Posted Jumanne,Agosti20 2013 saa 19:42 PM
Kwa ufupi
Wizara ya Uchukuzi ni moja ya wizara chache
nyeti hapa nchini ambazo zinashikilia uchumi wa nchi yetu na maisha ya
kila siku ya wananchi.
Kama kuna jambo ambalo halina ubishi miongoni
mwa wananchi hivi sasa ni suala la Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe kustahili kuitwa ‘Askari wa Mwavuli’ kutokana na uwajibikaji
wake katika kutekeleza majukumu aliyopewa na mamlaka iliyomteua kushika
wadhifa wa uwaziri.
Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu sana utendaji
wake wa kazi tangu alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya
Ujenzi baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita hadi alipopewa dhima ya kuongoza
Wizara ya Uchukuzi Januari 2011. Katika muda huo, hatukupata kutilia
shaka utendaji na utekelezaji wake wa majukumu mazito aliyokabidhiwa na
mkuu wa nchi, wala kuhoji dhamira na ujasiri wake katika kufikia malengo
yaliyowekwa bila woga wala upendeleo.
Hata hivyo, lazima tukiri kwamba uwajibikaji na
ujasiri wake katika utendaji wa kazi zake umejidhihirisha hasa baada ya
kupewa fursa ya kuongoza Wizara ya Uchukuzi. Kusema kweli hakuna naibu
waziri katika wizara yoyote ulimwenguni anayeweza kutegemewa kuonyesha
makucha yake halisi ya kiutendaji, kwani kimfumo anakuwa chini ya waziri
na anategemewa kutekeleza majukumu anayopewa na waziri ambaye ndiye
kiongozi wake. Vinginevyo, atalalamikiwa kwa kutaka kumfunika waziri na
ataibua hisia kwamba anataka kukalia kiti chake.
Tumesema yote hayo katika kujaribu kuonyesha kwa
nini Waziri Mwakyembe amejipambanua zaidi kama Askari wa Mwavuli baada
ya kuwa kiongozi mkuu wa Wizara ya Uchukuzi wakati hakuweza kuwa hivyo
wakati alipokuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi. Wizara ya Uchukuzi ni
moja ya wizara chache nyeti hapa nchini ambazo zinashikilia uchumi wa
nchi yetu na maisha ya kila siku ya wananchi. Hivi maisha pasipo vyombo
vya usafiri wala miundombinu ya kuviwezesha vyombo hivyo kufanya kazi
yangekuwa maisha ya namna gani?
Ni wizara nyeti kwa tafsiri yoyote ile, kwani
ndiyo inayosimamia usafiri wa reli, anga, maji na barabara, pia ndiyo
inayosimamia taasisi zinazoendesha bandari, viwanja vya ndege na
miundombinu ya reli. Ndiyo maana mawaziri waliomtangulia walishindwa
kuhimili vishindo, changamoto na mikikimikiki itokanayo na majaribu
yatokanayo na shughuli za wizara hiyo. Wengi walikosa ubunifu, ujasiri
na uthubutu wa kujaribu, hivyo wakaendekeza urasimu wa kusoma taarifa za
mafaili katika ofisi zenye viyoyozi.
Hakuna asiyejua nini kilitokea baada ya Waziri
Mwakyembe kupewa wizara hiyo. Kwanza alitangaza vita dhidi ya ufisadi,
rushwa na ubadhirifu katika wizara hiyo na taasisi zote zilizo chini
yake. Sote ni mashahidi wa nini kilitokea katika bandari zetu, Shirika
la Ndege, Shirika la Reli, Sumatra na viwanja vya ndege.
Kama tulivyoshuhudia katika matukio mbalimbali
kama wizi wa kontena na mafuta bandarini au upitishaji wa dawa za
kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, ufisadi na wizi katika
sehemu hizo pia umewahusisha baadhi ya watumishi katika vyombo vya
ulinzi na usalama, likiwamo Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa.
Waziri Mwakyembe amepambana na wahalifu hao bila
woga na ndiyo maana wananchi wengi wanataka apewe ulinzi wa uhakika. Kwa
mfano, vita yake dhidi ya dawa za kulevya bila shaka imemtengenezea
maadui wengi, tena wenye fedha. Tunamshauri Rais Jakaya Kikwete siyo tu
ampe ushirikiano, bali pia ulinzi wa uhakika dhidi ya mafisadi, magwiji
wa unga na wahalifu wengine wengi.
source: Mwananchi
source: Mwananchi