Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Septemba7 2013 saa 12:0 PM
Posted Septemba7 2013 saa 12:0 PM
Kwa ufupi
Marekani yahaha kutafuta kuungwa mkono kuhusu 
uamuzi wake wa kuivamia kijeshi. Urusi yashikilia msimamo wa kuzuia 
uvamizi wa kijeshi.
St Petersburg. Viongozi wa nchi zenye nguvu 
zaidi kiuchumi duniani wameshindwa kuafikiana kuhusu mzozo wa Syria 
katika mkutano unaofanyika nchini Urusi, huku Marekani ikitafuta 
uungwaji mkono kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria.
Katika mkutano huo wa mataifa hayo makubwa 
kiviwanda (G20) uliofanyika huko Petersburg, Urusi, suala la namna ya 
kuchukua hatua katika mgogoro unaoendelea nchini Syria ndilo 
lililotawala agenda za mkutano huo, ambao ni maalumu kwa ajili ya 
masuala ya uchumi na biashara.
Kumekuwa na mikutano ya dharura miongoni mwa pande
 mbili zinazotofautiana kuhusu namna ya kuchukua hatua kwenye mgogoro 
huo, ambapo Rais Barack Obama wa Marekani na Vladmir Putin wa Urusi 
wamekuwa wakijaribu kutafuta ushawishi kwa ajili ya kuungwa mkono.
Hadi jana mchana, viongozi waliopata fursa ya 
kulizungumzia suala hilo la Syria walisema hakukuwa na maafikiano kuhusu
 hatua za kuchukuliwa, ambapo Waziri Mkuu wa Italia, Enricco Letta, 
alithibitisha kupitia mtandao wa Twitter kuwa hakukuwa na maafikiano 
kuhusu mzozo wa Syria.
Urusi imekuwa ikisimama kidete kuhusu 
kutochukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad 
kuhusiana na madai kuwa ulitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake 
Agosti 21.
Hadi jana mchana, Rais Barack Obama alikuwa 
akiendelea na jukumu lake la kutaka kuungwa mkono kuhusu kuichukulia 
Syria hatua za kijeshi, ambapo aliweza pia kukutana na Rais wa China 
pembezoni mwa mkutano huo na baadaye kukutana na mshirika wake, Rais wa 
Ufaransa, Francois Hollande.
Mjumbe wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa, Samantha 
Power, ameishutumu Urusi kwa kulishika mateka Baraza la Usalama la Umoja
 wa Mataifa (UN) kwa kutumia kura yake ya turufu. Waziri Mkuu wa 
Uingereza, David Cameron, naye alisema nchi yake ina ushahidi mpya 
kuhusu shambulio hilo la kemikali.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), 
Ban Ki-Moon, aliwaambia viongozi hao wa G20 kuwa kutoa silaha kwa upande
 wowote katika mzozo wa Syria sio suluhisho kwani hatua za kijeshi 
haziwezi kuwa suluhisho la mzozo huo.
Washirika wa Syria bado hawaonekani kushawishika na kampeni za Obama za kuchukuliwa hatua za kijeshi.
Papa Francis ataka suluhisho
Wakati mkutano huo ukiendelea, kiongozi wa Kanisa 
Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, pia ameelezea hisia zake 
kuhusu mzozo huo na kutoa wito kutafutwe suluhisho la amani na wala si 
kwa kutumia nguvu za kijeshi akionya hatua za kijeshi zitaambulia patupu
 katika kuumaliza mzozo wa Syria.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, pia alisema 
mara kadhaa kuwa nchi yake haitashiriki katika shambulio la kijeshi 
litalaoongozwa na Marekani dhidi ya Syria na tayari Bunge la Uingereza 
lilipiga kura kupinga nchi hiyo pia kuhusika katika hatua hiyo.
Mkutano huo wa G20 uliofanyika kwa siku mbili ulimalizika jana 
ambapo Rais Putin aliyekuwa mwenyeji alipanga muda maalumu kujadili 
mzozo huo katika chakula cha usiku wa juzi, licha ya kuwa Syria haikuwa 
katika ajenda.
Utawala wa Syria umekuwa ukishutumiwa kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wakati wa mzozo huo uliodumu miezi 30 sasa.
source: Mwananchi
source: Mwananchi