Wednesday, 30 October 2013

Mzazi adaiwa kulawiti, kubaka binti zake


Na Rehema Matowo,Mwananchi

Posted  Jumatano,Oktoba30  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Inadaiwa amekuwa akitenda kosa hilo kwa muda mrefu baada ya kukimbiwa na mkewe


 Marangu. Baba mzazi wa mabinti wawili mkazi wa Kijiji cha Kiria Kata ya Mamba Kusini, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, amewabaka na kuwalawiti binti zake hao wenye umri wa miaka 10 na 13 na kuwajeruhi vibaya.
Kitendo cha baba huyo kufanya unyama huo kimedaiwa kuwapandisha hasira kinamama wa kijiji hicho walioamua kumkamata na kumpeleka Kituo cha Polisi Himo huku wakitishia kumuua iwapo polisi watamwachia huru, kwa madai imekuwa ni kawaida yao kila akifikishwa kituoni hapo kuhusiana na unyama anaowafanyia watoto hao huachiwa.
Mwanamume huyo anadaiwa kuwa na tabia ya kuwatendea vitendo hivyo wanaye hao kwa muda mrefu, kutokana na ugomvi baina yake na mkewe uliosababisha mkewe akimbie na kuwaacha watoto hao na baba huyo.
Akizungumza Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiria, Doroth Mtui, alisema taarifa hizo alizipata kutoka kwa majirani wa watoto hao, ambapo mtoto mmojawapo alimweleza kwa undani juu ya ukatili huo na baadaye walimkamata mwanamume huyo na kumpeleka Kituo cha Polisi Himo.
Alisema walipofika kituoni, walitakiwa kumpeleka mtoto huyo hospitalini ili kuthibitisha kama kweli amebakwa.
Taarifa iliyotolewa na daktari wa Hospitali Teule ya Kilema, ilionyesha mtoto huyo kuharibiwa sehemu zote mbili na kwamba kitendo hicho kimekuwa kikifanyika kwa muda mrefu.
Mtui alidai kuwa mwanamume huyo, alikuwa akiishi na watoto hao wawili ambao aliwatumia wote kwa zamu na kwamba mtoto mdogo, alifanikiwa kutoroka na mpaka sasa hajulikani aliko, aliendelea kumtendea ukatili huo mtoto aliyebaki huku akimtisha kumuua iwapo atatoa siri hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi wamekamilisha uchunguzi na huenda mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote.

SOURCE: MWANANCHI