Saturday, 7 September 2013

M23 yakubali mazungumzo na Serikali


Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Septemba7  2013  saa 11:51 AM
Kwa ufupi
Utayari huo unatokana na agizo lililotolewa baada ya mkutano wa wakuu hao wa nchi kukubaliana kwamba ni vyema Serikali ya DRC ikirejea kwenye mazungumzo na M23 kwa ajili ya kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani.


Munyonyo. Kundi la wapiganaji wa M23 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limesema kwamba lipo tayari kukutana na Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za maziwa makuu uliofanyika Uganda juzi.
Utayari huo unatokana na agizo lililotolewa baada ya mkutano wa wakuu hao wa nchi kukubaliana kwamba ni vyema Serikali ya DRC ikirejea kwenye mazungumzo na M23 kwa ajili ya kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani.
Katika mkutano huo uliofanyika huko Munyonyo, Uganda, wakuu hao wa nchi walisema kwamba ni vyema mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa M23 yakasitishwa kwa sasa ili kutoa mwanya wa mazungumzo.
Mkutano huo uliitishwa na Rais Yoweri Museveni ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Mkutano wa Kimataifa wa Nchi za Maziwa Makuu, ambao ni chombo muhimu katika kuangalia masuala ya amani na usalama kwa nchi 12 wanachama.
Mwaka jana, Serikali ya DRC na M23 walianza mazungumzo ya kutafuta amani chini ya Serikali ya Uganda lakini yalikwama huku M23 wakiituhumu Serikali kwa kukataa kutoa ushirikiano.
Kiongozi wa kundi hilo Bertrand Bisimwa aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba wapo tayari kufanya mazungumzo hayo ili kufikia mwafaka.
“Wawakilishi wetu wapo tayari Kampala na wameshakubaliana kwamba watazungumza kuhusu amani na viongozi hao wawili wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,” alisema Bisimwa.
Naye msemaji wa DRC, Lambert Mende , alisema kwamba Serikali imefurahia suala la kukubali kwa viongozi wa Kundi la M23 kufanya mazungumzo hayo.
Alisema Serikali na M23 wanatakiwa kukubaliana namna ya kuiweka DRC katika hali ya usalama kwani raia wengi wameshapoteza maisha mpaka sasa, huku wengine wakiishi bila amani.
M23 waliuvamia mji wa Goma Mashariki mwa DRC Novemba mwaka jana lakini jeshi la DRC likisaidiwa na kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa kwa ajili ya DRC, Monusco, ziliweza kuudhibiti mji huo.
Rwanda imeshutumiwa kwa kuwaunga mkono M23 madai ambayo hata hivyo iliyakanusha vikali.
Viongozi wa M23 walitangaza kusitisha mapigano wiki iliyopita wakisema wako tayari kushiriki katika kupatikana amani nchini humo.

Mazungumzo kati ya Serikali na kundi hilo yalisambaratika mwezi Mei mwaka jana. Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kanda ya maziwa makuu, Mary Robinson, yuko ziarani katika kanda hiyo.
M23 imetokana na askari Watutsi, ambao walitoka katika jeshi la nchi hiyo Aprili mwaka jana, ambapo inadaiwa walichukua silaha nyingi kutoka jeshini kabla ya kujitenga ambazo ndizo wanazitumia mpaka leo.
Wakati huohuo, Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimeelezea uwezekano wa kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya M23.
Msemaji wa vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Kongo Felix Basse alisema kuwa, vikosi hivyo vya Umoja wa Mataifa vinafanya juhudi za kurejesha usalama katika maeneo yaliyokombolewa kutoka mikononi mwa wapinzani.
Harakati za makundi ya wapinzani hususan M23 mkoani Kivu Kaskazini, zimezorotesha hali ya usalama wa eneo hilo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa eneo la Maziwa Makuu Barani Afrika wametaka kusitishwa mashambulio dhidi ya M23 , Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kutoa mwanya kwa mazungumzo ya amani yanayofanyika Kampala, Uganda.

source: Mwnanachi