Askari wa Kikosi cha Zimamoto wakipambana kulizima jengo la kanisa la
Jeshi la Ukombozi lililotiwa kiberiti na waandamanaji mjini Mombasa leo
mchana. PICHA | AFP
Na AFP
Posted Ijumaa,Oktoba4 2013 saa 17:56 PM
Posted Ijumaa,Oktoba4 2013 saa 17:56 PM
Kwa ufupi
- Hali ilianza kuonekana tete toka leo asubuhi,
ambapo wanausalama wa Kenya walionekana wakijaribu kuboresha ulinzi
katika mitaa mbali mbali ya mji wa Mombasa kufuatia mauaji ya Omar.
Mombasa. Watu 4 wameuawa
na wengine 7 kujeruhiwa mjini Mombasa katika ghasia zilizoanza baada ya
swala leo mchana kufuatia mauaji ya Shehe Ibrahim ‘Rogo’ Omar na
wenzake watatu jana.
Shehe ‘Rogo’ Omar na wenza walifariki baada ya
gari walilokuwa wakisafiria kumiminiwa risasi likiwa njiani kwenye
barabara ya Malindi-Mombasa, katika shambulizi linaloolekana lilikuwa
limepangwa ili kuwatoa roho.
Mkuu wa polisi katika eneo la Kisauni, Jolius
Wanjohi alithibitisha mauaji hayo ya Shehe Omar, lakini akashindwa kutoa
maelezo zaidi, hali iliyochochea hisia za wafuasi wa mhubiri huyo na
kusababisha waingie mtaani mapema mchana wa leo.
Hali ilianza kuonekana tete toka leo asubuhi,
ambapo wanausalama wa Kenya walionekana wakijaribu kuboresha ulinzi
katika mitaa mbali mbali ya mji wa Mombasa kufuatia mauaji ya Omar.
Hata hivyo kufikia mchana, waandamanaji waliokuwa
wakijikusanya katika vikundi vidogo vidogo waliingia barabarani kwa
ghadhabu, wakirushia magari mawe na kuwasha moto huku wakipambana na
polisi.
Angalau mmoja kati ya waliokufa katika vurugu hizo
alipigwa risasi, kwa mujibu wa Red Cross Kenya, huku magari na kanisa
la Jeshi la Ukombozi (Salvation Army) katika wilaya ya Majengo vikitiwa
kiberiti.
Shirika la habari AFP linaripoti marehemu wengine
yaonekana walikufa baada ya kuchomwa na vitu vyenye ncha kali katika
vurumai hiyo, likimnukuu msemaji wa Kituo cha Kukabiliana na Matukio ya
Hatari nchini Kenya.
Polisi wanadai walilazimika kutumia mabomu ya
machozi kuwatawanya waandamanaji katika viunga vya Majengo – eneo ambalo
wanaishi Wakenya wa kada ya kati, wengi wao wakiwa waumini wa dini ya
Kiislamu.
Huku Maimamu na viongozi wa kijamii wakiomba
utulivu, baadhi ya mashuhuda wameiambia AFP kuwa polisi walionekana
wakipiga risasi za moto hewani wakati wakijaribu kudhibiti vurugu hizo.
Kamanda wa polisi mjini Mombasa, Kipkemoi Rop,
amethibitisha wamewakamata watu 24 kufuatia ghasia za leo mchana,
akisisitiza jeshi lake halitavumilia “vikundi vya vijana wahuni
kuukamata mji [wetu].”
Marehemu Omar alikuwa mhubiri katika msikiti wa
Musa, na alikuwa mwandani wa mhubiri mwingine machachari wa Kenya, Shehe
Aboud Rogo Mohammed ambaye pia aliuawa katika tukio lisiloeleweka
Agosti, 2012.
Tukio hili la jana lilikuja katika kipindi kigumu
kwa wakazi wa Kenya, wengi wao wakiwa wamejawa hofu kufuatia shambulizi
la jumba la biashara la Westgate wiki mbili tu zilizopita – tukio hatari
lililoacha vifo zaidi ya 67 na kusababisha hatihati jijini Nairobi.
Shehe Omar anashutumiwa kuwa na uswahiba wa karibu sana na
wanamgambo wa Kisomali wa Al-Shabab ambao wamekiri kuhusika katika
uvamizi wa Westgate.
Baadhi ya Waislamu mjini Mombasa wamevilaani
vyombo vya dola, wakivituhumu kwa kuchukua ‘hatua za makusudi’ kumwinda
Shehe Omar na wenzake kama sehemu ya vita yao dhidi ya ugaidi – kauli
ambayo serikali ya Kenya imeikataa katakata.
SOURCE: MWANACHI