Kutoka kushoto ni Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Yoweri Museveni wa
Uganda na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Picha ya Maktaba.
Na Zacharia Osanga, Mwananchi
Posted Alhamisi,Septemba5 2013 saa 12:28 PM
Posted Alhamisi,Septemba5 2013 saa 12:28 PM
Kwa ufupi
Rais Jakaya Kikwete naye ana mipango ya kujenge reli kutokaTanzania Rwanda- Burundi mpaka DRC.
Wiki iliyopita Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta,
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa Rwanda, Paul Kagame
walikutana Mombasa nchini Kenya na kuzindua mradi mkubwa wa ujenzi wa
reli.
Katika uzinduzi huo marais hao wameweka muda wa
kuanza kwa miradi mitatu mikubwa. Mosi kuanza kwa mradi wa ujenzi wa
reli kutoka Mombasa-Kampala mpaka Kigali, ujenzi wa bomba la mafuta
kutoka Eldoret-Kampala mpaka Kigali na kujenga miundombinu ya umeme wa
uhakika.
Pia wamewaagiza mawaziri wa fedha wa nchi hizo
kuandaa mapendekezo ya utekelezaji wa miradi hiyo mitatu na taarifa ya
mapendekezo hayo wanatakiwa kuitoa kwa marais hao katika mkutano ujao.
Wanazungumza lugha moja
Kwa mujibu wa mratibu wa miradi hiyo, Monique
Mukaruliza, ujenzi wa bomba la kusafisha mafuta kutoka Eldoret-Kampala
mpaka Kigali, unatarajiwa kukamilika 2017 huku kabla ya mwisho mwa
mwaka huu, viongozi wa nchi hizo wamekubaliana kuzindua ushuru wa
pamoja wa forodha kwa ajili ya kusafirisha bidhaa kwa masharti nafuu
kutoka nchi moja hadi nyingine.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa zinaeleza kwamba
ujenzi wa reli hiyo utagharimu Dola 3.5 bilioni, lakini taarifa nyingine
zinasema kwamba mradi huo una thamani ya Dola 13 bilioni na mradi huo
utakamilika mwaka 2018 huku ujenzi wa awali wa mradi wa reli kutoka
Mombasa mpaka jijini Nairobi unatarajiwa kuanza Novemba, mwaka huu.
Vilevile kuanzia Januari mwakani, Rais wa Kenya,
Kenyatta na Kagame wamekubaliana kwamba wananchi wao waanze kutumia
vitambulisho vya uraia kusafiria katika nchi hizo wakati Uganda itatumia
kadi ya kupiga kura kusafiri Kenya na Rwanda.
Mbali na hayo taarifa iliyotolewa hivi karibuni
imebainisha kwamba katika mkutano wa pili uliofanyika Mombasa wiki
iliyopita, marais hao waliwaagiza mawaziri wa fedha wa nchi hizo kuandaa
mapandekezo ya utekelezaji wa miradi hiyo ndani ya mwezi mmoja na nusu
ujao.
Wataalamu wa masuala ya uchumi, wanabainisha
kwamba reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo na kwenda kilometa 80
kwa saa wakati itakapoanza kusafirisha mizigo katika ukanda huo.
Bandari ya Mombasa, inategemewa kwa zaidi ya
asilimia 50 na Rwanda katika kuagiza mizigo huku ikitegemewa na Uganda,
Mashariki mwa Demokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Kaskazini mwa mikoa ya
Tanzania na Sudani Kusini.
Burundi na Sudani Kusini
Katika mkutano huo marasi wa nchi hizo tatu
walikubali kuijumuisha Burundi na Sudani Kusini katika miradi hiyo baada
ya kuhudhuria mkutano huo kama wageni waalikwa.
Kutokana na makubaliano hayo ni dhahiri kwamba nchi hizo tano
zimekubaliana kufanya kazi pamoja katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa
lengo la kuboresha maisha ya wananchi wa nchi hizo kiuchumi.
“Wawakilishi wa Burundi na Sudani Kusini wanapaswa
kuwa sehemu ya miradi hiyo na hasa katika kamati za ufundi,” inaeleza
sehemu taarifa ya mkutano huo.
Mukaruliza anabainisha kwamba Burundi na Sudani
Kusini walialikwa kwenye mkutano huo kama watamazaji na baadaye waliomba
kuwa sehemu ya kuanzisha miradi hiyo.
Katika mkutano huo Rais Kenyatta alitoa taarifa ya
maendeleo ya miradi hiyo baada ya mkutano uliofanyika Entebbe, Juni
mwaka huu.
“Ninayo furaha kutoa taarifa ya mradi wa bomba la
mafuta na katika hatua ya kwanza ya maendeleo ya mradi wa bomba la
mafuta, unaendelea vizuri na hatua ya awali tayari imeanza na upembuzi
yakinifu umekamilika,” anasema Rais Kenyatta.
Pia Kenyatta anasema kuna changamoto zinazokabili
nchi hizo na kwamba wanapaswa kuungana pamoja kwa ajili ya kuzitatua na
kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kuhusu hati za kuruhusu watu wa Jumuia ya Afrika
Mashariki kuingia katika nchi moja hadi nyingine, katika mkutano huo
suala hilo lilijadiliwa na mawaziri husika waliagizwa kutoa taarifa kwa
nchi ya Kenya, Rwanda na Uganda katika mkutano wa tatu utakaofanyika
Oktoba mwaka huu ili mpango huo uanze Januari mosi, mwakani.
Vilevile mawaziri husika wameagizwa kukamilisha
mchakato wa kutumia vitambulisho vya uraia kabla ya Oktoba, mwaka huu
ili vitumike kama hati rasmi kusafiria katika nchi hizo Januari mosi,
mwaka huu.
Katika mkutano huo, Rais wa Sudani Kusini, Salva
Kiir Mayardit aliwakilishwa na waziri wake wa masuala nje Dk Barnaba
Marial Benjamin wakati waziri wa usafirishaji wa Burundi, Deogratias
Rurimunzu alimwakilisha Rais Pierre Nkurunziza.
Mkutano mwingine utafanyika Oktoba mwaka huu jijini Kigali.
Tanzania
Mwishoni mwa Mei, Rais Jakaya Kikwete alipofanya
ziara nchini Japan aliiomba nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kugharimia
ujenzi wa reli mpya kutoka Tanzania kwenda nchi za Rwanda, Burundi
mpaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ombi ambalo Serikali ya
nchi hiyo ilikubali.
Rais Kikwete anasema ujenzi wa reli hiyo utarahisisha
usafirishaji wa mizigo wa nchi hizo ambazo zinaitegemea bandari ya Dar
es Salaam kusafirishia bidhaa zake.
Taarifa zinasema Kampuni ya Burlington Northern
Santa Fe Railway ya Marekani ndiyo itakayofanya ukarabati huo ambao
utahusisha ujenzi wa reli mpya kutoka Isaka hadi Kigali ambayo pia
itaunganisha Jiji la Bujumbura, Burundi.
Hata hivyo uzinduzi wa mradi wa reli ya
Mombasa-Kigali, huku Rwanda na Uganda zikitishia kujitoa kutumia bandari
ya Dar es Salaam unaacha maswali mengi.
source: Mwananchi
source: Mwananchi