Monday, 22 July 2013

Tozo za simu sasa kuangaliwa upya

Na Ibrahim Yamola, Mwananchi  (email the author)
Posted  Julai20  2013  saa 22:30 PM
Kwa ufupi
Ni zile za laini ya simu zilizopitishwa na Bunge kama moja ya vyanzo vya kodi nchini na kupingwa na wengi.

Dar es Salaam. Serikali imekubali kupitia mawazo na maoni yaliyotolewa na Umoja wa Wamiliki wa Kampuni za Simu Nchini (MOAT), kuhusu kufutwa kwa tozo ya kodi ya laini za simu ‘Simcard tax’ ya Sh1000 kutokana na kulalamikiwa na wadau wa sekta ya mawasiliano.
Hali hiyo inatokana na kauli za viongozi wa Serikali, wabunge na wananchi wanaopinga tozo hiyo kwa kile wanachokieleza kitaongeza mzigo wa ugumu wa maisha kwa mtumiaji hususan wa kipato cha chini.
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa akizungumza na wandishi wa habari jana alisema, wamekutana na MOAT na kupokea mapendekezo yao na sasa wanayafanyika kazi.
“Tumeendelea kusikia malalamiko kutoka pande mbalimbali na juzi, tulikutana na MOAT na tumejadiliana na wametoa mapendekezo mazuri tu kipi kifanyike ili tupunguze makali ya kodi hii hususan kwa wananchi wa hali ya chini,” alisema Dk Mgimwa na kuongeza:
“Katika suala hili, jazba zisiwepo kwani ni suala la kisheria kutokana na kupitishwa bungeni hivyo ili kuondolewa ni lazima kufuata mkondo na tunatizama mapendekezo ya jinsi ya kulishughulikia.”
Dk Mgimwa aliendelea kusema “Hakuna mtu anayelenga kumkamua mwananchi,lakini hili lilitokana na mapendekezo 67 yaliyotolewa na Kamati ya Bajeti kuwa chanzo cha mapato kinachotekelezeka lakini kama inaonekana kuwa kikwazo tutangalia jinsi ya kukabiliana nalo.”
Waziri huyo alisema lengo la tozo hiyo ilikuwa kupata fedha zitakazoelekezwa katika miradi ya maji, barabara na umeme hususani vijijini kunakokabiliwa na changamoto mbalimbali muhimu za maendeleo.
Alisema mpaka sasa hakuna mtumiaji wa huduma hiyo ambaye ameanza kukatwa tozo hiyo kutokana na mchakato huo kuwa bado unaendelea katika utekelezaji wake.
Naye Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema, Serikali itahakikisha mwananchi hapati mzigo usiokuwa na sababu.
“Serikali ni sikivu na inawasikiliza wananchi wake hivyo kupitia mawazo na mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa yanafanyiwa kazi ili kutokuathiri pande zozote,” alisema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa alisema, uwekezaji hususani vijini umekuwa ukikabiliwa na changamoto za miundombinu ya barabara, umeme na maji vitu ambavyo vikiboreshwa vitawavutia wawekezaji wengi.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba Juzi alisema, wizara hiyo ilipinga tangu awali mpango huo kabla ya kupitishwa na kuwa sheria na kwamba anaamini itaondolewa.
 Nacho chama tawala, CCM,Chadema walikaririwa na vyombo vya habari wakiitaka Serikali kuangalia vyanzo vingine vya mapato badala ya tozo hiyo

source: Mwananchi news paper