Monday, 26 August 2013

Mbowe ashikiliwa polisi, ahojiwa kwa saa tano

           

“Naomba mniongeze dakika 10, ninawapongeza polisi wa Iringa kwa kuwa wavumilivu na kutumia busara wakati wote wa mkutano huu licha ya kuwa nimezidisha muda kwani wangekuwa askari wa maeneo mengine wangeanza kupiga mabomu,”  Mbowe. 


Posted  Jumatatu,Agosti26  2013  saa 8:6 AM
Kwa ufupi
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi zilisema Mbowe alikamatwa saa moja asubuhi alipokuwa katika Hoteli ya A.M Country Side, nje kidogo ya Mji wa Iringa alipokuwa amefikia.

Iringa. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho, jana walishikiliwa na polisi kwa zaidi ya saa tano kwa tuhuma za kuzidisha muda katika mkutano wa hadhara uliofanyika hapa juzi.
Baada ya kuhojiwa, waliachiwa kwa dhamana ya Sh2 milioni kila mmoja.
Wanatuhumiwa kuzidisha dakika 25 za mkutano huo ambao ulikuwa maalumu kwa ajili ya kukusanya maoni ya Rasimu ya Katiba Mpya uliofanyika juzi katika Viwanja vya Mwembetogwa, Iringa na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Viongozi wengine wa chama hicho waliokamatwa ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Iringa, Frank Nyalusi.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi zilisema Mbowe alikamatwa saa moja asubuhi alipokuwa katika Hoteli ya A.M Country Side, nje kidogo ya Mji wa Iringa alipokuwa amefikia.
Kamanda Mungi alisema Mbowe na wenzake walizidisha muda walipokuwa wakihutubia mkutano huo kitendo ambacho alisema ni kinyume cha sheria. Alisema jeshi hilo linawahoji na wakibainika kuwa na makosa watafikishwa mahakamani.
“Ratiba yao ilielekeza kuwa wangefika na kuanza mkutano wa kwanza katika Wilaya ya Mufindi saa 4.00 asubuhi lakini wao waliwasili saa 9.00 alasiri,” alisema.
Alisema muda wote huo polisi walikuwa eneo la mkutano kwa ajili ya ulinzi lakini hapakuwa na taarifa yoyote ya mabadiliko ya muda hadi walipowasili saa 9.00 alasiri.
Alisema kwa mujibu wa ratiba yao walipaswa kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 8:00 wafanye mkutano wao katika Tarafa ya Ilula wilayani Kilolo lakini walifika saa 10:51 jioni.
Alisema walivumilia hayo lakini viongozi hao wakazidisha muda walipofika katika Viwanja vya Iringa Mjini ambako walianza mikutano saa 9.00 alasiri na kumaliza saa 12.25 jioni.
“Licha ya kuwakumbusha mara kwa mara hususan Mbowe aliyekuwa akihutubia mkutano huo, alikaidi agizo la Polisi na kama polisi wangeamua kupanda jukwaani na kuwashusha wangeweza kusababisha vurugu.
Juzi, akifunga mkutano wa hadhara uliolenga kukusanya maoni ya Rasimu ya Katiba, Mbowe aliwapongeza polisi wa Iringa kwa uvumilivu, akidai wametumia busara wakati wa kusimamia mkutano huo.
 “Naomba mniongeze dakika 10, ninawapongeza polisi wa Iringa kwa kuwa wavumilivu na kutumia busara wakati wote wa mkutano huu licha ya kuwa nimezidisha muda kwani wangekuwa askari wa maeneo mengine wangeanza kupiga mabomu,” alisema Mbowe.

source: Mwananchi news paper