Thursday 23 May 2013

Askari-watuhumiwa-kubaka-kumwua-mjamzito-kupora-kuchoma-nyumba-moto

Picture
Askari wakiwa lindoni/doriani, Mtwara
Hali ya usalama katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani hapa imezidi kuwa mbaya baada ya askari polisi kudaiwa kufanya unyama kwa kuwabaka wanawake na kumpiga risasi mjamzito

Mbali na unyama huo polisi pia wanadaiwa kuchoma moto nyumba tatu za wananchi katika mtaa wa Magomeni na vibanda vya maduka kadhaa na kupora vitu vilivyomo ndani.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa anasema hali ni shwari na kwamba wananchi watoke nje kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni, zinazoaminika kuwa za risasi na hivyo kufanya idadi ya maiti zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia mbili na majeruhi 18: “Ni kweli kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa
miezi saba, amepigwa risasi tumboni...” “...pia tumepokea mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Chuno, amevunjwa miguu yote kwa risasi.”

Habari zinadai kuwa mjamzito huyo ameuawa akiwa nyumbani kwake baada ya polisi kuvamia makazi yake.

Huduma za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyo wazi, hakuna usafiri wa daladala wala pikipiki, mji upo kimya, sauti za milio ya mabomu na bunduki zimetawala, wanajeshi waliovalia sare wameuzingira mji wakiwa katika magari na pikipiki.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari kwa nyakati tofauti wakazi hao wamelalamikia kitendo cha askari wa jeshi la polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga, kuwabaka na kuwapora mali zao:

“Magomeni A hatuna amani askari wanaingia majumbani mwetu wanatupiga na kutunyang’anya simu, yani huku Magomeni hatuna amani kabisa, tumepoteza watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi” alisema Paulina Idd na kuongeza: “Majumba yetu yamechomwa moto wanaofanya fujo ni polisi wenyewe halafu wanakuja wanatubaka na kuiba mali zetu halafu tunateseka sisi yaani tumechoka kabisa na serikali yenyewe,” alisema Paulina.
Picture
Wanawake na watoto wakiwa hospitali ya rufaa ya Ligula, Mtwara kwa ajili ya kuomba hifadhi baada ya kuyakimbia makazi yao kwa hofu
Kamanda Sinzumwa alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa atapingana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Mchimbi aliyewasili Mtwara leo: “Kuhusiana na suala hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani nitapingana na Waziri wangu kwani leo ametoa tamko bungeni na leo atawasili,” alieleza Sinzumwa

Wakazi wakimbia maeneo yao
Wakazi wa maeneo mbalimbali wamekimbia makazi yao hususani wanawake na watoto na kuhamia hospitali ya rufaa kwa kuhofia usalama wao huku wengi wao wakipotezana na ndugu zao.

Hali hiyo imetokea kufuatia kuwepo kwa milipuko ya mobomu katika maeneo mbalimbali mjini hapa huku huduma za kijamii zikiwa bado zimesitishwa. Hali hiyo imetokea baada ya kusambazwa kwa vipeperushi vilivyokuwa vikihamasisha wananchi wa mkoani hapa kusitisha huduma zote hapo jana  ili kusikiliza hotuba ya wizara ya nishati na madini.

Kufuatia hali hiyo imesababisha kifo kwa raia mmoja aliyefahamika kwa jina Karim Shaibu (22) mkazi wa Chikongola ambaye alipigwa risasi wakati wa fujo kati ya jeshi la polisi na wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari mganga mkuu wa mkoa hospitali ya rufaa ya Ligula Dk Sadun Kabuma alithibitisha kupokea kwa kifo hicho ikiwa ni pamoja na majeruhi 17 wakiwemo askari watatu: “Ni kweli jana kuanzia majira ya saa 10 hadi saa 11 nilipokea majeruhi 17 ambapo kati ya hao wamishtuko ni wanawake watano na askari watatu na kijana mwingine ambaye alikuwa na jeraha na katika harakati zan kumwokoa maisha yake alifariki akiwa chumba cha upasuaji,” alisema Dk Kabuma

Wananchi wazungumzia bajeti

Wakizungumzia uwasilishwaji wa hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini wakazi wa hapa wamesema kuwa hawakubaliani na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwani mpango huo utawaletea dhuluma: “Mpango wa kusafirishwa kwa gesi asilia hatuna mpango nao kwa wakazi wote wa Mtwara kwa kifupi akina mama wa mtwara hatutaki itoke,” alisema Fatuma Abdallah.

---
Imenukuliwa kutoka wavuti.com kwa msaada wa KARIBU KUSINI Blog

Source: http://www.wavuti.com/4/post/2013/05/mtwara-askari-watuhumiwa-kubaka-kumwua-mjamzito-kupora-kuchoma-nyumba-moto.html#ixzz2U8mSnwWA