Na Fredy Azzah, Mwananchi
Posted Novemba2 2013 saa 8:34 AM
Posted Novemba2 2013 saa 8:34 AM
Kwa ufupi
Baadhi ya wadau hao wakizungumza na gazeti hili
jana, walisema Tanzania imeweka rekodi kwa nchi za Afrika kwa kuwa na
kiwango kidogo sana cha ufaulu cha alama F kuanzia 0 mpaka 19.
Dar es Salaam. Siku moja baada
ya Serikali kutangaza kupunguza viwango vya ufaulu kwa mtihani ya kidato
cha nne na sita, baadhi ya wasomi na wadau wa elimu wameponda uamuzi
huo na kusema una malengo ya kisiasa.
Baadhi ya wadau hao wakizungumza na gazeti hili
jana, walisema Tanzania imeweka rekodi kwa nchi za Afrika kwa kuwa na
kiwango kidogo sana cha ufaulu cha alama F kuanzia 0 mpaka 19.
Walisema, Serikali imechukua uamuzi huo kisiasa
ili kuhakikisha kuwa, wanatimiza lengo la Mpango wa Maendeleo Makubwa
Sasa (BRN), ambalo ni kuhakikisha matokeo ya ufaulu kwa Mtihani wa
Kidato cha Nne mwaka huu yanafikia asilimia 60 kutoka 33 ya mwaka jana.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Herme Mosha alisema kuwa kilichofanywa na Serikali ni
kupanua wigo wa watu kufaulu.
“Wanataka watu ambao walikuwa wanapata daraja la
nne wapate daraja la tatu, daraja la tatu wapate la pili na la pili
wapate la kwanza.
Hata hivyo, kwa muda wote, wadau wa elimu ambao
wanataka siyo kuona tu watu wanafaulu, wanataka elimu iliyo bora. Kwa
hatua hii waliyoichukua haitasaidia lolote katika kuongeza ubora wa
elimu ambao umekuwa kilio cha muda mrefu,” alisema Profesa Mosha.
Alisema kuwa, washikadau wengi wangependa kuona ubora wa elimu umeongezeka na siyo kuongeza wigo wa ufaulu.
“Huku ni kujidanganya, jambo la kwanza wangetakiwa
waende katika shule mbalimbali waone ni nini walimu wanataka, tatizo
lipo wapi halafu wachukue hatua kwa sababu ukiangalia sasa ni kama kuna
mgomo fulani hivi,” alisema.
Kwa upande wake Dk Kitila Mkumbo ambaye ni Mkuu wa
Idara ya Saikolojia ya Elimu na Masomo ya Mitalaa ya Shule Kuu ya Elimu
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema tatizo la elimu Tanzania
halijawahi kuwa ni viwango vya ufaulu.
“Wanataka tu kuona hiyo asilimia 60 waliyojipangia
inafikiwa. Walijiwekea lengo hilo wakijua kabisa kwenye elimu hakuna
miujiza, lazima mtu ufanye kazi ndiyo matokeo yaonekane,” alisema.
Alisema kiwango cha kufeli kilichowekwa kinaifanya Tanzania kuwa nchi yenye viwango vidogo sana vya elimu kwenye bara hili.
“Burundi wenyewe mtoto akipata 50 ndiyo anakuwa
amefeli, sisi huku tumeweka mpaka 19 ndiyo tunasema amepata hiyo F,
lakini bado tunaita amefaulu, huu ni utani,” alisema.
SOURCE: MWANANCHI
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT), Ezekia Oluoch alisema Matumizi ya Alama za Maendeleo ya
Mwanafunzi (CA) ni suala la kupongeza.
Hata hivyo, alisema kuwa kuna matatizo ya msingi kwenye elimu na ni lazima yafanyiwe kazi.
“Lengo lao la kushusha ufaulu ni ili ionekane kuwa BRN imefikia lengo, watoto wamefaulu ndiyo iwe furaha yao,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo
Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema wamepokea suala
hilo kwa mikono miwili.
“Zamani mtu alikuwa amapata sifuri na mwingine 33
wote tunasema wamepata F, lakini sasa kuna utofauti kwa hiyo unaweza
kuona ni namna gani uwatumie hawa watu.
Pia suala hili linatoa mwanya mpana hata kwa
Serikali na taasisi nyingine za elimu, ikitokea kwamba watu wa C
wamekosekana unaweza kuona sasa tutumie wapi,” alisema.
Alisema kuwa, kwa sasa sera ya elimu inasema watu
watakaoingia kidato cha tano wanatakiwa wawe na C tatu, lakini mwaka huu
Serikali ilichukua C moja na D mbili wakaenda kidato cha tano.
“Yote hii ni kwa sababu hakukuwa na njia mbadala, lakini kwa sasa kutakuwa na mianya mingi sana.
Hata hivyo, tujue kuwa, tatizo la elimu Tanzania
halikuwa madaraja, hii ilikuwa ni sehemu tu, lazima tuhakikishe
tunatafuta matatizo ya msingi ya elimu yetu tuyafanyie kazi. Tukibaki
kwenye hizi alama, basi nchi yetu itakwenda shimoni,” alisema.
SOURCE: MWANANCHI