Saturday, 2 November 2013

Kiwango cha ufaulu Waziri, Katibu Mkuu wajichanganya

2nd November 2013

Dk. Shukuru Kawambwa
Siku  moja tu baada ya serikali kupangua madaraja ya ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha Sita, kumeibuka kauli za kutofautiana kati ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Katibu wake kuhusu kiwango cha ufaulu kilichopangwa.

Juzi Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, akizungumza na waandishi wa habari alitangaza mfumo mpya wa usahihishaji wa mitihani kwa kushusha alama za ufaulu.

Alisema kuwa uamuzi huo umetokana na maoni ya wadau wa elimu kuhusu upangaji wa viwango vya alama katika mitihani kwa kidato cha nne na cha sita ambao utazingatia matumizi ya alama za tathimini ya mwanafunzi (CA) na kuamua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Katika taarifa hiyo alisema daraja sifuri linafutwa na kuwekwa daraja litakalojulikana kama daraja la tano ambalo litakuwa la mwisho katika ufaulu.

NIPASHE ilipozungumza na Dk. Shukuru Kawambwa kupata ufafanuzi kuhusu kuondolewa kwa daraja sifuri, alisema kuwa serikali haijapangua madaraja ya ufaulu bali kilichobadilishwa ni alama ya ufaulu.

Alisema daraja sifuri lipo pale pale halijafutwa na kumtaka Katibu aichapishe upya taarifa hiyo na kuisambaza katika vyombo vya habari ili kutoa ufafanuzi.

Dk. Kawambwa alisema kilichoongezwa  ni alama za ufaulu ambapo  zamani ilikuwa ni alama A, B, C, D na F.

Alisema katika muundo wa sasa kilichoongezwa ni alama mbili yaani B+ na E ambapo katika mfumo wa sasa kutakuwa na alama  A, B+, B, C, D, E na F.
Dk. Kawambwa alisema muundo huo ndiyo wenye manufaa na utasaidia kupambanua vizuri matokeo ya wanafunzi.

Licha wa Waziri kukanusha  kufuta daraja sifuri, NIPASHE ilitembelea tovuti ya elimu na kuikuta taarifa hiyo ikisomeka:  "Kwa mantiki hii, Daraja Sifuri linafutwa na kuwekwa daraja litakalojulikana kama Daraja la Tano na ambalo litakuwa ndilo la mwisho kabisa katika ufaulu"

Dk Kawambwa katika maelezo yake alisema mkakati wa mabadiliko hayo ni kuleta tija katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRB).

MAONI YA WADAU
Mkuu wa Kitivo cha Elimu wa Shule ya Ualimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo alisema serikali inachotaka ni kukwepa neno kufeli kwa kutaka kuweka mbadala wa kiwango cha ufaulu dhaifu.

Alisema kitaaluma suala hilo halipo, "sisi itakuwa ni wa kwanza kutokuwa na kiwango cha kufeli unajua kitaaluma lazima pawapo na wanafunzi waliofaulu na waliofeli katika mitihani."

Dk. Mkumbo alisema serikali inataka kufikia BRN bila kufanya kazi kubwa ambayo haitakuwa na maana.
Alisema serikali inalenga kupandisha kiwango cha ufaulu kufikia asilimia 60 ndani ya miezi miwili tangu kuanzishwa kwa BRN jambo ambalo lilitakiwa kufanyiwa kazi kwa muda.

Aidha, alisema serikali ilitakiwa ijipange na siyo chini ya mwaka mmoja na kufanya kazi kubwa juu ya suala hilo ili kuweza kufikia BRN.

Dk. Mkumbo alisema Tanzania haijawahi kuwa na tatizo la viwango vya ufaulu ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika "Ina maana Tanzania viwango vyetu bado vipo chini vya ufaulu hivyo hapa hatusolve tatizo,"

Kwa upande wake, Meneja wa Habari na Ushauri wa HakiElimu, Nyanda Shuli, taasisi yake imeunda kikundi kazi kwa ajili ya kujadili suala hilo.
Alisema suala hilo ni zito na kwamba tangu waanze kazi hawajawahi kukutana na jambo zito kama hilo.

Shuli alisema wamejifungia siku nzima ili waweze kuja na maoni yenye tija ili kutoa ushauri utakaoweza kufanyiwa kazi.

Mkufunzi wa Walimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Frank Tilya, alisema chuo hicho kinaanda utaratibu wa kutunga mitihani kwa watakaochaguliwa kujiunga na elimu ya juu ili kuepusha rundo la wasomi uchwara nchini.

Dk.Tilya amesema serikali imefanya mabadiliko hayo ili kuondoa aibu ya kimataifa, kwa kuficha ukweli kuwa wanafunzi wengi wanafeli mitihani yao kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu,  kwa utaratibu huu wa sasa kwa kutumia mfumo mpya wa usahihishaji.

“Utaratibu uliotumika haukufuata sheria za elimu ili kuwa na wasomi wanaokubalika kimataifa lazima vyuo vikuu vitunge mitihani yao ili kupata cream,”  alisema.

Aliongeza kuwa kwa utaratibu huo wanafunzi wengi watakuwa na vyeti vyenye ufaulu mzuri lakini wale waliofeli watajulikana kutokana na alama zao,  hawawezi kwenda elimu ya juu kwa maksi za chini pia hawawezi kupata kazi.

Alifafanua kuwa kubadili mfumo wa usahihishaji ni jambo la mwisho liliotakiwa kuwa na mtaala wa elimu unaoeleweka hata kwa walimu wanaoutumia kufundishia, kuondoa utitiri wa vitabu vya kiada na kuwa na kitabu kimoja kitakachofundisha shule zote nchini na lugha ya ufundishaji iwe moja, baraza liwe na utaratibu wakufuatilia matokeo ya wanafunzi mashuleni mwao kila mwaka.

Alisema serikali inatakiwa kuwajali walimu ikiwa ni pamoja na kuangalia upya vyuo vinavyotoa elimu kwa walimu.

" Je vinakidhi haja? Je walimu wanakielewa kile wanachofundisha, ikiwa ni pamoja na kuwalipa mishahara yao kwa wakati kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu," alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa  Mchome, alitangaza mfumo huo kuwa daraja la kwanza  litaanzia pointi 7 hadi 17 kama ilivyokuwa muundo wa zamani, daraja la pili litaanza na pointi 18 hadi 24 badala ya pointi 18 hadi 21 kama ilivyokuwa zamani na likiwa ni kundi la ufaulu mzuri, daraja la tatu litaanza na pointi 25 hadi 31 hili ni ufaulu wa wastani, daraja la nne ni 32 hadi 47 wakati daraja la tano ni pointi 48 hadi 49 na kundi la mwisho ni pointi 3 hadi 35 ambalo  ni kundi la ufaulu hafifu ambalo zamani lilijulikana kama sifuri.
 
CHANZO: NIPASHE