Monday, 5 August 2013

Mfalme wa Morocco abatili msamaha


 5 Agosti, 2013 - Saa 09:30 GMT

                             
Wengi walipinga hatua ya mfalme kumsahamehe Daniel ambaye inasemekana ametoroka nchini humo
Mfalme wa Morocco amebatili uamuzi wake wa kumsamehe mwanamume raia wa Uhispania aliyeshtakiwa kwa kuwaharibu watoto 11 walio kati ya umri wa miaka 4 na 15. Hii imethibitishwa na maafisa kutoka kasri la mfalme Mohammed wa sita.
Inaarifiwa mfalme hakuwa na uelewa wa ukubwa wa kosa alilofanya raia huyo mhispania kulingana na baraza lake la mawaziri kabla ya kuwasamehe wafungwa.
Mshukiwa huyo alikuwa miongoni mwa watu 48 raia wa Uhispania walioachiliwa huru kufuatia msamaha wa Mfalme , hali iliyosababisha maandamaano makubwa mjini Rabat siku ya Ijumaa.
Waandamanaji walitishia kufanya maandamano mapya mjini Rabat na Casablanca wiki ijayo.
Daniel Galvan Vina, anayeaminika kuwa na umri wa miaka sitini, alihukumiwa jela miaka 30 tangu Septemba mwaka 2011.
Hata hivyo, wiki jana , aliachiliwa baada ya mfalme kuamuru kuwa wafungwa waachiliwe kutoka jela la Kenitra, Kaskazini mwa mji mkuu Rabat. Inasemekana kuwa mtu huyo tayari ameondoka nchini.
Hata hivyo wizara ya sheria imesema kuwa itajadili hatua itakazochukua kutokana na raia huyo wa Uhispania.
Mamia ya watu walijeruhiwa katika makabiliano yaliyozua ghasia kati ya waandamanaji na polisi nje ya bunge la nchi hiyo siku ya Ijumaa.
Maandamano pia yaliripotiwa kufanyika katika miji ya Kenitra, Tangier na Tetouan, pamoja na nje ya ubalozi wa Morocco mjini Paris.
"mfalme hakuwahi kufahamishwa chochote kuhusu kesi hiyo, na mashtaka aliyokabiliwa nayo mtu huyo kiasi cha kufungwa jela, '' ilinukuu taarifa kutoka kwa Ikulu ya Rais mnamo Jumapiali.
Ni jambo la kawaida, kwa mfalme kuwasamehe wafungwa kwa kipindi maalum kama wakati wa sherehe za siku ya kutawazwa ufalme iliyoadhimishwa Jumanne iliyopita.
Waziri wa sheria wa Morocco, alisema Ijumaa kuwa msamaha ulitolewa kwa sababu za kitaifa na uhusiano mzuri na Uhispania.

chanzo: BBC Swahili