Wajumbe wa Baraza la Katiba kutoka Jumuiya na Taasisi za Kiislamu 
Tanzania wakipitia vifungu mbalimbali vya Rasimu ya Katiba Mpya Dar es 
Salaam, jana. Picha na Venance Nestory 
            
Kwa ufupi
Alisema Waislamu wengi waliotoa maoni yao 
kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walitaka kuwapo kwa mahakama hiyo 
lakini cha kushangaza tume hiyo iliyatupa.
Dar es Salaam. Wajumbe wa 
Baraza la Katiba la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, wametaka 
kipengele cha Mahakama ya Kadhi kiwekwe kwenye Katiba Mpya.
Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za 
Kiislam, Sheikh Mussa Kundecha, alisema jana kuwa ingawa rasimu ya 
Katiba haina kupengele hicho, lakini wao wanaona hiyo ni haki yao.
“Tunataka kipengele cha Mahakama ya Kadhi kiwekwe 
Katiba Mpya na  iendeshwe na kugharamiwa na Serikali,” alisema Sheikh 
Kundecha wakati wajumbe hao walipokuwa wakijadili rasimu ya Katiba.
Alisema Waislamu wengi waliotoa maoni yao kwenye 
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walitaka kuwapo kwa mahakama hiyo lakini 
cha kushangaza tume hiyo iliyatupa.
“Sasa licha ya kwamba kipengele hicho hakipo kwenye rasimu, bado tunaendelea na kilio chetu cha kutaka kiwekwe,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya 
Katiba, Jaji Joseph Warioba, wiki iliyopita alisema kipengele ambacho 
hakipo kwenye rasimu hakitawekwa kwenye Katiba Mpya.
Sheikh Kundecha alihoji iweje kuwe na Mahakama za 
Biashara inazoendeshwa na Serikali, wakati kuna Watanzania wachache 
ambao ni wafanyabiashara.
“Kuna wafanyabiashara wachache lakini wana 
mahakama yao, kunakuwa na ugumu gani kuweka Mahakama ya Kadhi  kwa ajili
 ya Waislamu?” alihoji Kundecha. Mwaka jana, Serikali iliruhusu 
kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi ambayo iko nje ya mfumo  wa Serikali.
source: Mwananchi news paper
source: Mwananchi news paper