Tuesday, 20 August 2013

Makali ya Dk Mwakyembe yaanza kukata watuhumiwa wa ‘unga’


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe 
Na Bakari Kiango na Aziza Masoud  (email the author)

Posted  Jumatatu,Agosti19  2013  saa 20:20 PM
Kwa ufupi
Uongozi wa Uwanja wa JNIA tayari umewakabidhi barua za kuwasimamisha kazi.

Dar es Salaam. Wafanyakazi wanne wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wanaotuhumiwa kula njama za kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine, wamesimamishwa kazi.
Mkurugenzi wa JNIA, Moses Malaki, alisema jana, kuwa utaratibu wa kuwapatia barua umekamilika, kinachofuata ni utaratibu wa kuunda tume unaotarajia kufanyika wakati wowote kuanzia jana.
“Tumewapa barua zao rasmi kuwasimamisha kazi leo (jana) saa 8:00 mchana, kama watakuwa na cha kujitetea, wasubiri tume itakayoundwa wakati wowote kuanzia sasa,” alisema Malaki.
Alisema tume hiyo itafanya kazi kwa siku 14, ikiwamo kuwahoji wahusika baada ya hapo itatoa maelekezo serikalini.
Kuhusu watuhumiwa hao kupelekwa polisi, Malaki alisema suala hilo wanaliachia chombo hicho kutekeleza wajibu wao kisheria.
Hatua hiyo inatokana na agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alilolitoa wiki iliyopita kuagiza wote waliohusika na njama hizo kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine, Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, limeomba polisi kumwongezea ulinzi Dk Mwakyembe kutokana na mapambano yake dhidi ya dawa hizo.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Mwakyembe kutangaza vita na waingizaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya, wanaotumia JNIA na kusababisha kuonekana uchochoro wa dawa hizo.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Alhad Mussa Salum, alisema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo nchini, jamii inapaswa kuwa na mikakati shirikishi ya kuondoa mtandao huo unaotisha.
“Kwa sababu mtandao wa dawa za kulevya unatisha, tunaomba polisi imwongezee ulinzi Mwakyembe kwa sababu anapambana na watu hatari na hawatamwacha,” alisema Salum.
Baraza hilo linajumuisha viongozi mbalimbali wa dini zote wakiwamo masheikh, maaskofu na wachungaji.

source: Mwananchi news paper