Wednesday, 21 August 2013

Mambo Mkakati

Tido Mhando 



Posted  Jumapili,Agosti18  2013  saa 13:26 PM
Kwa ufupi
Tido Mhando amefanya kazi ya utangazaji wa redio kwa muda mrefu sana.  Aliifanya kazi hii hapa Tanzania, Kenya na Uingereza, ikampatia umaarufu mwingi.


Tido Mhando amefanya kazi ya utangazaji wa redio kwa muda mrefu sana.  Aliifanya kazi hii hapa Tanzania, Kenya na Uingereza, ikampatia umaarufu mwingi. Je, maisha kama mtangazaji wa aina yake yalikuwaje katika enzi hizo? Tido analijibu swali hili katika simulizi zake hizi za kila Jumapili. Wiki iliyopita alitufahamisha mwanzo wa kuwika kwa mwanariadha ambaye, labda, ni bora kuliko wote Tanzania hadi sasa, Filbert Bayi, pale alipomshinda mkongwe wa riadha wa Kenya, Kipchoge Keino mwaka 1973. SASA ENDELEA...
Naweza kusema bila ya tashwishi yoyote kwamba, mwaka huo wa 1973 ndiyo uliokuwa  mwaka wangu wa mabadiliko makubwa sana kazini na hata katika hali ya maisha yangu binafsi.
 Kama nilivyoeleza hapo nyuma, huo ulikuwa ni mwaka ambao niliteuliwa, kwa mara ya kwanza, kwenda kufanya kazi nje ya Tanzania, pale nilipotumwa nchini Uganda kutangaza mashindano ya mpira ya nchi za Afrika Mashariki.
 Baada ya Filbert Bayi kumshinda Kipchoge Keino kule Lagos Nigeria, mwaka huo huo wa 1973, taifa la Tanzania likawa limeingiwa na msisimko mkubwa sana kuhusiana na michezo hii ya riadha na hasa ile ya kimataifa.
 Watanzania, hasa vijana, wakaanza kuchakarika kwelikweli na kujiingiza kwa wingi kwenye fani hii, huku Serikali nayo ikionyesha nia ya dhati ya kutaka kuiendeleza katika ngazi zote.
 Sisi pia pale Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), kila ilipowezekana tulifuatilia kwa karibu maendeleo hayo kwa kutangaza sana habari za mashindano mbalimbali ya riadha, iwe ya shule za msingi, sekondari na vyuo, hasa yale ya kitaifa na kimataifa.
 Kwa jumla ilipofika wakati huu, tayari nilikuwa najitambua kama miongoni mwa watangazaji walioanza kushamiri; nyota yangu ilikuwa imeanza kupata nuru yake.
 Nakumbuka siku moja katika mwaka huohuo wa 1973, tukiwa tunakaribia mwishoni mwa mwaka, aliyekuwa Mkurugenzi siku hizo, Paul Sozigwa, aliita mkutano adimu wa watangazaji wote.
 Nasema ulikuwa mkutano adimu kwani si mara nyingi mkuu huyo alikuwa anakutana nasi hivi, kwa hiyo tukajua bila ya shaka kuna mambo makubwa ambayo alitaka kutufahamisha au kushauriana nasi.
 Ikumbukwe ya kwamba hili lilikuja muda mfupi tu baada ya mimi kurejea kutoka Uganda, Uganda kwa Idi Amin Dada, Idi Amin ambaye tayari alikuwa ameshaanza kuzusha chokochoko na Tanzania.
 Halafu mkuu wetu huyo, Sozigwa, hakuwa tu mkuu wa kawaida. Alikuwa mtu mwenye kauli ya kutambulika na utawala wa ngazi za juu. Alikuwa karibu sana na Rais Mwalimu Julius Nyerere.

 Sozigwa alikuwa mtu wa kuzingatia maadili sana, kwa hiyo aliaminika pia kwa kiasi kikubwa katika chama tawala siku hizo, chama pekee cha siasa huku Tanzania Bara, chama cha Tanu. Ikumbukwe kule visiwani kulikuwa na chama cha Afro Shirazi.  Kwa jumla chama cha Tanu kilimtumia sana mkurugenzi huyu kwenye mambo yake ya propaganda zake.  Kwa kweli alikuwa na uwezo wa hali wa juu kwenye eneo hilo.
 Kwani ni yeye Sozigwa  ndiye aliyekuwa mtu wa mwanzo kabisa kuandika yale yaliyokuja kutokea kuwa labda mazungumzo bora ya habari kuwahi kutangazwa na redio yoyote barani Afrika.
 “Mazungumzo Baada ya Habari” yalikuwa na kila kitu ambacho msikilizaji alikihitaji na yeye mwenyewe kulengwa. Yaliandikwa kwa ufasaha mkubwa. Yaliandikwa kwa lugha yenye mvuto sikioni na yalisomwa kwa umakini wa hali ya juu na wasomaji bora wenye sauti adimu zenye mvuto.  Yalikuwa ni mazungumzo yaliyobeba ujumbe mzito wa kitaifa kwa watu wote, ujumbe uliotakiwa kueleweka na kila mtu bila ya taabu yoyote. Dhamana hii kwa mara ya kwanza aliibeba Sozigwa na kuitekeleza kwa ufanisi usio na kifani.
 Kila siku iendayo kwa Mungu, mara tu baada ya taarifa ya habari ya saa 2:00 usiku, Watanzania kwa mamilioni walikuwa wakitega sikio kusikiliza kipindi hiki cha dakika chache tu cha “Mazungumzo Baada ya Habari.” 
Zilikuwa dakika chache za kusisimua. Dakika chache zilizojaa kipaji cha  ubunifu wa kiwango kikubwa cha kumakinika. Dakika chache ambazo msikilizaji alikuwa anaelimika, anaburudika na pia anafahamishwa.  Mara zote, mazungumzo haya yalikuwa yakianza kwa hadithi ya aina fulani. Mara nyingi, mwandishi Sozigwa akizibainisha humo kuwa ni ya hadithi ya kweli.  Kama ni kweli, bali mwandishi huyu alikuwa akifahamu mengi, tena mengi mno!
 Nazikumbuka sana hadi leo baadhi ya hadithi nyingi hizi za kusisimua. Ikiwa ni pamoja na ile ya “Uchu wa Mzee Mikidadi”, iliyohusu mwanafunzi mmoja kutoka Shule ya Sekondari ya Mpwapwa ambaye wakati mmoja wa likizo alimkaribisha rafiki yake waende naye nyumbani kwao.
 Kama ilivyo kawaida, walipofika nyumbani kwa Mzee Mikidadi, walikaribishwa vizuri sana. Baba akaamuru lichinjwe jogoo kubwa kuliko yote miongoni mwa kuku wake ili mwanaye na mgeni wake waweze kufurahi.
 Ilipofika wakati wa chakula, Mzee Mikidadi na vijana wake wawili wakaketi pamoja kufaidi mlo wao huo huku mzee mwenyewe akichukua madaraka ya kugawa kile kitoweo  akisema “Kuleni wanangu, leo siku kuu yenu!”
  Wakati akisema hayo  mwenyewe alikuwa akijichukulia yale mapaja ya kuku makubwa yaliyonona pamoja na vitamu vinginevyo kama vile firigisi na kuwaachia wale vijana vipapatio.
 Hatimaye mazungumzo yale yalikuwa yakihitimishwa na ujumbe mzito kwa wote, ujumbe uliokuwa ukifikia kila mtu, wake kwa waume, wazee, vijana na hata watoto. Wafanyakazi na wakulima na hata wasiokuwa na kazi. Wasomi na wasiosoma. Kila mtu aliyapenda na kuyafuatilia kwa umakini wa hali ya juu.  
Kwa ujumla Watanzania wote waliyapenda mazungumzo yale ya habari. Ulikuwa ni wakati rasmi wa kufahamu msimamo wa chama na serikali kuhusu jambo fulani. Liwe la kisiasa au la kijamii. Liwe la kitaifa au la kimataifa, Sozigwa alikuwa anatufahamisha msimamo halisi.
 Lakini hitimisho wa ujumbe huu, lilikuwa ni ule usomaji wake wa kipekee. Walikuwa mara kwa mara wakitumiwa wasomaji wenye sauti adimu za mamlaka zenye uwezo wa kuwasilisha ujumbe muhimu kama huu.
Kwa maana hii, na hasa katika siku zile za mwanzoni kabisa, wasomaji wa kipindi hiki walichaguliwa kwa  umakini mkubwa. Hakuwa kila mtu tu anachaguliwa kusoma hata kama ulikuwa msomaji mzuri namna gani.
 Walikuwepo wachache tu waliokuwa na sauti za uzito huu, sauti zilizokubalika kwa mvuto wa aina yake. Nawakumbuka wachache wao wa mwanzoni siku zile. Wa kwanza alikuwa Abdul Baker halafu pia alikuwepo Abdul Ngarawa na baadaye akaja Juma Ngondae. Wakitakiwa kuwasilisha kwa umakini ubunifu huo wa Paul Sozigwa. 
Huyo basi ndiye aliyekuwa mkurugenzi wetu hapo RTD katika mwaka huo wa 1973. Ndiye aliyekuwa ametuita watangazaji wote kwenye mkutano wa aina yake siku hiyo isiyokuwa na jina katika jambo ambalo kamwe hatukulijua.
 Tulikusanyika mapema kama tulivyotakiwa sote kwenye ofisi kubwa ya iliyokuwa idara ya idhaa ya taifa, tukimsubiri mkurugenzi. Mimi nilikuwa bado na stori zangu za Uganda, nikiendelea kuzimwaga kila nilipopata nafasi.
 Kwa hiyo katika siku hii, nilikwenda kuketi nyuma kabisa na baadhi ya wale niliokuwa nimezoeana nao zaidi na kuanza kutia stori zangu hizo. Wala sikustuka sana wakati mkurugenzi alipoingia na kuanza kuzungumza, kwani bado kwa kiasi fulani mimi niliendelea kunong’ona. 
Kwa jumla alizungumza kwa kirefu kuhusu hali ya kisiasa ilivyokuwa nchini wakati ule na wajibu wetu kama shirika la Serikali. Kwa kiasi, alidokeza kuhusu tishio la Idi Amin Dada na pia akatupongeza mimi na Mshindo Mkeyenge kwa kazi nzuri tuliyokuwa tumeifanya kule Uganda.
 Nikiri ya kwamba bado tu sikuwa msikivu hivyo wa yale aliyokuwa akiyazungumza. Kumbe ghafla, mkurugenzi alibadili mazungumzo na kufahamisha ya kwamba menejimenti ilikuwa imeamua kuwa kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya RTD, itatuma watangazaji kufuatana na timu ya wanamichezo wa Tanzania watakaoshiriki kwenye michezo mikubwa ya Jumuiya ya Madola huko Christchurch, New Zealand, mapema mwaka unaofuata wa 1974.
 Mkurugenzi akaendelea kusema kwamba uamuzi huo ulizingatia umaarufu wa Tanzania hasa kwenye michezo ya riadha kufuatia kukua kwa umahiri wa mwanariadha Filbert Bayi.
 Pamoja na yote hayo mimi kule nyuma ya chumba cha mkutano bado nilikuwa naendelea na porojo zangu kiasi ya kwamba sikuweza kumsikia  mkurugenzi aliposema ya kwamba pia menejimenti imewachagua wale inayoamini wanao uwezo mkubwa wa kuifanya kazi hiyo kwa ubora unaotakiwa.
 Kwa mstuko wa wengi kwenye mkutano ule, Sozigwa akalitaja jina la Tido Dunstan Mhando na mwenzangu Abdul Omar Masoud kwamba ndio tulioteuliwa kwa safari hiyo. 
Kwa sababu ambazo sikuzifahamu, Abdul Masoud hakuwepo kwenye mkutano huo, halafu nami sikuwa msikivu wa dhati, kwa hiyo hata sikuwa nimemsikia mkurugenzi alipolitamka jina langu. 
Na kwa kweli ingawaje kwa kiasi nilikuwa nimemsikia alipoanza kuelezea kuhusu uamuzi huo wa kupeleka watangazaji kwenye msafara huo utakaokwenda New Zealand, lakini kamwe, tena niseme kamwe, sikuwa na fikira zozote ya kwamba ingewezekana nikawa mmojawapo.
Hasa kwa kuwa ilikuwa imekwishazoeleka kuwa safari kama hizi zilikuwa zikipewa watangazaji waandamizi; mimi sikuwa miongoni mwao. Kwa hiyo, nilishangaa kuona ghafla macho ya watangazaji wenzangu wote waliokuwemo ndani ya mkutano ule yakinigeukia mimi!  
ITAENDELEA JUMAPILI IJAYO…

Mwananchi news paper