Wednesday, 21 August 2013

Tusidanganyike, wahamiaji haramu bado lukuki

Rais Jakaya Kikwete ambaye hivi karibuni alivitaka vyombo husika kuhakikisha kuwa vinawasaka na kuwarudisha kwao wahamiaji haramu 


Posted  Agosti17  2013  saa 23:30 PM
Kwa ufupi
Kauli na matamko ya viongozi mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa katika nyakati tofauti yanaonyesha pasipo kuacha shaka kwamba Serikali bado haijatambua ukubwa wa tatizo la wahamiaji haramu katika mkoa huo.

Serikali inaonekana kupatwa na kiwewe na kuridhishwa na mafanikio kiduchu katika suala la kuwarudisha makwao wahamiaji haramu katika Mkoa wa Kagera.
Kauli na matamko ya viongozi mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa katika nyakati tofauti yanaonyesha pasipo kuacha shaka kwamba Serikali bado haijatambua ukubwa wa tatizo la wahamiaji haramu katika mkoa huo.
Inawezekana kwamba viongozi serikalini hawakuamini kwamba agizo la Rais Jakaya Kikwete kuhusu wahamiaji haramu mkoani Kagera kurudi makwao lingepata mafanikio angalao kidogo. Yafaa tukumbuke hapa kwamba Rais alipofanya ziara katika Mkoa wa Kagera mwishoni mwa mwezi uliopita aliwapa wiki mbili wahamiaji haramu wawe wamerudi makwao kwa hiari yao, vinginevyo wangekamatwa katika operesheni maalumu ya kijeshi baada ya muda huo kuisha.
Takwimu zilizotolewa baada ya muda huo kuisha ziliwapa viongozi wa Serikali matumaini makubwa kupita kiasi, hivyo kutoa matamshi na kauli zilizoibua hisia miongoni mwa wananchi kwamba sasa tatizo la wahamiaji haramu katika mikoa hiyo limekwisha. Bahati mbaya ni kwamba wananchi hawakuweza kutambua kwamba tatizo la wahamiaji haramu bado ni kubwa mno kuliko Serikali inavyofikiria, mbali na takwimu zilizotolewa na viongozi mbalimbali serikalini katika wakati tofauti kutofautiana, hivyo kuibua maswali mengi kuhusu usahihi na uhalisia wa takwimu hizo.
Juzi katika nyakati tofauti viongozi wa Serikali walitoa takwimu zilizoonyesha mkanganyiko huo. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe alisema kati ya Julai 29 mpaka juzi wahamiaji haramu 8,262 walikuwa wameondoka mkoani humo kuelekea Rwanda, Burundi, Uganda na DRC. Alisema kati ya hao, wahamiaji 5,200 walikwenda Rwanda, 2,800 walikwenda Burundi, 220 Uganda na 42 walielekea DRC, huku wakisalimisha silaha 42, zikiwamo za kivita aina ya AK47.
Lakini siku hiyohiyo, Wizara inayohusika na masuala ya kigeni, ilitoa taarifa kwamba idadi ya wahamiaji haramu walioondoka kwenda makwao ni 8,509. Alisema waliokwenda Rwanda ni 5,521 na kwamba Burundi walikwenda 2,744 wakati Uganda walirejea wahamiaji 244. Kuhusu silaha, wizara hiyo ilisema bunduki 60 zilizotengenezwa kienyeji ndizo zilizosalimishwa.
Hata hivyo, takwimu ambazo hazikuwa na utata ni za mifugo. Taarifa ya Wizara na ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera zote zinataja 1,996 kama idadi ya mifugo iliyosafirishwa na wahamiaji hao wakati wakirudi makwao.
Tumechapisha takwimu hizo ili kuonyesha kutokuwapo kwa umakini katika mamlaka zinazohusika na jambo nyeti kama hilo na pia kuonyesha kwamba tatizo la wahamiaji haramu bado ni kubwa mkoani Kagera. Inakadiriwa kwamba wapo wahamiaji haramu mkoani humo zaidi ya 50,000.
Sensa ya watu hao ya mwaka 2006 ilionyesha walikuwa 32,000 na iliongezeka kwa kasi ya ajabu baadaye kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi katika mamlaka za kiserikali, zikiwamo Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Takukuru na Serikali za Mitaa.
Tunachotaka kusema hapa ni kwamba Serikali isibweteke kwa kuondoka wahamiaji haramu 8,000 tu wala kusalimishwa kwa bunduki 42. Wamebakia wahamiaji haramu na silaha lukuki. Lazima operesheni aliyoitangaza Rais Kikwete ianze sasa kuwanasa wahamiaji haramu waliobaki na silaha wanazozitumia kuua na kuteka wananchi.
Tatizo pekee tunaloliona ni kukwamishwa kwa operesheni hiyo iwapo itahusisha pia watumishi wa mamlaka hizo hapo juu ambao ndio waliosababisha hali hiyo.