Na Daniel Mjema, Mwananchi
Posted Jumapili,Septemba15 2013 saa 2:0 AM
Posted Jumapili,Septemba15 2013 saa 2:0 AM
Kwa ufupi
Kisumo ambaye ni mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la
Wadhamini wa CCM, alisema ameanza kupata wasiwasi kuhusu mhimili wa
Bunge hususan kiti cha Spika hasa katika suala la Mbowe.
Moshi. Mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo
amezungumzia vurugu zilizotokea bungeni akisema Naibu Spika, Job Ndugai
na Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe, wote wana makosa.
Kisumo ambaye ni mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la
Wadhamini wa CCM, alisema ameanza kupata wasiwasi kuhusu mhimili wa
Bunge hususan kiti cha Spika hasa katika suala la Mbowe.
Mwanasiasa huyo aliyasema hayo wakati akizungumza
na gazeti hili jana ku tokana na vurugu zilizotokea Bungeni wiki
iliyopita baada ya Naibu Spika kuamuru kutolewa nje kwa nguvu kwa Mbowe.
Kisumo alisema alichopaswa kufanya Ndugai baada ya
Mbowe kukaidi amri ya kutoka nje ni kumwita mpambe wa Bunge (Sergeant
at Arm) na kama ataendelea kukaidi alitakiwa kuahirisha Bunge.
“Mbowe alitolewa na Polisi nadhani Naibu Spika
alikosea…Mpambe ndiye alipaswa amtoe na akishindwa alipaswa aahirishe
Bunge halafu amshtaki kwenye kamati husika,” alisema Kisumo.
Kisumo alisema kitendo cha Ndugai kuamuru Polisi
kuingia ndani ya Bunge ambao wamefunzwa kutumia nguvu, kilikuwa ni
makosa makubwa na kusisitiza katika hilo Ndugai alikosea.
Hata hivyo alisema hata Mbowe, naye alikuwa na makosa pale alipokataa kutii maagizo ya kiti (Naibu Spika).
“Mbowe na chama chake kisichukulie ubabe wao
katika mikutano ya hadhara ambayo haina lugha ya kibunge na kuzipeleka
bungeni haya ni makosa makubwa,” alisema.
Kisumo alisema binafsi anapenda vyama vingi lakini
hapendi aibu ya kupigana mahali patakatifu kama bungeni na kuutaka
upinzani pamoja na uchache wao Bungeni, kushindana kwa hoja zenye nguvu.
“Vyama vya upinzani haviwezi kushinda hoja yoyote
bungeni itakayoamuliwa kwa njia ya kura kwa sababu ya uchache wao… Wao
waendelee kutoa hoja na mwisho wa siku umma utawaelewa,”alisema.
Kisumo alisisitiza kuwa Chadema wasichukulie mambo
yao ya majukwaani yaliyojaa kile alichodai tamaa ya madaraka kuongoza
nchi wakayapeleka bungeni ambako kuna kanuni na taratibuSOURCE: MWANANCHI