Posted Alhamisi,Agosti22 2013 saa 20:51 PM
Kwa ufupi
- Lakini lalamiko kubwa zaidi la nchi hizo ni kwamba Serikali ya Tanzania haieleweki wala kuaminika pale yanapokuja masuala ya kibiashara na mengine mengi yanayohitaji uamuzi wa haraka.
Habari kwamba Rwanda na Uganda zimeamua kujitoa
kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia mwezi ujao ni za kusikitisha
kama ambavyo ni za kushtua. Chama cha Wasafirishaji wa Mafuta (Tatoa),
kilitangaza juzi baada ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge
inayosimamia Bajeti kwamba nchi hizo zinajitoa kutokana na matatizo sugu
mbalimbali ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakilalamikiwa lakini
Serikali ikaamua kutia pamba masikioni badala ya kuyatatua.
Hivyo, tunaposema uamuzi wa nchi hizo mbili ni wa
kushtua hatumaanishi hatua hiyo imekuja kwa kushtukiza. Hii ni kutokana
na ukweli usiopingika kuwa, nchi hizo pamoja na nchi nyingine jirani,
zikiwamo Zambia na DRC, kwa muda mrefu zimekuwa zikilalamikia hasara na
kadhia wanazozipata kwa kutumia Bandari hiyo. Sababu zinazotolewa ni
pamoja na wizi wa mizigo, yakiwamo makontena na vifaa vya magari kama
vile redio; uchakachuaji wa mafuta; urasimu na ucheleweshaji wa mizigo
kutoka bandarini; ukubwa wa ushuru wa forodha na barabara; na ugumu wa
kufika na kutoka bandarini kutokana na misururu ya magari.
Lakini lalamiko kubwa zaidi la nchi hizo ni kwamba
Serikali ya Tanzania haieleweki wala kuaminika pale yanapokuja masuala
ya kibiashara na mengine mengi yanayohitaji uamuzi wa haraka.
Tumedokezwa kwamba kutoeleweka na kutoaminika kwa Serikali ya Tanzania
kunatokana na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na ugeugeu na undumila kuwili
kwa kutenda kinyume na makubaliano yaliyofikiwa na wakati mwingine
kusema ‘ndiyo’ wakati ikiwa na maana ya kusema ‘hapana’. Hilo ni
lalamiko mtambuka ambalo pia linazungumziwa miongoni mwa nchi wanachama
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Pamoja na ukweli kwamba uamuzi wa Rwanda na Uganda
ulitazamiwa na wengi kutokana na Tanzania kutoshughulikia malalamiko ya
nchi hizo kwa muda mrefu, sisi tunadhani uamuzi huo umelishtua taifa
kiuchumi. Kitendo cha mataifa hayo kuamua kutumia Bandari mbadala ya
Mombasa ni pigo kubwa kwa Tanzania kiuchumi, kwani pengo lake katika
pato la taifa halitaweza kuzibwa kirahisi katika miaka mingi ijayo.
Pamoja na vitendo vya ufisadi na wizi wa mabilioni
ya fedha uliopo katika Bandari hiyo, Ripoti ya Benki ya Dunia (WB),
inasema bado Bandari hiyo inaweza kuinua uchumi wa Tanzania na nchi
jirani kwa asilimia kubwa iwapo zitachukuliwa hatua za kuleta ufanisi
katika Bandari hiyo. Hivi sasa bado meli zinatia nanga kwa muda mrefu
zikisubiri kupakuliwa mizigo na hali ni hiyohiyo kwa mchakato wa
kuiondoa bandarini.
Tunachotaka kusema hapa ni kwamba asitafutwe
mchawi asilani, kwani mchawi ni sisi wenyewe tuliozilazimisha Rwanda na
Uganda kutumia Bandari ya Mombasa kutokana na uzembe na udhaifu wa
Serikali yetu. Tayari kuna madai yasiyo na mashiko kwamba hizo ni hujuma
za Rwanda dhidi ya Tanzania eti kutokana na hali ya ‘kutoelewana’ kati
ya marais Jakaya Kikwete na Paul Kagame.
Hatua hiyo ya Rwanda na Uganda bila shaka
itaisukuma Serikali ya Tanzania kusoma maandishi ukutani na alama za
nyakati, kwamba isipopiga vita wizi na ufisadi na kuleta ufanisi
bandarini, Zambia na DRC pia zitaondoka kama ilivyofanya Msumbiji na
sasa Uganda na Rwanda. Tayari Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
ameanza kuchukua hatua stahiki. Tunarudia kuishauri Serikali imuunge
mkono.
chanzo: Mwananchi
chanzo: Mwananchi