Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Alhamisi,Januari2 2014 saa 8:31 AM
Posted Alhamisi,Januari2 2014 saa 8:31 AM
Kwa ufupi
Ni Dk William Mgimwa, alikuwa akitibiwa Afrika Kusini, Rais Kikwete atuma salamu za rambirambi
Dar es Salaam na Iringa. Waziri
wa Fedha na Mbunge wa Kalenga (CCM), Iringa, William Mgimwa amefariki
dunia jana katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika
Kusini alikokuwa akitibiwa.
Habari zilizopatikana jana kutoka Ubalozi wa
Tanzania nchini Afrika Kusini kupitia kwa Msemaji wake, Habib Awesi
zilisema Waziri Mgimwa amefariki dunia mchana... “Ni kweli amefariki leo
mchana tumepeleka taarifa Ikulu, Dar es Salaam.”
Baadaye jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kusema Waziri
Mgimwa alifariki dunia saa 5:20 kwa saa za Afrika Kusini (saa 6:20).
“Kinachofanyika kwa sasa ni maandalizi ya
kuurudisha nyumbani mwili wa marehemu na hilo linafanywa na Serikali kwa
kushirikiana na familia yake. Taarifa zaidi zitatolewa baadaye kadiri
zitakavyopatikana,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumzia msiba huo, Naibu Spika wa Bunge, Job
Ndugai alisema: “Bunge limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Dk
Mgimwa, alikuwa ni mtu mwaminifu katika kazi zake na alishirikiana
kikamilifu na wabunge katika kutekeleza kazi za Serikali. Taifa
limepoteza mtu makini aliyefanya kazi katika sekta ambayo aliisomea,
jambo ambalo lilimfanya awe na ufahamu mzuri wa mambo katika wizara
(Fedha),” alisema Ndugai.
Kikwete atuma rambirambi
Jana jioni Rais Jakaya Kikwete alitoa taarifa akielezea kushtushwa na kifo cha Waziri Mgimwa.
“Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za
kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa,” ilisema taarifa yake
kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu.
Alisema taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika
kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa
ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na
mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Katika salamu zake kupitia kwa Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda na kwa familia ya marehemu Mgimwa, Rais Kikwete alisema:
“Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia
taarifa za kifo cha Mgimwa.
“Binafsi nilimtembelea mara mbili hospitali
alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika.
Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa
yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.
“Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote
tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu... Natoa
pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana familia wote kwa
kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo
mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni
majonzi yangu,” alisema Rais Kikwete.
Read more: Dr. Mgimwa
Read more: Dr. Mgimwa