Rais Dkt.Jakaya Kikwete akisalimiana na Tundu Lissu Chadema. Nyuma ni James Mbatia NCCR Mageuzi. 
            
    Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba16 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
- Rais Kikwete alionekana mwenye furaha tele wakati alipokutana na viongozi wa vyama hivyo na kivutio zaidi ilikuwa pale alipokutana na Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani, Tundu Lissu.
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete na viongozi 
wa vyama vya siasa vya CCM, Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP na UDP 
wamekubaliana mambo mawili makubwa baada ya kuweka pembeni tofauti za 
kiitikadi na kutanguliza masilahi ya taifa walipokutana jana Ikulu 
jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliitishwa na Rais Kikwete ili kuondoa
 sintofahamu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko
 ya Katiba uliopitishwa Septemba na Bunge lilipokutana mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano 
Ikulu jana jioni ilisema katika mkutano huo ilikubaliwa kwamba vyama 
vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha 
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe 
mapendekezo yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya kuyashirikisha 
mapendekezo hayo katika marekebisho ya sheria hiyo.
Pia Rais na vyama hivyo walikubaliana kwamba vyama
 vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, 
viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na 
maridhiano kwa lengo la kusukuma mbele mchakato huo kwa masilahi mapana 
ya nchi yao na mustakabali wa taifa.
“Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa 
jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa 
vyama hivyo na wadau wengine nchini,” iliongeza taarifa hiyo.
Viongozi wa vyama vyama vya siasa waliohudhuria 
mkutano huo ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa
 Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip 
Mangula, Isaack Cheyo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo
 na Nancy Mrikaria ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa TLP, Augustine 
Mrema. Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.
Wengine ambao waliambatana na wenyeviti wao ni 
Mohamed Mnyaa na Julius Mtatiro wa CUF, Tundu Lissu na John Mnyika wa 
Chadema na Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.
Vicheko Ikulu
Vicheko na bashasha vyatawala Ikulu
Ilikuwa fursa kwa Rais Kikwete kukutana na 
viongozi hao baada ya kipindi cha miezi miwili cha kurushiana maneno 
baina ya viongozi wa Bunge, Serikali, CCM waliokuwa wakivutana na 
viongozi wa vyama vitatu vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi.
Kama mtu yeyote angeulizwa kutabiri katika tukio 
lililotokea jana lingetokea basi angekuwa na wakati mgumu kutokana na 
ukali wa maneno na malumbano katika kipindi chote baada ya kumalizika 
kwa mkutano wa Bunge wa Septemba.
Rais Kikwete alionekana mwenye furaha tele wakati alipokutana na
 viongozi wa vyama hivyo na kivutio zaidi ilikuwa pale alipokutana na 
Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani, Tundu Lissu.
Viongozi hao walisalimiana huku wote wakitabasamu 
na kuashiria kuwa waliamua kuweka tofauti zao pembeni na kuangalia 
masilahi ya nchi.
Kumbuka katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi 
Septemba, Rais Kikwete alimshutumu Lissu kwa kusema kwamba katika uteuzi
 wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa yeye hakuheshimu mawazo
 ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo 
Tanzania (CCT).
Rais Kikwete alikaririwa akisema kauli hiyo ya 
Lissu ni uzushi, uongo na uzandiki wa hali ya juu, huku akisisitiza kuwa
 mbunge huyo alitoa kauli hiyo ili kupotosha ukweli na pengine isaidie 
kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la 
Katiba.
Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, 
alipinga tuhuma hizo na kusisitiza Rais aliteua wajumbe wa Tume ya 
Mabadiliko ya Katiba kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Jumuiya
 ya Kikristo Tanzania (CCT) bila ya ridhaa yao.'
Chikawe, Wassira na Lukuvi ndani
Mawaziri watatu, ambao walitetea kwa nguvu kupitishwa kwa muswada ule ndani na nje ya Bunge walihudhuria mazungumzo hayo.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu 
anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, Waziri wa 
Sheria na Katiba, Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais
 anayeshughulikia Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira walikuwemo 
kwenye mazungumzo ya jana.
Mawaziri hawa kwa nyakati tofauti walitetea kuwa 
mchakato wa muswada ule haukuwa na matatizo yeyote na kushikilia kuwa 
lazima Rais lazima asaini muswada kwani ulikuwa umepitishwa kihalali na 
Bunge.
Pia walikuwa wameshikilia kuwa safari hii kulikuwa hakuna mambo ya mazungumzo kati ya Rais na upinzani.
Chanzo cha sintofahamu
 SOURCE: MWANANCHI
Wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walisusia 
mjadala wa muswada huo wakipinga matayarisho yake kutoshirikisha upande 
wa Zanzibar na pia walikuwa hawakubaliani na baadhi ya vipengele vya 
muswada huo.
Katika hatua nyingine, taarifa kutoka Ikulu 
zilisema kwamba Rais Kikwete alisaini muswada huo tangu Oktoba 10 mwaka 
huu siku ambayo wapinzani walipanga kufanya maandamano nchi nzima.
Katika mahojiano na Mwananchi jana jioni, 
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema muswada huo 
tayari ulikwishasainiwa na Rais na kama kuna marekebisho yatafanywa.
Mwananchi ilimtafuta Rweyemamu baada ya kusikia 
akithibitisha kusainiwa kwa muswada huo katika mahojiano na BBC Idhaa ya
 Kiswahili jana.
Akizungumza na Mwananchi Rweyemamu alisema, “Rais 
ameshasaini tangu Oktoba 10, unajua kulikuwa hakuna tatizo lolote kuhusu
 muswada huu kwa sababu ulifuata taratibu zote bungeni.”
Rweyemamu alisema kuwa awali Ikulu ilitoa taarifa kuwa Rais atakutana na wapinzani, pia atausaini muswada huo.
“Muswada umepitishwa bungeni na yeye amekamilisha 
kazi kwa kuusaini ili kuwa sheria. Alipokutana na wapinzani leo (jana) 
amewaeleza hilo na wameridhika” alisema Rweyemamu.
