Wednesday, 2 October 2013

Uhamiaji yapangua maofisa wake

1st October 2013
Kamishina Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile.
Idara ya Uhamiaji imefanya mabadiliko katika safu ya maofisa wake wa mikoa, wilaya na wafawidhi wa vituo mbalimbali kwa kuwateua wapya.

Mabadiliko hayo yamefanywa na Kamishina Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile.

Walioteuliwa ni Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Jacob Sambai, ambaye alikuwa Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Manyara.

Naibu Kamishna Barikieli Shayo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi amechukua nafasi ya Mkoa wa Mtwara wakati Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Augustino Haule, ameteuliwa kuwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa Morogoro.

Mabadiliko hayo pia yamefanyika kwa vitengo vya makao makuu, wafawidhi wa vituo pamoja na maofisa Uhamiaji wa Wilaya.Katika mabadiliko hayo, Naibu Kamishna Hilgaty Shauri aliyekuwa Mdhibiti wa Pasi za Kusafiria Makao Makuu, amekuwa Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Kinondoni.

Nafasi yake imechukuliwa na Naibu Kamishna Abuu Mvano, ambaye kabla ya mabadiliko hayo alikuwa ni Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Naibu Kamishna Safina Muhindi ameteuliwa kuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Kinondoni.

Wengine ni Naibu Kamishna Fredrick Kiondo aliyekuwa Mfawidhi Kituo cha Holili anayekuwa Mfawidhi KIA, wakati nafasi yake ikichukuliwa na Naibu Kamishna Estomih Urio, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa ni Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Karatu.

Naibu Kamishna Apolinary Msuya ameteuliwa kuwa Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Karatu akitokea Ofisi ya Uhamiaji  Tarakea mkoani Kilimanjaro.

Aidha, Kamishna Evarist Mlay kutoka Tunduma anahamia Mkoa wa Dar es Salaam na nafasi yake inachukuliwa na Naibu Kamishna Alphonce Kwikubya aliyekuwa Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Kinondoni akisaidiwa na Naibu Kamishna Lusarago Mreka kutoka Makao Makuu.

Naibu Kamishna Sipora Moshi aliyekuwa Mfawidhi Kituo cha Bandari ya Dar es Salaam ameteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Ubalozi Makao Makuu ya Uhamiaji na nafasi yake inachukuliwa na Naibu Kamishna Harride Mwaipyana aliyekuwa Ofisi ya Uhamiaji Kabanga.

Mabadiliko hayo, ambayo yanaanza mara moja ni sehemu ya kuimarisha utendaji kazi na uwajibikaji ndani ya Idara ya Uhamiaji katika kuwahudumia wananchi, kuwezesha uingiaji na utokaji wa watu pamoja na udhibiti wa wageni nchini.

Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abbas Irovya, alisema Idara imeandaa mkakati wa maboresho ya kitaasisi, rasilimali watu pamoja na vitendea kazi ili kuhakikisha kwamba, watumishi wanaondokana na utendaji wa mazoea.
CHANZO: NIPASHE