Na Elias Msuya, Mwananchi
Posted Jumatatu,Septemba16 2013 saa 12:30 PM
Posted Jumatatu,Septemba16 2013 saa 12:30 PM
Kwa ufupi
- Tindikali inaonekana kuwa na athari kubwa nchini na huenda isipoangaliwa italeta athari zaidi hasa katika chaguzi zijazo.
- Ubaya wa tindikali ni kwamba ni rahisi kubebeka, mtu anaweza kufikiri umebeba chupa ya maji, kumbe ni tindikali, inapokuwa kwenye chupa haina athari.
Matukio ya kumwagiwa tindikali yameendelea
kukithiri huku Serikali ikiendelea kutoa ahadi za kudhibiti bila
mafanikio. Hivi karibuni baada ya raia wawili wa Uingereza kumwagiwa
tindikali Zanzibar, Serikali iliweka mikakati mikali ya kudhibiti
matumizi ya kemikali hiyo, lakini bado matukio hayo yameendelea kuwepo.
Tukio la kumwagiwa tindikali kwa Padri wa Kanisa
Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang’amba ni
mwendelezo wa uhalifu huo ambao Serikali imeshindwa kabisa kuudhibiti.
Akieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea, Padri
Mwang’amba anasema alikuwa nje ya duka linalotoa huduma za mawasiliano
ya mtandao (Sun Shine Internet Caffee) liliopo eneo la Mlandege Wilaya
ya Mjini Unguja, ndipo alipotokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.
Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar
Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio
ya viongozi wa dini na Serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa
kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.
Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa maeneo ya
usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo
alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka
visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Kwa upande wake, Padri wa Parokia ya Mtakatifu
Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na kiongozi huyo mpaka
MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang’amba alitolewa vitisho na mtu
ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha wazee cha
Welezo.
Alisema kabla ya kufika kituoni hapo, kuna eneo
ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi barabarani ambapo kuna
mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho.
Tukio hilo linafuatia tukio la Agosti 7, mwaka huu
ambapo raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18)
walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji Mkongwe, Zanzibar na vijana
wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya Vespa.
Waingereza hao walisafirishwa siku tatu baadaye kurudi kwao Uingereza kwa ajili ya matibabu.
Utetezi wa Serikali
Siku tano baada ya tukio la Waingereza hao
kumwagiwa tindikali, Serikali kupitia vyombo vyake vya uchunguzi
iliwataka wananchi kuisaidia kuwafichua na kutoa ushahidi wa uhalifu huo
kwani ni vigumu kuwabaini wahusika.
Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja jana na Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa
Samwel Manyele na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) Eliezer
Feleshi, katika mkutano wao na waandishi wa habari, uliolenga kueleza
mikakati ya kupambana na matumizi yasiyo sahihi ya tindikali nchini.
“Mkemia Mkuu, Polisi hawawezi kubaini matukio haya bila
ushirikiano wa wananchi kwani Tanzania ni nchi kubwa na ina watu zaidi
ya milioni 45. Watu wanaingiza tindikali lakini wapo ambao wanatumia
tindikali hiyo kwa matumizi haramu,” alisema IGP Mwema.
Amesema tindikali inaweza kutolewa kwa ajili ya
shughuli za viwandani, maabara na usafirishaji na kwamba watu wanapotaka
kuitumia kwa ajili ya kufanya uovu wanaweza kugundulika kupitia kwa
taarifa zitakazotolewa na wananchi, kwa sababu wanakuwa wamezungukwa na
jamii ya watu mbalimbali.
Matukio mengine
Tukio lingine lililoshtua ni lile la bilionea Said
Mohamed Saad ambaye ni mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre,
kumwagiwa tindikali mwanzoni mwa mwezi Agosti.
Said anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini na inaelezwa kuathirika vibaya usoni, mikononi na kifuani.
Alimwagiwa tindikali Julai 19, mwaka huu akiwa kwenye moja ya maduka yake katika Jengo la Msasani Mall, Dar es Salaam.
Taarifa za siku ya tukio zilibainisha kuwa Said
alikuwa akizungumza na mfanyakazi wake muda wa saa moja jioni ndipo
akatokea kijana mrefu, mwembamba ambaye alimmwagia kimiminika
kinachosadikiwa kuwa ni tindikali.
Ilibainishwa kwamba mfanyakazi huyo wa Said,
Hassan Ahmad naye alijeruhiwa kidogo katika purukushani hiyo lakini
alipopelekwa Hospitali ya Ami Wellness Centre, alitibiwa na kuruhusiwa
huku bosi wake akipelekwa Afrika Kusini usiku huohuo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius
Wambura anasema matukio ya kutumia pikipiki yanaonyesha kupangwa hivyo
inakuwa vigumu kuwabaini wahalifu mapema.
Tukio hilo linafanana na lile lililotokea Septemba
8, mwaka huu ambapo mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Christian Msema
wa Mburahati jijini Dar es Salaam, alimwagiwa kemikali hiyo na watu
waliokuwa kwenye pikipiki ya matairi matatu.
Msema maarufu kama Mnyalu amelihusisha tukio hilo
lilitokea jioni ya Jumamosi Septemba 8 na mgogoro wa eneo la wazi ambapo
yeye alikuwa akipinga mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa)
kulitumia kuegesha magari yake.
Akizungumza kwa shida katika hospitali ya Taifa ya
Muhimbili alikolazwa anakiri kuwa mstari wa mbele kupinga eneo hilo
kutumiwa kinyume na sheria.
“Awali vijana wasio na ajira waliomba eneo hilo ili walitumie
kwa mradi wa kuegesha magari, wakaandika barua, lakini Serikali ya mtaa
ikakataa ikisema hilo ni eneo la kazi. Hiyo ilikuwa mwezi Oktoba mwaka
jana, ilipofika Novemva, tukaona malori yanaegeshwa pale. Tulipofuatilia
tukaambiwa ni mwenyekiti wa mtaa ameruhusu,” anasema na kuongeza:
“Tukajiorodhesha wana mtaa tukafika kama watu 60
na mimi nikawa mwenyekiti wao, tukapeleka barua yetu kwa Mkurugenzi wa
Manispaa ya Kinondoni ambaye aliipeleka kwa ofisa wa mipango miji.”
Ameongeza kuwa ofisi ya mipango miji ya Kinondoni
ilisema hilo ni eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya
sekondari hivyo ikaagizwa kuwa magari hayo yaondolewe.
“Kampuni iliyopewa tenda ya kuondoa yale magari
ilifanya kazi bila kutoa notisi, ndipo yule mwenye magari akaenda
kulalamika kwa mkuu wa mkoa. Malalamiko yakafika kwa Mkurugenzi ambaye
aliagiza kampuni hiyo irejeshe hayo magari ili utaratibu ufuatwe,”
alisema. Aliendelea kusema kuwa yule mfanyabiashara aliendelea kukaidi
kwa kuongeza magari mengine kwenye uwanja huo hadi yalipokuja kuondolewa
kwa nguvu.
Msema alisema wakati mvutano huo ukiendelea,
aliwahi kukutana na mlinzi wa mfanyabiashara huyo ambaye
alimtahadharisha kuwa harakati zake hizo zitamponza kwani anafuatiliwa.
“Mimi sikukata tamaa kwani lile ni eneo la umma
kwa nini mtu ang’ang’anie? Lakini watu wengi walinitahadharisha kuwa
yule jamaa ananifuatilia, ndiyo maana siku ile ya tukio kuna bajaji
kumbe ilikuwa inanifuatilia kwa muda mrefu,” anasema.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mburahati, Tungaraza
amekanusha kuwepo kwa mgogoro huo huku akimtaka mwandishi afike ofisini
kwake kwanza. Matukio hayo yameanza muda mrefu na wakati mwingine
yamehusishwa na chuki za kisiasa.
Baadhi ya wananchi wanashauri Serikali kuwa imara na tindikali hasa katika chaguzi zijazo, kwani tindikali ni rahisi kuibeba.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI