AKIWA na lundo la chupa tupu za maji ya kunywa zilizokwishatumika, za kampuni tofauti, kijana Mohamed (si jina lake halisi), anapita mtaa hadi mwingine akiokota chupa tupu hizo na kuziweka katika kiroba.
Na akifanya hivyo, hasemi na mtu yeyote, macho yake wakati wote yanaangaza kuona ni wapi atapata anachokitafuta na kwenda kuziuza. Ni kazi ngumu, lakini anayoifanya kwa jitihada kubwa ingawa hali yake haibainishi hasa ni kipi anachopata katika biashara hiyo.
Mohamed ni mmoja wa makumi ya wengine wakiwamo kinamama, ambao kila siku wapo mitaaani wakikusanya chupa tupu za maji kwa ajili ya kwenda kuziuza kwa wafanyabiashara wa jumla, ambao nao wanaziuza katika viwanda zinakoyeyushwa na kutengenezwa bidhaa nyingine za plastiki.
Biashara hiyo iliyoshika kasi hivi karibuni, hususan jijini Dar es Salaam, wakati mwingine huleta maswali zaidi kuliko majibu iwapo kweli wanachopata kinalingana na mihangaiko yao hiyo, na kitaweza kubadili hali za maisha yao katika namna ya kupunguza umaskini kulingana na lengo la kwanza la milenia mwaka 2015.
Mwanasaikolojia mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye hapendi jina lake kutajwa gazetini, anasema kuwa kimsingi watu hao wanatafuta riziki lakini ana wasiwasi na aina hiyo ya ujasiriamali ambayo anasema kuwa pengine ingetambuliwa watendaji nao wangebadilika.
Anasema kuwa katika nadharia ya utafutaji ikiwa ni pamoja na kazi ambayo mtu anaifanya huwa ni lazima ifanye mrejesho ambao ni pato kwa mhusika, ambalo litaweza kubadili maisha yake hivyo ana wasiwasi kuwa kuna watu wananufaika kupitia migongo ya waokotaji hao.
“Kuna wakati kazi anayoifanya mtu inaweza kumuathiri na kwamba kuna watu wanaoifanya kazi hiyo wanaoelekea kuathirika pengine kutokana na 'nature' (asili) ya kazi yenyewe," anasema na kuongeza kuwa kazi hiyo ni kama nyingine lakini inatakiwa kuleta mabadiliko kwa watendaji.
Anasema kuwa mtu anaifanya kwa miaka miwili mitatu hali yake haibadiliki na mbaya zaidi anakuwa katika muonekana au mazingira ambayo yanaweza kumuingiza katika hatari ya kupata maradhi mengine basi hiyo haina tija kwake.
Mkazi mwingine wa jijini aliyejitambulisha kwa jina la Shaabani Ngigi, anabainisha kuwa kazi hiyo ina tatizo kutokana ukweli kuwa huhitaji lundo la chupa nyingi kuweza kupata kilo chache.
Anabainisha kuwa kilo moja haizidi sh 400. Anasema kuwa lundo kama hilo mtu si rahisi kulipata kwa siku moja ni lazima afanye kazi ya ziada - si kwa siku zisizopungua mbili hadi tatu akizunguka kote anakoweza kupita kutafuta chupa hizo.
"Fikiria kuna watu wanafamilia na anategemea biashara hiyo ya rejareja ambayo kwa siku kipato chake hakitoshelezi ikilinganishwa na nguvu unazotumia kuzitafuta," anasema na kuongeza kuwa wanaonufaika ni wale wanaoziuza jumla viwandani.
Ngigi anakiri kuwa wanamchango mkubwa katika kusaidia kuweka jiji katika hali ya usafi, lakini kampuni na wanunuzi wa jumla wanatakiwa kuwasaidia ama kwa kuboresha bei au vitu vingine vya namna hiyo, kutokana na ukweli kuwa siku za nyuma mtu ukiokota makopo au vitu vingine vya namna hiyo unaonekana 'mwendawazimu'.
Mfanyabiashara mwingine wa kuokota chupa hizo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mama Sarayu kutoka eneo la Jangwani, Dar es Salaam, anabainisha kuwa biashara hiyo ni kama nyingine, ina ugumu na unafuu wake, ila kikubwa ni kwamba mkate wa kila siku unapatikana.
Anasema kuwa yeye binafsi kila baada ya siku mbili au tatu za utafutaji hujikuta ameambulia sh 2000 zikiwa nyingi pato ambalo anakiri kuwa halifanani na ugumu wa kazi yenyewe. "Ndiyo hivyo tena watu tumejiajiri lakini ukweli ni kuwa ni kazi ngumu inayohitaji uvumilivu," anasema na kuongeza:
"Hata hivyo ninaishi kwa kutegemea biashara hiyo kutokana ukweli kwamba hakuna ajira na kuna wimbi kubwa la wasio na ajira za kueleweka".
Mjasiriamali huyo anabainisha kwamba suala la bei ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo wao, kwa kuwa wanapanga wanunuzi kulingana na hali halisi ya soko na awali anakiri kuwa kazi hiyo ilifanywa zaidi na vijana ambao ama walikuwa wakionekana walevi wa vijiweni au watumiaji wa mihadarati.
"Zamani mateja ndio waliokuwa wakionekana kuzikusanya na kuziuza ili wapate pesa za kufanyia mambo yao, lakini sasa ni tofauti, wote tunatafuta ili kukidhi shida tulizonazo," anasema.
Mnunuzi wa jumla wa chupa hizo eneo la Temeke Chang'ombe, Ibrahim Nsaa, anasema uokotaji wa chupa tupu si wendawazimu, bali ni ajira kutokana na hali halisi ya maisha ilivyo hivi sasa.
Anasema kuwa yeye anayenunua kilo moja kwa sh 200 hadi 300, kwa wiki bila kutaja kiwango cha bei zake katika soko la jumla, anaeleza kuwa kuna watu ambao maisha yao yamebadilishwa na biashara hiyo.
Nsaa anabainisha kuwa kuna vijana na watu wengine ambao ni watumiaji wa mihadarati, ambao wamejitumbukiza katika biashara hiyo ili kupata pesa kwa ajili ya uraibu wao, ndio wanaoitia dosari biashara hiyo na kuifanya ionekane ya watu ambao wana matatizo ya akili.
"Zamani ilikuwa kuokota makopo ni wendawazimu lakini sasa ni tofauti - ni ajira," anasema na kwamba kimsingi ni mtu mwenyewe na malengo yake aliyojiwekea. Anasema kimsingi hakuna kazi mbaya, ila ni vile wewe mwenyewe utakavyojiweka na jinsi utakavyoifanya kulingana malengo yako.
Anasema kuwa kuna watu ni wajasiriamali wa jumla wa chupa hizo, lakini awali walianza kwa kuokota moja moja mitaani. Biashara hiyo imeonekana kuwa ngumu zaidi pale muhusika anapojikuta anatumika siku nzima huku na kujikuta anaambulia mfuko mmoja, ambao haufiki hata kila moja, hivyo kumfanya ajitume kwa wiki nzima kuhangaikia angalau apate kilo mbili.
Kuna wengine wanasema kwamba wanapata unafuu kidogo pale wanapoziponda, kwani huongeza angalau uzito kidogo lakini bila hivyo kilo tatu hujaza pick-up ambayo hupata pengine shilingi 1200 au chini ya hapo.
Kwa wastani biashara inayofanywa na wajasiriamali hao bila kujali anapata kilo ngapi kwa siku, ukweli unabaki kwamba ni ngumu na inahitaji kupewa thamani hasa kwa wanaonunua bidhaa hizo angalau kwa kuongeza kiwango cha malipo wanayonunulia, kwani kimsingi chupa hizo zina faida kwa wanaokwenda kuzalisha malighafi nyingine.
Source: Mtanzania Daima, 22.07.2008














