Saturday, 7 September 2013

Sumatra wahimiza matumizi ya vitambulisho kwa wasafiri


Na Frederick Katulanda, Mwananchi

Posted  Septemba7  2013  saa 11:41 AM
Kwa ufupi
Akizungumza na waandishi wa habari jana,Meneja wa Sumatra Kanda ya Ziwa, Mhandisi Japhet Ole Loisuimaye alisema, utaratibu huo umelenga kuhakikisha kuna kuwa taarifa za kina kwa kila abiria anayesafiri na meli ama boti ndani ya Ziwa Victoria.


Mwanza. Mamlaka ya Usafirishaji ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra),imeagiza wasafirishaji wanaotumia vyombo vya majini kanda ya ziwa kupitia Bandari zote Ziwa Victoria kusafirisha abiria mwenye kitambulisho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,Meneja wa Sumatra Kanda ya Ziwa, Mhandisi Japhet Ole Loisuimaye alisema, utaratibu huo umelenga kuhakikisha kuna kuwa taarifa za kina kwa kila abiria anayesafiri na meli ama boti ndani ya Ziwa Victoria.
Alisema utaratibu huo utaanza kutumika Septemba 9, mwaka huu na kubainisha kwamba kila abiria atapaswa kuwa na moja kati ya kitambulisho kifuatacho, Kitambulisho cha Uraia, cha Ukaazi, Paspoti, cha Kupigia Kura, Kazi, Leseni ya Udereva ama kwa wale wasiokuwa na hivyo vyote basi wawe na barua toka Serikali za Mitaa yenye picha.
“Agizo hili limetolewa na Serikali kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na kumbukumbu sahihi za abiria (passenger manifest) wote wanaosafiri na meli ama boti kwa umbali usiozidi maili za majini (noutcal miles) 20 kati ya bandari, hivyo agizo hili halitawahusu abiria wanaosafiri na vivuko,” alifafanua. Alisema agizo hilo linapaswa kufuatwa na wasafirishaji wote kwa vile ni utekelezaji wa Kanuni za Kuhakiki na kusajili abiria kama zilivyoainishwa.

source: Mwananchi