Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto nimekuwa nikizisikia, lakini huo ni 
upofu, mimi si mtu wa kutumika nina elimu yangu nzuri ya shahada ya 
kwanza ya utawala wa biashara, najua ninachokifanya ni kwa masilahi ya 
chama.
Samson Mwigamba 
            
Na Mussa Juma, Mwananchi
Posted Jumatatu,Oktoba28 2013 saa 8:31 AM
Posted Jumatatu,Oktoba28 2013 saa 8:31 AM
Kwa ufupi
Mwigamba asema kikao kilichomsimamisha hakina 
mamlaka, adai chanzo ni kudaiwa kutumiwa na Zitto; Mnyika apigilia 
msumari wa mwisho hukumu hiyo.
Arusha. Mwenyekiti wa Chadema 
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amepinga uamuzi wa kusimamishwa  kwa 
maelezo kuwa kikao kilichochukua uamuzi huo hakitambuliki kikatiba huku 
akikanusha tuhuma za kutumiwa na Naibu Katibu Mkuu,  Zitto Kabwe, 
kukisambaratisha chama hicho.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mwigamba alisema 
kikao ambacho kina mamlaka ya kumwajibisha ni Kamati Kuu baada ya 
kupokea tuhuma na kumsikiliza.
“Baraza la uongozi la Kanda halina mamlaka ya 
kunisimamisha uenyekiti, lakini kwa kuwa mimi bado ni mwanachama hai wa 
Chadema na sitahama Chadema, nitakaa pembeni ili chama kifanye uchunguzi
 wa tuhuma zangu nikiwa nje ya ofisi,” alisema Mwigamba.
Hata hivyo, alisema anakusudia kufafanua chanzo 
cha mgogoro wake na baadhi ya viongozi leo, baada ya kukabidhiwa 
kompyuta mpakato (laptop) na viongozi wa chama hicho ambao waliichukua 
ili kuifanyia uchunguzi.
 Akana kutumiwa na Zitto
Akizungumzia tuhuma za muda mrefu kuwa, amekuwa 
akitumiwa na  Zitto hasa kuelekea uchaguzi ndani ya chama hicho, 
alisema  wanaofikiri hivyo ni vipofu wa kisiasa.
“Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto nimekuwa 
nikizisikia, lakini huo ni upofu, mimi si mtu wa kutumika nina elimu 
yangu nzuri ya shahada ya kwanza ya utawala wa biashara, najua 
ninachokifanya ni kwa masilahi ya chama,” alisema Mwigamba.
Alisema kama angekuwa mtu wa kutumiwa sasa, 
angetumiwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye ana uwezo 
wa kifedha kuliko Zitto au Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa ambaye atakuwa
 mgombea wa urais wa chama hicho na ana uwezekano wa kushinda.
Alisema kabla ya tuhuma za sasa kwamba anatumiwa 
na Zitto, aliwahi kutuhumiwa pia na Zitto kuwa anatuhumiwa na Mbowe hasa
 kutokana na misimamo yake na kauli zake katika vikao na maeneo 
mbalimbali, lakini baadaye ilithibitika kuwa alikuwa na hoja za msingi.
“Mimi ni mwanachama hai wa Chadema na nimekuwa 
nikitoa maoni yangu si kama Mwenyekiti wa Chadema Mkoa. Nina uhuru wa 
kutoa maoni katika kuhakikisha chama changu kinashika dola,” alisema 
Mwigamba.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, 
Mchungaji Israel Natse alitangaza juzi kusimamishwa Mwigamba hasa 
kutokana na tuhuma za kukichafua chama hicho kwenye mitandao ya kijamii.
Kabla ya hatua hiyo, Mwigamba alipata kipigo 
kutoka kwa vijana wa Chadema  baada ya kutuhumiwa kurusha kwenye mtandao
 wa Jamii Forum   tuhuma za matumizi mabaya ya fedha ndani ya chama 
hicho akiwa ndani ya kikao cha Baraza la viongozi Kanda ya Kaskazini.
Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanaamini kuna uwezekano kuwa 
mgogoro katika chama hicho unatokana na vuguvugu la uchaguzi uliosogezwa
 mbele hadi mwakani.
Kuna wasiwasi huenda yakajirudia ya mwaka 2009 
wakati Zitto alipojaribu kuwania nafasi ya Mwenyekiti dhidi ya Mbowe na 
kuzua mvutano mkubwa ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, Zitto aliweka bayana kuwa hawezi kuzungumzia mambo hayo kwani hafahamu hata huo uchaguzi  wa ndani utafanyika lini.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mwenezi wa 
Chadema, John Mnyika alifafanua kuwa kikao kilichomsimamisha Mwigamba 
kilikuwa halali.
Mnyika alisema, hata hivyo, ikiwa Mwigamba 
hajaridhishwa  na hatua hiyo anapaswa kukata rufaa na siyo kulalamika 
kwenye magazeti.
Alisema kuwa Mwigamba anapaswa kusoma katiba ya 
chama hicho na kuelewa mambo ya chama yanamalizwa na kikao husika na 
siyo kwenye vyombo vya habari. 
“Kikao kile kinaweza kumsimamisha ila kama hajaridhishwa na uamuzi ule basi aende kwenye ngazi inayofuata,” alisema Mnyika.
Mnyika, hata hivyo, alisema kwa ngazi ya taifa 
wanasubiri taarifa ya kikao kilichomsimamisha kwani walikuwa hawajapokea
 na  wala kutumiwa malalamiko yoyote na Mwigamba.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI

