Na Beatrice Moses na Raymond Kaminyonge
(email the author)
Posted Alhamisi,Agosti22 2013 saa 19:54 PM
Posted Alhamisi,Agosti22 2013 saa 19:54 PM
Kwa ufupi
Alikariri maneno yaliyorekodiwa kwenye Hansard ya Bunge yaliyosemwa na viongozi hao watatu.
Dar es Salaam. Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema itawafikisha kwenye Kamati ya
Maadili ya Bunge, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri
wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akiwatuhumu kwa kulidanganya Bunge.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mwenyekiti wa PAC,
Zitto Kabwe baada ya kumhoji Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi
Herbert Mrango kuhusu hati ya mashaka waliyoipata kutoka kwa Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka wa fedha 2011/2012.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti ya mwaka
huo kiasi cha Sh348,075,000,000 fedha za ndani zilizokuwa zimetengwa
chini ya fungu lililotajwa kuwa ni la mradi maalumu (Special Road
Construction Project) hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa bungeni.
“Ni vizuri leo uiambie kamati fedha hizi ziliombwa
kwa kitu gani na zilitumika kwa jambo gani. Tunajua kwamba fedha hizi
zilipunguzwa kiasi cha Sh95 bilioni na kupelekwa Wizara ya Uchukuzi,
zilibakia Sh252.975bilioni katika kifungu hicho lakini kuna bilioni 100
zimetumika visivyo,” alisema Zitto, ambaye pia ni Mbunge huyo wa Kigoma
Kaskazini (Chadema).
Alisema katika majumuisho ya Bajeti ya wizara
hiyo, Dk Magufuli na Dk Mwakyembe wakati huo akiwa Naibu Waziri wa
Ujenzi na Lukuvi walitoa maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu fedha.
Alikariri maneno yaliyorekodiwa kwenye Hansard ya Bunge yaliyosemwa na viongozi hao watatu.
“Tunaomba fedha Sh252 bilioni kwa ajili ya kuanzia
kazi za ujenzi wa barabara,” Zitto alisema akikariri maneno ya Dk
Magufuli wakati anawasilisha bajeti.
“Fedha hizi zitachangia miradi ya wafadhili,” haya yalikuwa maneno ya Dk Mwakyembe wakati akifanya majumuisho.
“Hizi ni fedha kwa ajili ya counterpart fund,” alimkariri Lukuvi wakati akichangia hotuba ya wizara hiyo.
Zitto alisema CAG alihoji mwaka huu kuhusu
matumizi ya fedha hizo na alitoa taarifa akidai kuwa fedha hizo zilikuwa
miradi hewa na kasma kivuli.
Zitto alisema kuwa Dk Magufuli na Katibu Mkuu wake walipohojiwa walidai kutumia fedha hizo kulipa madeni.
“Kwa nini mlidanganya Bunge? Mliomba fedha za
kuanza miradi maalumu. Hamkuomba fedha za madeni. Kwa nini mliunda kasma
kivuli na kuifuta baada ya pesa kulipwa?” Zitto alimhoji Balozi Mrango.
Mwanacni news paper
Katika majibu yake, Balozi Mrango alisema kwa nia njema, fedha
hizo zilitumika kuwalipa makandarasi waliokuwa wamechachamaa, huku
baadhi yao wakisisitiza kusitisha kuendelea na miradi. Hivyo
wakalazimika kuomba fedha kwa njia hiyo ili miradi kuendelea katika
maeneo mbalimbali ya nchi.
Zitto hakuridhishwa na majibu hayo akisema
hapakuwa na haja ya kutumia fedha hizo kuwalipa makandarasi wakati
kulikuwa na kasma yao ya awali. Alisema kama kulikuwa na haja hiyo,
wizara isingeita mradi rasmi.
“Jambo hili siyo sahihi hata kidogo kulidanganya
Bunge na hadi sasa wewe na waziri wako hamuonyeshi kukubali kosa hili,
hata Waziri Lukuvi naye alisisitiza bungeni kwamba fedha hizo zinaombwa
ili kutekeleza mradi maalumu lakini sasa imebainika sivyo, kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge tutawafikisha kwenye Kamati ya Maadili ili wahojiwe nao
wajieleze kwa kulidanganya,” alisema Zitto.
Pia kamati hiyo imeitaka wizara hiyo kutoa
ufafanuzi wa kina kuhusu matumizi ya Sh100 bilioni zilizotumika kinyume
na maombi yaliyowasilishwa kwenye Bajeti ya mwaka huo wa fedha.
CAG ameshauri madeni yote ambayo Wizara ya Ujenzi
inadaiwa yaorodheshwe ili yawe wazi kuepuka migongano katika matumizi ya
fedha.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Lukuvi alisema
haelewi chochote na kusisitiza kuwa akipata taarifa rasmi za Kamati ya
PAC, atatoa ufafanuzi.
Halmashauri zinavyotafuna mabilioni
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAACc), imeeleza namna mamilioni ya fedha za Serikali
zinavyoibwa kutoka Hazina kupitia halmashauri za wilaya huku Ilala
ikitajwa kuongoza kwa ufisadi huo.
Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk Mohammed
aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Hazina imekuwa ikipeleka
fedha kwenye halmashauri zikiwa zimezidi na kwamba kiasi kinachozidi
hakirudishwi badala yake huliwa.
Alisema kamati hiyo imefanya uchunguzi kwenye
halmashauri 43 na kubaini kwamba mtindo huo ndiyo unaotumika kuiba fedha
za Serikali.
“Mwaka 2011/12 kiasi cha Sh1.5 bilioni zilipelekwa
zikiwa zimezidi kwenye halmashauri hizo lakini hazikurudishwa Hazina
kama inavyoonyesha kwenye ripoti ya CAG.
Alisema kati ya kiasi hicho, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala
ilipewa ziada ya Sh213 milioni ikifuatiwa na Geita iliyopewa Sh129
milioni.
“Fedha hizo za mishahara zilipelekwa kwenye
halmashauri hizo na Hazina kimakosa zikiwa zimezidi lakini watendaji wa
hawakuzirudisha kama wanavyotakiwa kisheria badala yake zikayeyuka,”
alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa uchunguzi huo pia
ulibaini kwamba katika halmashauri hizo 43 kiasi cha Sh693 milioni
hulipwa mishahara hewa ambayo wafanyakazi wake walishakufa na wengine
kustaafu.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ililipa
mishahara hewa yenye thamani ya Sh79.4 milioni ikifuatiwa na Ukerewe
iliyolipa Sh57.5 milioni.
Kwa upande wa fedha za miradi ya maendeleo, mwaka
2011/12, Hazina ilipeleka katika Halmashauri ya Mbarali, Mbeya Sh724
milioni kwa ajili ya Mradi wa Maendeleo ya Elimu Sekondari wakati mradi
huo ulikuwa ukihitaji Sh70 milioni tu.
“Kiasi cha Sh654 milioni zilipelekwa kimakosa na
Hazina lakini badala ya kurudishwa zilitumiwa katika mazingira ya
kutatanisha,” alisema.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe
ilipelekewa ziada ya Sh500 milioni na Mvomero ilipewa Sh85 milioni.
“Kuna mtandao mkubwa wa Hazina na halmashauri ambao ukiachwa utaendelea
kupoteza fedha nyingi za walipakodi,” alisemaMwanacni news paper