Saturday, 7 September 2013

Dakika 90 zatumika kupitisha muswada


Mbunge wa Mkoani, Zanzibar (CUF) akiomba mwongozo wa Spika kutaka Bunge liondoe Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliosababisha vurugu bungeni Juzi. Picha na Fidelis Felix 
Na Daniel Mjema, Mwananchi

Posted  Septemba7  2013  saa 11:43 AM
Kwa ufupi
Hata hivyo, muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM na mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP) huku wabunge wa vyama vingine vya upinzani wakiususia.


Dodoma. Dakika 90 zilitosha kwa Bunge jana kupitisha muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya mabadiliko ya Katiba na sasa Rais Jakaya Kikwete ndiye anayesubiriwa kutia saini ili uwe sheria.
Hata hivyo, muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM na mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP) huku wabunge wa vyama vingine vya upinzani wakiususia.
Vyama vilivyosusia majadiliano na upitishaji wa muswada huo ni Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kutokana na kile walichosema kuwa ni kukiukwa kwa kanuni na utaratibu mzima wa mchakato wake. Wabunge walikaa kama Kamati ya Bunge zima kuanzia saa 6:30 mchana na ilipofika saa 8:00 mchana, muswada huo ulikamilika kwa hatua zote.
Wakati wabunge wa upinzani wakiwa wametoka nje, Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda na Clara Mwaituka (CUF) walikuwepo bungeni hadi Bunge lilipofikia kuwa kamati ndipo walitoka ndani ya ukumbi.
Hata hivyo, Serikali ilikubali mapendekezo ya wabunge kikiwemo kifungu kilichohusu taasisi kupeleka majina kwa Rais ili ateue mjumbe mmoja kuingia katika Bunge Maalumu la Katiba.
Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Mathias Chikawe alisema kutokana na Serikali kuridhia mapendekezo hayo ya wabunge, sasa taasisi hizo zitapeleka majina tisa ili Rais ateue jina moja.
Hata hivyo pamoja na kupeleka majina hayo tisa, sheria haitambana Rais kwamba ni lazima ateue mmojawapo kutoka katika orodha hiyo na idadi ya wajumbe kutoka taasisi hizo haitazidi 166.
Pia Serikali iliridhia pendekezo la wabunge la kuondoa takwa la lazima la mwombaji wa nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba kwamba awe na ama shahada ya sheria, uchumi ama sayansi ya siasa. Chini ya mabadiliko hayo sasa, mwombaji wa nafasi hiyo sasa atatakiwa kuwa na shahada kutoka katika chuo kikuu chochote kinachotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).
Pia Serikali imeridhia kukifanyia marekebisho kifungu kinachohusu ukomo wa Bunge la Katiba kutoka siku 90 zilizokuwa zimependekezwa awali na sasa suala hilo litakuwa mikononi mwa Rais.
Wakati wa mchakato huo, suala la wabunge wa upinzani kutoka nje na kususia vikao vya Bunge liliendelea kuchomoza, huku Serikali ikisisitiza kwamba Zanzibar ilishiriki kikamilifu katika kutoa maoni ya mabadiliko hayo
 
 
source: Mwnanachi