Kwa ufupi
Lengo ni kuwa na idadi inayolingana na hali halisi ya ufanisi, yafanya mkutano na wafanyakazi kufafanua hilo
Dar es Salaam. Kampuni ya Ndege ya Fast Jet
inatarajia kupunguza wafanyakazi wake ili kuimarisha utendaji wa kazi
kwa gharama nafuu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Meneja
Mkuu wa Fast Jet, Lee Foster alisema kuwa katika kutekeleza mpango huo,
wafanyakazi wameandaliwa mkutano maalumu ili kujadiliana namna ya
kuboresha upunguzaji wa wafanyakazi wake.
Katika mkutano huo wafanyakazi wataambiwa sababu
za kupunguzwa na kupanga namna gani ya kuwafidia wafanyakazi ambao
wataathiriwa na mpango huo.
Alisema hatua hiyo ya kuwapunguza wafanyakazi ni
muhimu kwa kuwa kampuni hiyo inaendesha shughuli zake kwa gharama kubwa
huku bei ya tiketi zake ikiwa ni ndogo.
“ Najua ili kuboresha huduma kwa Watanzania wengi
na kwa bei nafuu inatakiwa pia kuhakikisha kuwa tunapunguza matumizi
ambayo sio muhimu, ikiwamo kupunguza wafanyakazi,” alisema Lee Foster.
Alisema kuwa tangu kuanza kutoa huduma hapa nchini Fast Jet imekuwa ikiongeza huduma zake kwa kuanzisha safari nyingi mikoani.
Alisema kuwa Fast Jet imeuza tiketi zaidi ya
40,000 kwa bei ya chini ya Sh32,000 huku utafiti ukionyesha kuwa kuna
asilimia 38 ya wateja wake hawakuwahi kutumia usafiri wa ndege.
Alisema kwa sasa tayari kuna wafanyakazi tisa
katika Matawi ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam ambao walikuwa kwenye
vitengo vya mauzo na utendaji.
Akizungumzia matarajio ya safari za kampuni hiyo
ya kutokea Dar es Salaam kuelekea jijini Johannesburg alisema itaanza
Septemba 27 mwaka huu.
Alisema kuwa kutakuwa na safari kwa siku za
Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kwa wiki huku kukiwa na matarajio ya
kuongezeka kwa safari kulingana na ongezeko la uhitaji.
Alisema kama mafanikio yatapatikana, Fast Jet
itaanza safari za Zambia, Kenya na Rwanda kwa kuwa kampuni hiyo inalenga
kuwa kampuni ya kwanza kutoa huduma kwa bei nafuu huku ikiwawezesha
Watanzania kwenda nchi waitakayo kwa gharama nafuu zaidi.
Aliwashukuru wateja wote.