye ndiye msimamizi wa magari yote ya FFU na
ndiye mkuu wa kikosi hicho katika mkoa huo, kwa utaratibu wa magari ya
FFU hayaendi popote bila yeye kujua, ikitokea hakujua na mpaka gari
limevuka nje ya mkoa maana yake hakutimiza wajibu wake ipasavyo, kamati
ilishauri avuliwe madaraka,” alisena na kuongeza;
“Nilipoipata taarifa ya kamati juzi niliagiza polisi wamvue madaraka na hilo lilifanyika siku hiyohiyo.”
Alisema kuwa Inspekta Ramadhani ambaye ni Mkuu wa Upelelezi
Wilaya ya Mvomelo alikuwa na taarifa juu ya mpango wa kufanyika utapeli
katika maeneo ya Dakawa na Dumila ambapo matapeli walipanga kwa
kushirikiana na polisi wasio waaminifu kumbambikizia kesi ya fuvu la
kichwa cha binadamu mfanyabiashara, Samson Mwita Kihindi wa Dumila kwa
lengo la kupata fedha.
Alisema Inspekta Mpamba alionyesha udhaifu katika
utendaji wa kazi kwa kutosimamia kikamilifu askari waliopo chini yake,
kitendo kilichosababisha askari hao kujipangia kazi nje ya utaratibu,
ikiwa ni pamoja na kuhusika katika tukio hilo la kubambikizia kesi.
Alisema ASP Bendarugaho amevuliwa madaraka
kutokana na kushindwa kusimamia upelelezi wa jalada la kesi ya mauaji ya
Gasper Mussa Sigwavumba (36) ambaye alipigwa na askari wawili (Koplo
Peter na PC Sunday) Disemba 25, mwaka jana, kuwekwa katika mahabusu ya
kituo kidogo cha polisi cha Heru Ushingo wilayani Kasulu, bila msaada wa
matibabu na kufariki dunia siku moja baadaye.
Waliofukuzwa kazi
“Koplo Edward wa FFU mkoani Arusha na PC George wa
kituo cha polisi Ngarananyuki wilaya ya Arumeru mkoani humo,
wamefukuzwa kazi Mei 20 mwaka huu baada ya kukiri kosa la kusafirisha
bangi kwa kutumia gari la polisi walilolifanya Mei 18,” alisema na
kuongeza;
“Nimewafukuza kazi Sajenti Mohamed na Koplo Nuran
wa kituo cha polisi Dumila na Sajenti Sadick Madodo wa kituo cha polisi
Dakawa, kutokana na kushirikiana na raia wawili matapeli ambao
walisambaza fuvu la kichwa cha binadamu kwa Kihindi. Askari hao
wamefukuzwa kazi na wameshtakiwa kwa uhalifu waliotenda.”
Alisema Koplo Peter na PC Sunday wamefukuzwa kazi
baada ya kumpiga Sigwavumba na kisha kumweka katika kituo cha polisi
bila msada wowote mpaka alipokutwa na mauti.
Aliyepanda cheo,waliopewa onyo
Alisema ASP Francis Duma ambaye alikuwa kiongozi
wa tukio la kukamata gari la polisi lililokuwa limebeba bangi mkoani
Kilimanjaro amepandishwa cheo na kuwa Mrakibu wa polisi kuanzia juzi.
“Askari 14 waliokuwa na Duma siku ya tukio
nimeagiza wapongezwe na Mkuu wa Jeshi la polisi nchini, IGP Said Mwema
kwani wako chini ya mamlaka yake” alifafanua.
Aliwataja waliopewa onyo kuwa ni Ispekta Salum
Juma Kingu wa kikosi cha FFU mkoani Kilimanjaro ambaye alibaki katika
gari umbali wa mita 80, kutoka nyumba ya Koplo Edward ambaye alipelekwa
kutoka wilayani Moshi, kukabidhi vifaa vya jeshi hilo na kusababisha
mtuhumiwa huyo kutoroka.
Mwingine ni Ispekta Mikidadi Galilima ambaye alishindwa kutimiza
wajibu wake ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kushidnwa kumshauri Giro
katika usimamizi wa rasilimali za kikosi.
Kamati iliyoundwa kuchunguza matukio hayo
iliongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Malalamiko cha polisi, Agustino Shayo,
Kamishna Msaidizi wa polisi, ACP Germanus Muhume na Kamishna Msaidizi
wa Jeshi la Magereza, Manland Tesha.