29th September 213
Kisa alichelewesha mwiko wa kusongea ugali
Mtoto
 mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Zuhura (6), mkazi wa Lulumba, 
Wilaya ya Iramba mkoani Singida, amefariki dunia baada ya kumwagiwa maji
 ya moto na bibi yake.
Imedaiwa kuwa bibi huyo, Magreth Sombi 
(55), alimmwagia mtoto huyo maji ya moto baada ya kuchelewa kumpelekea 
mwiko wa kusongea ugali aliomtuma.
Akielezea kisa hicho, Mwenyekiti wa mtaa huo, Abel Seth, alisema tukio hilo lilitokea Jumanne iliyopita.
Alisema bibi huyo anadaiwa kumtuma mtoto 
huyo mwiko na alipochelewa alimmwagiwa mwilini maji ya moto yaliyokuwa 
yamechemka kwa ajili ya kupikia ugali.
"Kama haikutosha, Magreth kwa ushirikiano 
na mtoto wake, Naomi walimkamata kwa nguvu Zuhura na kutumbukiza viganja
 vyake vyote ndani ya sufuria iliyokuwa na maji yaliyochemka...mtoto 
aliungua sana na nyama zote kutoka..." alisema kwa masikitiko.
Aliongeza kuwa binti huyo alifariki dunia kesho yake (Septemba 25) wakati akipatiwa tiba katika hospitali ya wilaya ya Iramba.
Alisema baada ya binti huyo kufariki, 
Magreth alimtuma mtoto wake aliyemtaja kwa jina la Naomi kwenda nyumbani
 kwa mwenyekiti huyo kutoa taarifa ya kifo hicho bila ya kutoa taarifa 
kwa majirani wanaowazunguka.
"Nilipomhoji ni kwanini hajawajulisha 
majirani zao juu ya kifo hicho, alinionya kuwa nisiwaambie watu wengine 
wala majirani kwa sababu hataki watu wajue au waje warundikane kwake eti
 mwili wa Zuhura utachukuliwa na wazazi wake kwenda kuzikwa Singida 
mjini wakati wowote," alisema Seth.
Mmoja wa majirani wa karibu katika msiba 
huo, Elieza Mgwali, alisema msichana huyo ambaye ana miezi miwili tangu 
aanze kuishi na bibi yake alikuwa na wakati mgumu kutokana na mateso 
makubwa aliyokuwa anapata kutoka kwa mtuhumiwa Magreth.
"Mtoto ameteseka sana, alifanyishwa kazi 
nzito zilizo nje ya uwezo wake na mara nyingi alikuwa akinyimwa hata 
chakula...alikuwa anakuja kwetu na moja kwa moja anaingia jikoni 
kujichukulia chakula bila hata kuomba, tulishatambua mateso yake hivyo 
tulikuwa tunamruhusu ale mpaka ashibe," alisema Mgwali.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa mtaa huo, mtuhumiwa Magreth na mwanawe Naomi wanashikiliwa na polisi kwa  mauaji hayo.
Jeshi la polisi Mkoa wa Singida kupitia 
kamanda wake, Geofrey Kamwela, amekiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba 
taarifa kamili anatarajia kuitoa kwa wanahabari wakati wowote.
     CHANZO:
     NIPASHE JUMAPILI