Na Kelvin Matandiko, Mwananchi
Posted Januari11 2014 saa 14:16 PM
Posted Januari11 2014 saa 14:16 PM
Kwa ufupi
- Hata hivyo, kumekuwa na tetesi kuwa miongoni mwao wamekuwa wakienda kufanya shoo bure, huku wakiambulia kubadilisha mazingira ya hali ya hewa na kutakasa macho kwa kufika katika nchi hizo zilizoendelea.
Kila kukicha tumekuwa tukisikia taarifa
mbalimbali za wasanii wa Bongo Fleva kusaini mikataba ya kwenda kufanya
shoo katika nchi za Ulaya. Baadhi ya wasanii hao wa Bongo Fleva wamekuwa
wakitangaza shoo hizo pasipo kueleza ukweli wa mikataba wanayoingia.
Hata hivyo, kumekuwa na tetesi kuwa miongoni mwao
wamekuwa wakienda kufanya shoo bure, huku wakiambulia kubadilisha
mazingira ya hali ya hewa na kutakasa macho kwa kufika katika nchi hizo
zilizoendelea.
Mmoja wa wasanii hao ni MB Dog ambaye sasa anakiri
kutokunufaika na ziara hizo, baada ya kuzamia Ujerumani na baadaye
Uingereza kwa miaka mitatu mfululizo kabla ya kurejea nyumbani.
Vyanzo vyetu vya habari vinaonyesha kuwa,
kumekuwepo na mawakala nje ya nchi, ambao wamekuwa wakiwaalika wasanii
hao kwa makubaliano ya kuwalipia nauli tu ya kwenda na kurudi.
Starehe lilimtafuta mmoja wa mawakala kutoka
nchini Uingereza maarufu kwa jina la Steve, ambaye hata hivyo hakuweza
kupatikana kwa simu, lakini likafanya mahojiano na baadhi ya wasanii wa
Bongo Fleva kutaka kujua ukweli kuhusu ziara hizo za nje ya nchi.
Siku chache zilizopita msanii Chege Chigunda
kutoka kundi la Wanaume Family, ambaye alisema kuwa kwake safari hizo
amekuwa akizifanya kwa lengo la kutafuta fursa tu. Anasema kuwa katika
shoo nyingi za nje, wengi wa wasanii wamekuwa wakizifanya bila masilahi
yoyote.
“Unajua siyo kila safari lazima msanii utegemee
masilahi ya kifedha tu, shoo zinatofautiana, zipo zenye masilahi ya
fedha ila kwa hizi za Ulaya ni ‘exposure’ (Fursa) tu,” anasema Chege.
Hali halisi inavyokuwa
Kwa upande wake, Jhikolabwino Manyika maarufu kama
Jhikoman naye ni mmoja kati ya wasanii wachache wanaopata mialiko ya
nje ya nchi na kufanya matamasha nchi mbalimbali duniani kupitia muziki
wa asili na reggae anaoufanya kwa muda wa miaka 12 sasa, anasema kuwa
wasanii hao wamekuwa wakienda Ulaya kufanya shoo, nyingi zikitumia
sebule kuwa ukumbi husika, iwe kwa malipo au bila malipo.
“Wasanii hawa hufanyiwa mipango na mawakala ambao
ni kama madalali wa Ulaya. Msanii mwenye nyimbo yake iliyofanya vizuri
Bongo, basi anaingia mkataba, inaweza kuwa bure bila hata malipo.
Kinachofanyika ni kwamba, atalipiwa nauli ya kwenda na kurudi tu,”
anasema Jhikoman na kuongeza: “Akifika huko, ukumbi atakaofanyia shoo ni
chumba kidogo kitachokuwa kimekusanya Watanzania wachache wanaoishi
huko, akirudi hapa nyumbani tunaambiwa alikwenda Ulaya kufanya shoo.”
Jhikoman anasema kuwa jambo hilo ni fedheha na
aibu kwa wasanii wa Tanzania, akiongeza kwamba tatizo la Bongo Fleva
kukosa mashabiki nchi za Ulaya linatokana na aina ya muziki wanaoufanya.
”Bongo Fleva ni kopi ya muziki wa Ulaya, hivyo
wakifika huko wanaonekana hakuna kitu kipya kwa sababu wanachofanya ni
sawa na wanachokifanya wasanii wao tena kwa ubora zaidi,” anasema
Anaongeza: “Mimi siwalaumu wasanii, ila chanzo ni wadau na
vyombo vya habari ambao wamekuwa wakiwapumbaza na kwafanya waamini
kwamba muziki wao unakua. Ni wachache sana ambao wanajitahidi kwa mbinu
zao kuendelea.”
Kwa upande wake, Mrisho Mpoto anasema kuwa muziki wa Bongo Fleva, unawadanganya wasanii kutokana na presha za vyombo vya habari.
“Mimi naweza kusema kuwa hapa nchini sikubaliki
kama ilivyo kwa nchi za Ulaya, hali hiyo inatokana na kukubalika kwa
kazi zangu. Ni kwa sababu ya tofauti iliyopo kati ya muziki wangu wa
asili na Bongo Fleva,” anasema Mpoto.
Mpoto ambaye ameteka soko na mialiko mbalimbali
kutoka taasisi, wizara, asasi na mashirika anasema kuwa mbaya zaidi ni
kwamba wengi wa wasanii hao hawajajitambua kwa muziki wanaoufanya.
“Wasanii wetu hawa mimi nadhani wamezaliwa kwa
ajili ya kufanya muziki wa aina hiyo, bado hawajatambua wanapaswa
kufanya nini ili kukuza muziki wao,” anasema.
Profesa Jay afafanua
Naye Profesa Jay anaizungumzia hoja hiyo katika
mitazamo miwili tofauti akisema kuwa; kwanza muziki wa nyumbani (Bongo),
bado haujafikia kiwango cha kuwa na shoo kubwa tofauti na zinazofanyika
sasa nje ya nchi. “Bado muziki wetu hatujafikia ‘level’ (kiwango), kama
za P Square, ambao wanaweza kufanya shoo kubwa Ulaya,” anasema Jay na
kuongeza:
“Sababu kubwa inayokwamisha ni pamoja na wasanii
wengi kukosa ubunifu. Unaweza kuwachukua wasanii 10 kwa sasa, wakafanana
kila kitu wanachoimba, yaani wanafanya ‘kucopy’ (kuiga), tu. Kwa jinsi
hiyo, muziki hauwezi kufika mbali.”
Jay anasema kuwa pamoja na udhaifu huo jambo la
pili ni vyombo vya habari kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha katika
kuutangaza muziki wa Bongo Fleva kama inavyofanyika kwa wasanii wengine
wa Nigeria
“Nigeria wanafanyiwa ‘promo’ kubwa na hawana
muziki wa kushangaza lakini; ‘media’ zetu zinapromoti mambo ya ajabu
kabisa, uchafu tu,kwa hivyo hakuna nafasi muhimu kama mchango wa media
kwenye kukuza muziki wetu,” anasema Jay.
Mbali na mazingira hayo Jay anapingana na kauli ya Chege akisema wasanii wanatofautiana thamani zao.
“ Pamoja na kufanya shoo hizo huwezi ukasema wote
tunafanya ili kutafuta ‘exposer’, kwa mfano mimi na Chamilione ni kitu
ambacho hakiwezekani kufanya shoo za bure,” anasema Jay.
Waliogoma kwenda Ulaya
Starehe imezungumza na baadhi ya wasanii ambao
baada ya kubaini shoo za aina hiyo waliamua kutokwenda kabisa hadi pale
masilahi na faida zitakapoanza kuonekana.
Mmoja kati ya wasanii hao ni pamoja na Izzo B
ambaye anasema kuwa kwa upande wake ametambua kuwa shoo za hapa nyumbani
zinamlipa vizuri kuliko malipo na mikataba ya kwenda Ulaya.
“Mapromota wengi wananifuata, lakini siko tayari
kwa sababu sioni tofauti na shoo za hapa nyumbani, nitakuwa tayari
kwenda nje endapo nitapata mikataba mizuri tofauti na hivyo sitakwenda
kamwe,” anasema. Roma Mkatoliki naye anaeleza kuwa wasanii wengi
huchukuliwa na kufanya shoo za bure kwa sababu ya ushamba wa kutembelea
Ulaya.
“ Wengi wanakwenda kucheza shoo bure, wanalipiwa
tiketi ya kwenda na kurudi tu, faida yake ni kutembea na kupata fursa ya
kuona mazingira tofauti,” anasema na kuongeza;
“Siwezi kufanya shoo kama hizo kwa sasa mpaka
nitakapoona kuna faida, yaani ni bora niende Mafinga kwa shoo yangu
itakayonilipa 7 milioni saba kwa mara moja kuliko kwenda kuimbia watu
bila malipo.”
SOURCE: MWANACHI
SOURCE: MWANACHI