Tuesday, 15 October 2013

Mtoto wa Nyerere avunja ukimya

Mtoto wa kwanza wa Hayati Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumanne,Oktoba15  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Asema viongozi wa sasa wameshindwa kufuata nyayo za baba yake, Mwalimu Nyerere na wapo hatua 20 nyuma.Pia anaamini vyama vya upinzani vinaweza kupata mafanikio dhidi ya CCM katika chaguzi zijazo ikiwa vitaungana kukikabili chama hicho tawala.


Mtoto wa kwanza wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aitwaye Madaraka, amesema viongozi wa sasa wameshindwa kufuata nyayo za kiongozi huyo kutokana na sababu ambazo amesema “haziko wazi”.
Katika mahojiano yake na gazeti hili, Madaraka anasema: “Mazingira ya sasa hayaruhusu malengo ya uadilifu kuenziwa kwa sababu nafasi za umma zinakubalika sasa kuwa ni maeneo ya kujinufaisha mimi kwanza, halafu Tanzania Mungu akipenda”.
Yafuatayo ni mahojiano kamili na Madaraka.
Mwananchi: Ni miaka 14 sasa tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, unaizungumziaje miaka hiyo kimaisha katika familia, bila kuwapo kwa Mwalimu?
Madaraka: Binadamu tumeumbwa na uwezo wa kukabiliana na kuondokewa ndugu na jamaa zetu wa karibu. Majonzi yalikuwa makubwa baada ya kufariki Mwalimu, lakini tunatambua kuwa kuna umuhimu wa kuomboleza na baadaye kuendelea kukabiliana na changamoto za kila siku za maisha. Na yeye angetarajia hivyo.
Mwananchi: Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa nchi, ni zipi fikra au mtazamo wako jinsi viongozi wetu wa sasa wanavyomuezi kwa kuwa wafuasi wa nyayo zake?
Madaraka: Hebu tuseme tu bila unafiki kuwa katika masuala mengi ya uongozi, hasa ya uadilifu, suala la kumuenzi Mwalimu Nyerere ni lengo ambalo viongozi wengi wa sasa wanaweza kuwa wanalo, lakini kutokana na sababu ambazo haziko wazi basi hilo lengo siku zote halikamatiki, liko hatua kumi mbele yao. Na kila wakielekea kama kulifikia na kulitimiza basi wanateleza na kuanguka na lengo hilo linawaacha hatua nyingine 20 mbele.
Mazingira ya sasa hayaruhusu malengo ya uadilifu kuenziwa kwa sababu nafasi za umma zinakubalika sasa kuwa ni maeneo ya kujinufaisha mimi kwanza, halafu Tanzania Mungu akipenda.
Mwananchi: Miongoni mwa mambo ambayo Mwalimu Nyerere aliyaenzi na kuyasimamia enzi za uhai wake, ni Muungano. Kwa maoni yako unadhani hili linaenziwa vipi? (rejea mvutano wa sasa wa Serikali mbili, tatu nk, unatokana na mchakato wa Katiba Mpya).
Mwananchi: Nitumie msemo wa kisiasa kuwa sasa hivi suala la kutengua Muungano linazungumzika. Wakati waasisi wenyewe wapo hai wale waliofikiria kutengua Muungano walipata kigugumizi au walishindwa kuwa wazi na fikra zao. Sasa hivi inaelekea kuna baadhi ya makundi ya viongozi pande zote mbili za Muungano hawataki Muungano, lakini wanashindwa kuwa wazi kutetea msimamo wao huo. Ni sauti chache sana utazisikia zikisimama bila kutetereka kutetea kuwepo kwa Muungano.
Ni dhahiri kuwa sauti za kutaka Zanzibar iachane na Muungano zimekuwa na nguvu zaidi kuliko zile ambazo zinatetea Muungano. Naamini kuwa viongozi wanaozungumzia Muungano wa mkataba hawajapata ujasiri wa kisiasa wa kusema kuwa hawataki kabisa Muungano.
Naweza kuwa siko sahihi, lakini naamini kuwa yeyote anayejaribu kutetea umoja mkubwa zaidi kati ya Bara na Visiwani na siyo mfano tu wa umoja anapingana na mtazamo uliojengwa juu ya fikra kuwa maendeleo ya Zanzibar yanakwamishwa na kuwepo ndani ya Muungano.

Kwa sababu ni baadhi ya wanasiasa ndiyo wanajenga fikra hizi tunaweza kusema kuwa ni siasa ndiyo inasukuma ukweli badala ya ukweli kusukuma siasa. Kwa maoni yangu, ukweli wa kisiasa unajengwa juu ya kushinda uchaguzi ujao.
Hilo ndilo jambo la msingi. Kusimamia ukweli tofauti na hapo kunaweza kusababisha kushindwa uchaguzi. Ukweli ninaoamini mimi ni kuwa siku zote umoja huleta nguvu, utengano udhaifu. Hii ni kweli katika suala la uchumi na hata kisiasa.
Lakini iwapo hilo ndilo wananchi wanataka, huwezi kulikwepa. Matokeo yake ni Serikali tatu. Umoja wa kweli ungekuwa Serikali moja na sauti za ‘mimi’ na ‘wewe’ (Zanzibar na Bara) zingepotea na kuchukuliwa na suala la ‘sisi’ (Watanzania). Lakini suala la Serikali moja lilionekana haliwezekani, mwaka 1964 na la Serikali mbili likaonekana mwafaka. Kwenda kwenye Serikali tatu ni kama kupiga hatua moja nyuma katika kuulinda Muungano.
Mimi nalaumu uwezekano wa kupatikana kwa rasilimali ya mafuta kama kichocheo kikubwa cha kuyumbisha Muungano. Siku zote pesa na utajiri ndiyo hugombanisha ndugu. Ndugu wenye utajiri wana fursa nyingi zaidi za kutoelewana kuliko ndugu wasio na utajiri.
Ukweli ni kuwa kama huna mali hutakuwa na ugomvi kuhusu mali na ndugu yako. Mara tulipopata harufu ya mafuta chini ya Bahari ya Hindi basi masuala ya kuukosoa Muungano yakapamba moto.
Mwananchi: Nje ya Serikali ambako Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi, kuna familia ambako alikuwa baba. Ndani ya familia je, mnamuenzi vipi Baba wa Taifa?
Madaraka: Ukiwa ndani familia huna uchaguzi juu ya kama unataka kumuenzi Mwalimu au la. Watu watakupachika matarajio yao na kiwango cha ulinganishi kimeshawekwa na Mwalimu Nyerere.
Kwa hiyo mwanafamilia anapokuwa na mwenendo ambao haufanani na hicho kiwango kinachotarajiwa, basi wengi wanashangaa. Mfano, mimi nikivuta bangi nitaandikwa kwenye gazeti, lakini kitendo hicho kikifanywa na Mtanzania ambaye baba yake hana wadhifa mkubwa wa uongozi hiyo haiwezi kuwa habari.
Labda wengine watasikitishwa na suala hilo. Watakaofurahi ni wale ambao wanakubali kuwa uadilifu katika uongozi na utumishi wa umma ni suala lisilowezekana.
Baadhi ya wanafamilia tunasimamia kutangaza Kijiji cha Butiama kama eneo la kihistoria na la kiutamaduni. Wageni wengi bado wanafika kutembelea Butiama mahususi kwa sababu ndipo alipozaliwa na kuzikwa Mwalimu Nyerere.
Mwananchi: Ni tabia ya viongozi wengi wa Afrika kujilimbikizia mali wanapokuwa madarakani. Ukiwa kiongozi wa familia ya Mwalimu Nyerere, unaweza kueleza tofauti yao na Baba wa Taifa? Je, yeye aliwaachia mali kiasi gani (kwa maana ya fedha, nyumba na mashamba)?
Madaraka: Awali, mimi siyo kiongozi wa familia ya Mwalimu Nyerere. Hatuna nafasi hiyo ndani ya familia.

Mimi naamini kuwa mtu ambaye hana tamaa ya kujilimbikizia mali huzaliwa hivyo. Huwezi kupenda kujilimbikizia mali na utajiri (kwa njia halali au vinginevyo) halafu ukakaa madarakani kwa miaka 23 bila tabia yako hiyo kujitokeza katika matendo yako au ya wale waliokuzunguka. Ukweli utabainika tu.
Sasa inawezekana kuwa kiongozi akashika wadhifa akiwa mwadilifu halafu akiwa madarakani akapata vishawishi vya kujilimbikizia mali.
Hapa ndiyo natoa hoja kuwa kama wewe ulizaliwa kuwa mtu usiyesumbuliwa na kukosa mabilioni ya shilingi kwenye akaunti yako basi hivyo vishawishi havitakusumbua. Lakini tofauti ya hivyo utashawishika kujitajirisha mwenyewe na kusahau wajibu kwa umma.
Sisi hatukuachiwa mali yoyote ambayo ilitokana na kipato chake. Kuna nyumba ile ya Msasani ambayo aliijenga kwa mkopo ambao hakuweza kuulipa wakati anastaafu na aliamua kuikabidhi Serikali, lakini Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi ilipitisha uamuzi wa kulipa au kufuta deni na akakabidhiwa nyumba. Kuna nyumba ndogo ambayo alijenga akiwa Rais, iko Butiama.
Vilevile, baada ya vita vya Kagera alijengewa nyumba na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambayo baadaye Serikali ilichukua jukumu la kuikamilisha. Awali, ni wanajeshi wenyewe walikuwa wanakatwa mishahara yao kuchangia ujenzi wa nyumba hiyo.
Nyumba nyingine ipo Butiama na alijengewa na CCM baada ya viongozi wenzake kuamua kuwa nyumba yake aliyojenga Butiama ni ndogo sana na haistahili kutumiwa na Rais wa nchi.
Alipewa eneo la shamba na Kijiji cha Buturu, jirani na Kijiji cha Butiama, ingawa kumekuwa na mbinu za kutaka kupora hilo shamba zinazoongozwa na baadhi ya viongozi wa zamani wa kijiji hicho.
Mwananchi: Novemba 2004, familia ya Baba wa Taifa ililalamikia Sheria ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa iliyopitishwa na Bunge, kwa hofu kwamba ingepoteza uhalali wa kumilikia baadhi ya mali za Mwalimu Nyerere. Ni kipi kinajitokeza kama changamoto tangu kupitishwa kwa sheria hiyo?
Madaraka: Jibu hili litakuwa refu kidogo kwa kuwa lina masuala mengi ndani yake. Mimi nilikuwa mmojawapo wa wajumbe wa kamati ndogo ya Serikali iliyoshiriki kwenye kazi ya kuchangia vipengele vya muswada wa ile sheria.
Nilikuwa ninaiwakilisha familia pamoja na dada yangu Rosemary. Kuna baadhi ya vipengele ambavyo tulipendekeza kama familia wakati wa kuandaa muswada na waziri mhusika alienda bungeni kutoa tamko tukiamini kuwa mapendekezo yetu yangekuwa sehemu ya sheria, lakini waziri alipofika huko hakuchukua mapendekezo yote kutoka upande wa familia.
Changamoto siyo nyingi, lakini kuna jambo la msingi ambalo nafikiri linahitaji kutolewa uamuzi haraka. Sheria inaweka wazi kuwa kazi ya kuwaenzi waasisi wa Tanzania ni jukumu la pamoja na kuwa yeyote anayemiliki kumbukumbu za Mwalimu Nyerere na za Sheikh Abedi Amani Karume ataendelea kumiliki hizo kumbukumbu, lakini atatarajiwa kushiriki kwenye kizitunza kwa mujibu wa sheria hii na sheria nyingine zilizopo.
Itaendelea kesho
 SOURCE: MWANANCHI