Na Daniel Mjema na Habel Chidawali, 
            (email the author)
    Posted 
    Jumanne,Agosti27 
2013 
saa
21:48 PM
Kwa ufupi
Dk Aman anapingwa kutokana na hatua yake ya 
kuanzisha miradi ya kupima viwanja vya Mji wa Bukoba, ukarabati wa soko 
na ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ambayo inadaiwa kuwa na harufu ya 
ufisadi.
Dodoma. Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi 
(CC-CCM) kimeiomba Serikali kumtuma Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu 
za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kwenda Bukoba, Kagera kuchunguza 
tuhuma dhidi ya Meya wa Manispaa hiyo, Dk Anatory Aman.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini 
Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kamati 
hiyo imewaagiza Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki na Dk Aman 
kurudisha utulivu wa kisiasa katika Manispaa hiyo ambayo katika siku za 
karibuni imekuwa na mgogoro mkubwa.
Alisema Kamati Kuu inaamini kuwa kwa CAG kwenda 
Bukoba kutasaidia kujulikana kwa mambo anayolalamikiwa ili ukweli 
ujulikane na hatua stahiki zichukuliwe.
Alisema CAG ametakiwa kwenda haraka Bukoba na uchunguzi unatakiwa kufanyika katika kipindi cha muda mfupi kuanzia jana.
“Hivi ninavyozungumza ama CAG ameondoka kuelekea 
Bukoba au yuko katika maandalizi ya kwenda Bukoba kufanya uchunguzi huo 
na ukweli utajulikana. Hatuna hofu juu ya kwenda CAG maana katika kikao 
hiki yupo Waziri Mkuu na vyombo vingine kwa hiyo wamewasiliana naye,” 
alisema Nape.
Nape alisema wamelazimika kuitaka Serikali kumtuma
 CAG kwa kuwa tume iliyotangulia iliyomhusisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, 
Abbas Kandoro na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi haikuwa ya 
kiuchunguzi, bali ilishughulikia suala la migogoro.
Alisema kuwa taarifa ya uchunguzi huo inapaswa 
kupelekwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba ili 
waijadili na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji 
wa halmashauri hiyo.
Dk Aman anapingwa kutokana na hatua yake ya 
kuanzisha miradi ya kupima viwanja vya Mji wa Bukoba, ukarabati wa soko 
na ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ambayo inadaiwa kuwa na harufu ya 
ufisadi.
Madiwani wapeta
Akizungumzia kubatilishwa kwa uamuzi wa 
Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Kagera wa kuwafukuza uanachama 
madiwani wanane wa Manispaa ya Bukoba, Nape alisema uamuzi huo ulikiuka 
Katiba ya CCM ya mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.
Alitaja kifungu kilichokiukwa kuwa ni Ibara ya 93 
(15) ambacho kinataka CC kujulishwa uamuzi huo kabla ya kuchukuliwa kwa 
hatua hiyo.
“Kamati Kuu inawataka madiwani wa CCM wa Manispaa 
ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba na Meya wa Manispaa hiyo kurudisha utulivu 
katika halmashauri yao. Pia kurudisha mshikamano katika chama ili Ilani 
ya CCM itekelezwe kama ilivyokusudiwa,” alisema Nape.
Mgogoro katika halmashauri hiyo ulikiweka njiapanda CCM baada ya
 kutoa uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao Agosti 13, mwaka huu hali 
iliyoilazimu Kamati Kuu kuingilia kati na kuwahoji viongozi wote 
waliohusika akiwamo Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamisi Kagasheki, Dk
 Aman na viongozi wa mkoa wa wilaya.
Madiwani waliokuwa wamefukuzwa ni Richard Gaspar 
(Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye
 pia ni Naibu Meya (Buhembe) na Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert 
Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro), Dauda Kalumuna 
(Ijuganyondo) na Yussuf Ngaiza (Kashai).
source: Mwananchi
source: Mwananchi