Saturday, 7 September 2013

Mbunge ‘Sugu’ awachenga Polisi Dodoma


Na Daniel Mjema, Mwananchi

Posted  Septemba7  2013  saa 11:40 AM
Kwa ufupi
Mbunge huyo kijana alifanikiwa kuwapiga chenga ya mwili (kutoroka) polisi hao waliokuwa wametanda eneo la Bunge juzi, mahususi kwa lengo la kumkamata lakini aliwatoroka bila wao kumtambua.


Dodoma. Polisi mkoani Dodoma, wanaumiza vichwa namna ya kumpata Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) wanayemtafuta kwa udi na uvumba kwa tuhuma za kumpiga Polisi wa Bunge.
Mbunge huyo kijana alifanikiwa kuwapiga chenga ya mwili(kutoroka) polisi hao waliokuwa wametanda eneo la Bunge juzi, mahususi kwa lengo la kumkamata lakini aliwatoroka bila wao kumtambua.
Habari za uhakika zilizopatikana jana na juzi, zilisema tayari polisi wamesambaza taarifa ya simu ya upepo katika mikoa ya jirani ya Morogoro na Singida ili wamkamate watakapomuona.
Polisi hao wa Bunge na makachero wengine, juzi jioni walitanda katika Viwanja vya Bunge kwa lengo la kumkamata lakini mavazi aliyokuwa ameyavaa mbunge huyo yakawachanganya wasimtambue.
“Unajua Polisi walikuwa wamejiandaa wakijua Sugu (Mbilinyi) angefika jioni kipindi cha Bunge akiwa amevaa suti aliyovaa asubuhi yake, lakini akaja na mavazi tofauti kabisa,”kilidokeza chanzo chetu.
Sugu alifika eneo hilo la Bunge juzi saa 11:00 jioni akiwa katika gari la Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB), Freeman Mbowe na kushiriki mkutano wa wanahabari Ukumbi wa Msekwa.
Akizungumza na gazeti hili juzi kabla ya mkutano huo na wanahabari, mbunge huyo alisema, tayari amepata taarifa ya kuwapo maagizo ya yeye kukamatwa lakini akasema yuko tayari kutetea haki yake.
“Nimeambiwa OC-CID (mkuu wa upelelezi) ametoa maagizo nikamatwe eti kwa kumpiga Polisi… Mimi nashangaa sana kwa sababu mimi ndiye niliyepigwa lakini natakiwa kukamatwa,”alisema.
Haifahamiki aliwezaje kuwatoroka polisi na kufanikiwa kuondoka lakini waliendelea kuganda viwanja vya Bunge hadi saa 3:00 usiku wakiamini bado alikuwa ofisi za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Susan Kaganda, jana alilithibitishia gazeti hili kumsaka mbunge huyo kwa mahojiano na kwamba tayari taarifa hiyo wameiwasilisha kwa Katibu wa Bunge.
“Ni kweli tunamhitaji kwa ajili ya mahojiano na kama unavyojua utaratibu unavyosema lazima uliarifu Bunge na sisi tayari tumemuandikia katibu wa Bunge ili amtaarifu (Mbilinyi) ili aje,”alisema Kaganda.
Juzi jioni wakati akiahirisha Bunge, Ndugai alisema mbunge huyo amefanya vitendo vya aibu kwa kumpiga kichwa na kumchania sare polisi mmoja wa Bunge na kuharibu kipaza sauti cha Bunge.

Wakati Ndugai akisema hivyo, jana Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka aliomba mwongozo wa Spika kuhusu Mbilinyi kujichukulia sheria na kumpiga Polisi nje ya ukumbi.
Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama alisema atautolea maamuzi mwongozo huo baada ya kushauriana na Wanasheria wa Bunge na viongozi wa taasisi nyingine zinazoshabihiana na hilo.
Kiini cha kutafutwa kwa mbunge huyo ni vurugu zilizotokea juzi mchana ndani ya ukumbi wa Bunge baada ya Naibu Spika ,Job Ndugai kuwaamuru polisi kumtoa kwa nguvu kiongozi wa Upizani,Mbowe.

source: Mwananchi