Tuesday 1 October 2013

Kampuni ya kimataifa ya kuhamisha pesa kuwekeza nchini Tanzania


29th September 2013
Kampuni ya kimataifa ya kuhamisha pesa kwa njia ya mtandao, 'Times of Money' ya India, inatarajiwa kuwekeza huduma hiyo nchini Tanzania kama sehemu ya mpango wake wa kujipanua Barani Afrika.


Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kampuni ya Times of Money, imesema iko katika hatua za awali za kuleta nchini mageuzi ya utumaji pesa kwa njia ya mtandao kutoka nje ya nchi.
“Mfumo huu utawawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kupata au kutuma fedha kutoka sehemu yoyote duniani na kuingia moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki, kadi za malipo ya kabla (pre-paid cards),” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa Times of Money, Avijit Nanda.

Aidha, Nanda alisema kupitia mfumo huo, Watanzania watakaotumia huduma hiyo wanaweza moja kwa moja kupokea pesa zitakazotumwa kwao kutoka nje ya nchi moja kwa moja kwenye simu zao za mkononi.

Katika kuimarisha huduma hiyo, kampuni hiyo, hivi karibuni tumeingia mkataba na Benki ya Diamond Trust nchini Kenya kutoa huduma kwa wateja wake wa mfumo unaojulikana kama ‘NationHela’.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Tanzania idadi ya Watanzania wanaoishi na kufanya kazi nchi sehemu mbalimbali duniani milioni mbili, huku ripoti ya Benki ya Dunia, inakadiriwa kuwa Watanzania hao waliingiza nchini kiasi cha Sh.120 bilioni mwaka jana.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI