Na Daniel Mjema,Mwananchi
Posted Ijumaa,Novemba1 2013 saa 24:0 AM
Posted Ijumaa,Novemba1 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Wadaiwa kuwa wamesharejesha Sh80 milioni baada ya kubanwa na makachero wa polisi.
Moshi. Askari polisi wawili wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kula
njama na kushiriki katika uporaji wa Sh220 milioni za Kampuni ya Dot
Services ya mjini Moshi.
Habari za uhakika zilisema baada ya kubanwa na
makachero, askari hao walirejesha Sh60 milioni na watuhumiwa wengine
wawili ambao ni raia, walirejesha Sh23 milioni. Askari hao ni wale
walioko katika Kikosi cha Polisi wa doria wanaotumia pikipiki na jana
watuhumiwa wote walitawanywa katika vituo mbalimbali ili wahojiwe kwa
nyakati tofauti tofauti.
Habari za kipolisi zilisema askari hao hawakwenda
eneo la tukio lakini walifahamu mpango mzima kuhusu uporaji huo
uliowawezesha kupata mgawo wa fedha hizo.
Waliotiwa mbaroni wana vyeo vya Constable (majina
tunayo) na inaelezwa kuwa tukio hilo limewachukiza baadhi ya polisi
wakidai ni kuwa mfululizo wa matukio yanayochafua sura ya jeshi hilo.
Habari hizo zimebainisha kuwa tukio hilo ni mpango
mahususi uliowashirikisha watu wasiopungua 10 wakiwamo baadhi ya
watumishi wa Kampuni ya Dot Services waliovujisha mpango wa kuhamisha
fedha hizo.
Kulingana na vyanzo vya habari, idadi ya
walioshiriki katika mpango wa kupora fedha hizo ni kati ya watu wanane
na 10 na tayari polisi wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz
alikaririwa akisema kuwa fedha hizo ziliporwa Jumanne asubuhi katika
makutano ya Barabara za Arusha na Boma mjini Moshi.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, baada ya kufika katika
makutano hayo, wafanyakazi wa Kampuni ya Dot Services waliokuwa na gari
aina ya Toyota Hilux T.864 AZM walisimama kuruhusu pikipiki ipite.
Kamanda Boaz alisema wakati wakisubiri pikipiki
ipite, ghafla walijitokeza watu wawili wakafungua milango na kuingia
ndani ya gari na kuwateka wafanyakazi na kuwaamuru waelekee eneo la
Shanty Town.
Hata hivyo mkurugenzi wa Fedha wa kampuni hiyo ya
ujenzi yenye makao yake makuu nchini Uganda, Shuresh Bab alifanikiwa
kuruka kwenye gari hilo na kutoa taarifa polisi.
Kamanda Boaz alifafanua kuwa msako wa kuwatafuta
wahusika ulianza mara moja ambapo polisi walifanikiwa kulipata gari hilo
na wafanyakazi wakiwa wametelekezwa mto Karanga mjini Moshi.
SOURCE: MWANANCHI