Wednesday, 6 April 2011

Mkutano Mkuu wa TASAO na Uchaguzi wa Viongozi Wapya




Tarehe 1 Aprili, 2011 wanajumiya ya TASAO walifanya mkutano mkuu kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yahusuyo jumuiya hiyo pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wapya. Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa wana-TASAO walioweza kuhudhuria mkutano huo. Licha ya kuwa na shauku ya kuonana kama kikundi cha Watanzania baada ya miezi kadhaa, ilikuwa ni nafasi nzuri kwao kushirikishana juu ya mambo mbalimbali yanayojiri hapa Norway na hata kule nyumbani Tanzania, huku wakijipatia vinywaji baridi na vitafunwa. Suala la babu wa Loliondo anayegawa 'vikombe' vya tiba ya magonjwa mbalimbali lilivuta hisia za wajumbe, hasa wale waliofika dakika za mwanzoni, huku baadhi yao wakionesha wasiwasi juu ya uwezo wa tiba hiyo.

Baada ya kujadili agenda mbalimbali juu ya mafanikio na changamoto zinazoikabili TASAO, wajumbe wa mkutano walichagua viongozi wapya kwa ajili ya kukiongoza chama kwa kipindi cha mwaka 2011/2012. Yafuatayo ni majina ya viongozi wateule na vyeo vyao kwenye mabano: Ndg. Doreen Ndossi (Mwenyekiti), Ndg. Andrew Munisi (M/Mwenyekiti), Ndg. Janeth Mwakalinga (Katibu), Ndg. Michael Pima (Mhazini), Ndg. Ellance Mbilu (blog moderator).

Mwenyekiti mteule wa tume ya muda ya uchaguzi, Mch. Syprian Hilinti, aliwatangaza rasmi viongozi hao wapya na kuwataka wanachama wawape ushirikiano.