Wednesday 2 October 2013

Uamuzi wa pingamizi za Msigwa dhidi ya Kinana kutolewa Des 12

1st October 2013
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa
Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imesema itatoa uamuzi Desemba 12, mwaka huu dhidi pingamizi zitakazowasilishwa na upande wa mlalamikiwa kwa njia ya maandishi dhidi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Kinana anamtaka Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, kufuta matamshi ya kumkashifu, kumfedhehesha  na kumhusisha na ujangili wa meno ya tembo.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Zainabu Muruke, baada ya kuziamuru pande zote mbili kuwasilisha majibishano ya kisheria kuhusu pingamizi hizo.

Jaji Muruke alisema upande wa mlalamikiwa Mchungaji Msigwa, kupitia wakili Peter Kibatala, uwasilishe pingamizi lao kwa njia ya maandishi Oktoba 14, mwaka huu na wakili  Eric Ng'maryo wa mlalamikaji Kinana ajibu pingamizi hizo Novemba 11, mwaka huu.

"Baada ya pande zote mbili kuwasilisha pingamizi na majibishano ya kisheria kwa njia ya maandishi, mahakama hii itatoa uamuzi wake Desemba 12, mwaka huu" alisema Jaji Muruke.

Katika kesi ya msingi, Kinana kupitia  wakili  Ng’maryo, amemtaka Mchugaji Msigwa, kufuta matamshi hayo aliyoyatoa Aprili 21, mwaka huu, katika mkutano wa hadhara wa kisiasa uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Wakili huyo wa Kinana, amemweleza Mchungaji Msigwa kuwa hana kinga ya Bunge kwa matamko yake dhidi ya Katibu Mkuu huyo wa CCM, maana hotuba yake bungeni ilidhihirisha kashfa aliyoitamka wakati akiwa nje ya Bunge.

“Umma unaamini matamko yako (Msigwa) na hawayachukulii kwamba ni upuuzi wa mtu asiyekuwa makini au ni ujanja ujanja na porojo za kisiasa,” ilisema sehemu ya taarifa ya wakili huyo.

Wakili huyo alisema Kinana ana nia ya kumfungulia kesi ya madai Mchungaji Msigwa ili uchafu alioupaka kwenye jina lake, usafishwe kisheria na awajibishwe kwa madhara na hasara alizozipata.

Wakili huyo amemweleza Msigwa kuwa kama atakuwa na ujasiri na uungwana wa kufanya hivyo, basi Kinana ataacha kumfungulia kesi ya madai.
CHANZO: NIPASHE